jk akizungumza na Bw.Daniel Cooper (pili kushoto) na Bw. Tom Veegh (shoto) mambao ni sehemu ya ujumbe wa barlington Northern Santa Fe ambapo walizungumzia juu ya suala la ujenzi wa Reli kati kuanzia Isaka (Tanzania) hadi Kigali (Rwanda) ikulu,k dar, leo. habari kami8li soma chini hapo.
Ujenzi wa Reli kuunganisha Tanzania na Rwanda kuanza mwakani


UJENZI wa reli kuunganisha Isaka, Tanzania na mji mkuu wa Rwanda, Kigali umepangwa kuanza mwakani, Rais Jakaya Kikwete ameambiwa leo.

Ujumbe wa kampuni ya Barlington Northern Santa Fe (BNSF) kutoka Marekani pia umemwambia Rais Kikwete kuwa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika 2013.

Ujumbe huo pia umemwambia Rais kuwa kazi ya ujenzi wa reli hiyo mpya, utakwenda sambamba na matengenezo makubwa na upanuzi wa Reli ya Kati, kati ya Isaka na Dar es Salaam.

Upanuzi huo utalenga kuiwezesha Reli ya Kati kufikia kiwango cha kimataifa cha reli, kuongeza nguvu ya reli hiyo kuweza kubeba mabehewa zaidi, na kubeba mizigo mikubwa zaidi na kupunguza muda wa safari.

Katika mazungumzo kati ya ujumbe huo na Rais Kikwete, Ikulu, Dar Es Salaam, ujumbe huo pia umemwambia kuwa mahitaji yote muhimu kwa ajili ya ujenzi wa reli kati ya Isaka na Kigali karibu yanakamilika.

Ujumbe huo ulikuwa ni pamoja na Daniel Cooper na mashirika wake, Tom Vegh kutoka kampuni ya masuala ya fedha ya Fox River Financial Resources, ambayo inahusika na masuala ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo, pamoja na John Orrison kutoka kampuni ya BNFS.

Mazungumzo hayo pia yamehudhuriwa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji; Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa.

Wakati maandalizi yanaendelea kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Isaka-Kigali, na upanuzi wa Reli ya Kati, maandalizi pia yanafanyika kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa ujenzi wa reli kati ya Isaka-Kigali-Bujumbura.

Mbali na hiyo, mipango pia inaandaliwa na kuangalia uwezekano wa kuunganisha Isaka na mji wa Mwanza, na kuunganisha Tabora na Kigoma kwa reli bora zaidi.

Rais ameuelezea ujumbe huo kuhusu furaha yake kusikia habari hizo, na kusema kuwa Serikali yake inaiunga mkono mipango hiyo kwa “asilimia 150”

“Ujumbe wangu ni mfupi tu – tunataka njia ya reli. Na tunaunga mkono juhudi zenu asilimia 150,” Rais ameuambia ujumbe huo.

Rais pia ametaka kuangaliwa kwa uwezekano wa kuunganisha Reli ya Kati na Reli ya TAZARA, na hivyo kuwezesha mizigo kutoka kusini mwa Afrika kusafirishwa hadi Tanzania, na mizigo ya majirani wa kaskazini wa Tanzania kusafirishwa kwa urahisi kwenda kusini mwa Afrika.

Ameuambia ujumbe huo kuwa upanuzi na matengenezo makubwa katika Reli ya Kati utakwenda sambamba na upanuzi mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam.


Ikulu
Dar es Salaam
25 Januari, 2008

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Mimi ninafurahishwa sana na habari hii. Utafiti wangu wa haraka haraka (google) umedhihirisha kwamba kampuni ya BNSF ni ya maana sio kama Richmond. Jamaa wa Richmond ni wezi tu. Hamna lolote. Sijui ni waarabu au wahindi wale. Vyovyote vile ni wababaishaji tu. Heri wajapani, wachina au wazungu. Maana yake walahu kazi itafanyika hatakama pesa italiwa.

    ReplyDelete
  2. Duh Reli kati ya Tanzania na Rwanda, sasa hao wazungu sijui wa nini hapo. Au utaalamu wa kujenga reli pia hatuna? Kama ndo hivyo funga vitivo vyote vya Engineering katika vyuo vikuu huko bongo maana havina faida yoyote.

    ReplyDelete
  3. Hii Serekali vipi?? Mnaacha Kujenga madaraja vivukoni kama kigamboni na mito kibao inayowapa tabu Raia wa TZ mnaenda kutuletea wakimbizi na majangiri wa kirwanda kwa kuwapa access kilaiini kuja Kuchota vya watu? Alhamdullilah Mi Mungu aliniondoa mapemaa Inji Hiyo. Ila nasikitika sana Kwamba viongozi wanafanya maamuzi kuelekea NYUMA badala ya kwenda Mbele. Nchi Ina usafiri wa ajabu ile mbaya.. Inaenda kujengwa reli ya mabilioni Kwenda Nchi ambayo mwisho ni kututegemea na sio sisi kufaidika au kufaidishana. Hivi TAZARA Inaingiza Nini Nchini na kama vinaingia vinaishia wapi .. manaake tunajua huku kwa wwalioendelea huduma moja ikiwa inaleta mapato inasaidia na huduma Nyingine.. Sasa hizo huko vipi?
    Ee Mungu Eeep Iokoe Nchi yetu inazama hii.

    ReplyDelete
  4. Kwa kuangalia haraka haraka hiyo picha Kikwete anatibua. Wote hao suti zinafanana na soksi na kwamba wamevaa suti. Yeye anavaa bleza na shati lake la zambarau. Hivi kwani huyu bwana mkubwa hana washauri angalau wa mavazi maaana hizi staili zake za wanamuziki haziendi kabisa na hadhi yake kama raisi. Nadhani ndio maana watu wanafanya mikataba ya kupunda punda kwa sababu mh. hajaa kama mtu mwenye mamlaka.
    shs.0.02

    ReplyDelete
  5. Walalama mmerudi tena! sasa huku mwalalama reli kujengwa huku tena mwalalama hakuna maendeleol. Sasa maendeleo bila ya miundombinu yatakujaje?

    Mara nyingine mwalalama kuwa bandari ya Salama inapigwa kumbo na bandari ya Mombasa, sasa mnafikiri hiyo bandari salama bila reli ya kuwezesha kusafirisha hayo makontena ya mizigo ya nchi zisizo bahari itafanyaje kazi.

    Hebu acheni tabia za kitoto za kulalamikia kila kitu wala sio sifa. Kama mambo ya miundo mbinu na uchumi hamjui kaeni kimya. Na hao mainginia wa bongo watajenga reli bila pesa! Walalama mpooooooo??

    ReplyDelete
  6. wewe mdau wa 5;35 huna akili kabisa na huelewi na kabla ya kuropoka bora siku nyingine uulize na ndio maana umekimbia nchi uko kwa watu unadowea dowea tuu,eti reli ya kubeba majambazi na wataishia kututegemea,akili yako ndogo sana...ngoja nikueleweshe kidogo tuu,hiyo reli itafanya nchi nzima ya Rwanda watumie bandari ya dar kwa 100%,can you imagine mizigo ya nchi nzima inapita bongo na kuripiwa kodi?wewe unafikiri nchi itatengeneza kaisi gani?na hizo barabara na madaraja ya kigamboni yatajengwa kirahisi sana kama tukikusanya na kutumia kodi vizuri,naq huu mradi ukikamilika ndio kitu kikubwa kabisa kinachoingiza pesa tulichofanya kwa miaka mingi sana naongelea billions of shillings...next time acha ujinga!

    ReplyDelete
  7. Hao ni makaburu tu hao wanataka kutuletea matatizo. Hao watu toka hiyo nchi jirani wakianza kufurika tza watachukua uongozi na kuleta matata.
    Usimwamini mzungu yeyote anayesema ataleta maendeleo bongo. Huyo ni jambazi ataiba rasilimali zote ajengapo.
    Hawa ndio maadui wa uhuru.
    Waliyafanya ya kutisha ktk nchi hizi kwa kuwaweka kwenye madeni makuu. Je sisi wabongo watatufanyaje???
    http://www.prothink.org/2007/12/jewish-role-in-african-slave-trade_29.html,
    http://video.google.com/videoplay?docid=-1583154561904832383,
    http://video.google.com/videoplay?docid=-7336845760512239683
    Haya shime hebu tueneza ukweli huu.

    ReplyDelete
  8. Mzee uko nyumbani?,ahh...tulidhani umesafiri ili ukajipumzishe baada ya ziara kabambe vijijini huko kagera!!!jamani wako wataalamu popote wanaoweza kutuambia kwamba 'Air miles'ngapi Mzee huyo wa ikulu amekujisanyia?

    ReplyDelete
  9. mzee michuzi ni bahati nzuri blog hii ina wajinga wachache tu kama huyo 5.35.hiyo haijengwi na serikali ya Tanzania ulizia vizuri.unaita wenzio majambazi angalia uchumi wao umefika wapi,na ni juzi tu kulikua na genocide.uliza michuzi kafika huko atakueleza.tanzania bado inahitaji majirani .

    ReplyDelete
  10. Mi ni truck driver hapa US and A. Kama hiyo kampuni BNSF watajenga reli Tanzania, tegememea kitu kweli kweli. Bila kufanya uchunguzi wowote, naamini zaidi ya 80% ya reli za mizigo za hapa marekani wanazimiliki hao jamaa. Hata mabehewa karibu yote ya mizigo yana hiyo chata ya "Santa Fe" au B. Northern. Ila kwa bongo wamekula bingo mbaya. Huku ardhi inamilikiwa na watu binafsi na kujenga reli lazima kunakuwa na vikwazo si mchezo. Kwetu ardhi nje nje. Lakini taifa litafaidi naamini. Peace!

    ReplyDelete
  11. Kwanini sisi hatuna uwezo wa kutengeneza reli zetu wenyewe?

    ReplyDelete
  12. Duu...hii kubwa hatuna pantoni za kusafirisha watu Kigamboni twafikiria kuweka reli na Rwanda!Yaani nchi ina vituko kila kukicha!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...