Tanzania yaombwa kujaribu aina mpya ya msaada duniani
.
JK akubali kimsingi, ili mradi usiingilie misaada ya sasa
. Sekta ya Elimu yalengwa kama eneo mwafaka la kuanzia
Na Mwandishi Maalum, Washington, Marekani

Tanzania imeombwa kuwa nchi ya kwanza duniani kujaribu aina mpya ya msaada unaojulikana kwa jina la Cash on Delivery na unaolenga kuzawadia mafanikio ya dhahiri katika huduma za kijamii, bila kugusa misaada ya sasa katika huduma hizo. Tanzania inaombwa kuanzia na sekta ya elimu.

Kwa mujibu wa mjumbe maalum wa Dk. Nancy Birdsall, Rais wa Kituo cha Maendeleo Duniani cha Center for Global Development (CGD), chenye makao yake mjini Washington D.C., Marekani, aina hiyo mpya ya msaada inalenga kuchangia na kuongeza thamani katika misaada ya sasa katika huduma za kijamii.
Mjumbe huyo amesema kuwa mpango huo, mbali ya kuongeza misaada zaidi kwa nchi husika, pia unaziruhusu nchi zinazopokea misaada kuamua mipango yake ya maendeleo, na hivyo kuondoa nguvu ya nchi fadhili katika maamuzi ya mipango hiyo, ili mradi nchi husika ithibitishe kuwa imepata mafanikio yanayothibikika katika sekta yoyote ya kijamii.

Amesema kuwa tathmini ya kuamua ni mafaniko kiasi gani nchi imefikia katika sekta yoyote, yatafanywa na kundi la watu wanaojitegemea, na wala siyo wafadhili kama ilivyo kwa mipango ya sasa ya misaada.

Mjumbe huyo amemwambia Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa kituo hicho kinaiomba Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kubeba jukumu hiyo, kwa sababu ya mafaniko makubwa ambayo Tanzania imeyapata hasa katika elimu na katika huduma za jamii kwa jumla.

Katika mkutano kati ya mjumbe huyo na Rais Kikwete kwenye Hoteli ya Omni-Shorem mjini Washington D.C., leo (Jumamosi, Septemba 27, 2008) CDG linasema kuwa mpango huo unalenga kuzawadia mawazo mapya na ubunifu katika kuwapelekea wananchi huduma za kijamii.

“Chini ya mpango huu, nchi inahukumiwa kwa mujibu wa utendaji wake, na fedha inaongezwa katika jitihada za maendeleo ya nchi hiyo kwa mujibu wa kigezo hicho, bila wafadhili kuweka masharti yoyote, na wala kuingilia maamuzi ya nchi husika katika mipango yake ya maendeleo,” amesema mjumbe huyo.

“Tanzania mmefanya vizuri mno kiasi cha kwamba sisi katika CGD tunaamini kuwa mnayo haki ya kuwa nchi ya kwanza kufanyiwa majaribio ya mpango huo mpya wa misaada duniani. Kumbuka, hakuna hata senti moja itachukuliwa katika misaada ya sasa. Hii ni nyongeza tu ya msaada ya sasa,” amesema mama huyo.

Amesema kuwa elimu ni sekta nzuri kuanza nayo katika Tanzania kwa sababu ya mafaniko yasiyokuwa kifani ya Tanzania katika sekta ya elimu.

Mbali na mipango ya Mpango wa Elimu ya Msingi (MEM) na Mpango wa Elimu ya Sekondari (MES), Tanzania imepata mafaniko makubwa katika miaka miwili iliyopita.

Katika miaka miwili iliyopita, Tanzania imejenga sekondari nyingi zaidi kuliko zilizojengwa katika miaka yote 44 iliyotangulia baada ya Uhuru, ikiwa imeongeza kiwango cha sekondari kwa asilimia 200.

Pia katika kipindi hicho, Tanzania imeongeza kiwango cha wanafunzi wanaoingia sekondari kwa zaidi ya theluthi mbili, na kwa wastani, Tanzania imejenga sekondari moja kila siku tatu katika kipindi hicho katika utendaji ambao pengine unavunja rekodi ya dunia.

“Elimu ni sekta nzuri ya kuanza mpango huo, na Tanzania ni nchi inayofaa zaidi duniani kwa ajili ya kufanya majaribio ya mpango huu. Kwa hakika, baadhi ya wafadhili tayari wamekubali kugharimia aina hii mpya ya misaada, na tunakuombeni Tanzania mkubali kuwa nchi ya kwanza kujaribu mpango huu,” amesema mama huyo.

Rais Kikwete, baada ya kuwa amesikiliza maelezo ya mama huyo, amesema kuwa Tanzania itakubali kujaribu mpango huo kama nchi ya kwanza duniani ili mradi tu shahaba za mpango huo ziwe wazi, na zisilenge kupunguza misaada ya sasa katika elimu.

“Nimesikiliza, na sasa nimeelewa. Kama mpango huu unalenga kuzawadia mafanikio, hiyo ni sawa kabisa. Hatutaki mpango huu utuhukumu kabla ya hatujafanikiwa kumaliza ujenzi wa shule nchini, na kama mpango huo haugusi uwekezaji wa sasa katika elimu ya watoto wetu katika Tanzania, basi hakuna taabu.”

“Kama hizi ni fedha za nyongeza, na wala siyo fedha za mpango wa awali kuwekeza katika elimu, kama ni fedha za kuzawadia utendaji, basi hakuna taabu.”

Mama huyo baadaye amemwomba Rais Kikwete, katika nafasi yake kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kufikiria uwezekano wa kuandaa mkutano wa nchi nyingi zaidi za Afrika, ili ziweze kuelezwa kuhusu mpango huo baada ya kuwa umeanza katika Tanzania.

Rais Kikwete aliyekwenda Washington D.C. kwa siku mbili katika ziara yake katika Marekani kuhudhuria Kikao cha 63 cha Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), amerejea mjini New York usiku wa leo, tayari kujiandaa kwa safari ya kurejea nyumbani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Habari njema Mh. Rais na tuanze huo mradi wa kuzawadia halmashauri zinazotoa elimu bure kwa wanafunzi kama katika halmashauri za Tarime chini ya Chadema.

    Nasema hivyo kwa sababu halmashauri zilizo chini ya vyama pinzani zimeonesha umakini katika matumizi ya mapato yatokanayo na mapato toka halmashuari zao na pia kwa fedha zitokazo serikali kuu.

    ReplyDelete
  2. Pongezi Rais Jakaya Kikwete, juhudi zinaonekana na tunategemea utekelezaji mzuri toka kwa wasaidizi wako pamoja nasi wananchi. Usisikilize kelele za wapinga maendeleo kuhusu safari zako za kikazi. Mungu akupe muono na afya njema.
    Mwananchi, Dar

    ReplyDelete
  3. MISAADA MINGI HUWA INAISHIA KWA MA MIDLEMAN HAWA WATU WA KATIKATI HUWA WANATUMIA ZAIDI YA NUSU YA MIASAADA KAMA GHARAMA ZA MALIPO KWA WAO WENYEWE KUWEZESHA HIYO SHUGHULI. KITU MUHIMU HAPO NI KUWA NAWATANZANIA WENYEWE AMBAO WAKO TAYARI KUTOA MCHANGO WAO WA HUDUMA KWA JAMII KAMA SADAKA HUKU TUKI MSUBIRI MUNGU ATUSHUSHIE NEEMA BAADA YA KUHAKIKISHA KWAMBA TUNAWAJALI WAJA WAKE/ WATU WAKE. VINGINEVYO UMASIKINI UTAZIDI KUJIKITA NA BARAKA ZITAZIDI KUJIFUNGA.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...