Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda akisalimiana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi , Dk.. Yves Sahinguvu, kabla ya mazungumzo yao katika Kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika, Caribbean na Pasifiki (ACP) jijini Accra.

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Tanzania itaendelea na taratibu za kurejesha asilimia 20 ya wakimbizi waliokubali kurejea makwao kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR).

Ametoa kauli hiyo jana jioni na usiku kwa nyakati tofauti alipokutana na Makamu wa Rais wa Burundi, Bw. Yve Sahinguvu; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Congo-DRC, Bw. Nkurlu Kilombo na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Rwanda, Bi. Monique Nsanza-Baganwa kwenye ofisi za Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Accra (AICC).

Waziri Mkuu Pinda ambaye anahudhuria Mkutano wa Sita wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika, Caribbean na Pasifiki akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete alitumia fursa hiyo kuwaita viongozi wa nchi hizo tatu ili apate mawazo yao na mtazamo wao kuhusu Tanzania inavyolishughulikia suala la kurudisha wakimbizi na hali ya usafirishaji wa mizigo yao kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumzia suala la wakimbizi, Makamu wa Rais wa Burundi alisema zoezi hilo linaendelea vizuri lakini akakiri kwamba kazi waliyonayo ni kubwa kwa vile kila wiki wanapokea wakimbizi wapatao 3,000wanaorejea makwao.

« Tunapowapokea jasho linatutoka, kwa sababu watu 3,000 ni wengi [WINDOWS-1252?]mno… kuwatafutia malazi, mavazi, chakula, dawa na hasa watoto wapate shule za kusoma ni kazi [WINDOWS-1252?]hasa… inabidi tupewe muda tujipange upya, » alisema.

Alisema anaiomba Serikali ya Tanzania iwape walau miezi sita zaidi baada ya muda wa makubaliano kuisha ambao ni Desemba, 2008 ili waweze kukamilisha vizuri zoezi hilo la sivyo watajikuta wanafungua makambi mengine ndani ya Burundi.

« Nia ya kuwarejesha nyumbani ni kuwafanya wapende kukaa nyumbani, tusipokuwa makini na kuwarudisha kiholela wakajikuta wanafikia tena kwenye makambi zoezi zima linaweza kuharibika, » alisema Bw. Sahinguvu ambaye muda wote alikuwa akizungumza Kiswahili.

Hata hivyo, alikiri kuwa tatizo ni kubwa zaidi kwa wakimbizi waliongia nchini miaka ya 1965 na 1972 kwa sababu wanaporudi inakuwa vigumu kupata mali zao au ndugu zao tofauti na wale wa mwaka 1993 ambao wengi waliweza kukuta baadhi ya ndugu na mali bado zipo japo kuna ambazo zilikuwa zimechukuliwa na wengine.

« Kwa wale ambao wanakuta mali zao zipo lakini zimechukuliwa, tumekubaliana kuwa tunagawanya nusu kwa nusu na waliozichukua na wengi wamekuwa wakiridhika na uamuzi [WINDOWS-1252?]huo… wale wa mwaka 72 baadhi wamekuta ndugu zao lakini wale wa mwaka 1965 ndiyo tunapata nao taabu zaidi kwa sababu hakuna dalili za kukuta mali zao au ndugu [WINDOWS-1252?]zao… hawa bado tunawatafutia maeneo mapya na kuwapangia waende huko kuanza upya maisha, » alisema.

Kuhusu usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam, Makamu huyo wa Rais alikiri kuwa hali sasa imebadilika na kwamba usumbufu umepungua.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara wa Rwanda, Bi. Monique Nsanza-Baganwa akigusia suala la wakimbizi, alimweleza Waziri Mkuu kuwa zoezi la kurejesha wakimbikizi lilianza lakini halikukamilishwa tangu lilipokwama mwaka 2006.

Alisema wengi wa waliokuwa wakirejeshwa walikuwa wakidai wao ni Watanzania na hivyo, ameiomba Serikali ya Tanzania iwasilishe Rwanda taarifa ya kupitia upya majina ya wakimbizi ili zoezi hilo lianze tena.

Kwa upande wao, mawaziri wa Congo-DRC na Rwanda walimweleza Waziri Mkuu kwamba usafirishaji wa mizigo umebadilika lakini wakaomba taratibu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za kutoza kabla ushuru wa bidhaa zinapokuwa njiani (on-transit fees) uangaliwe upya kwani unawaumiza.

Bw. Nkurlu Kilombo wa DRC-Congo alisema kwamba TRA ina utaratibu wa kuwatoza ushuru huo mizigo inapowasili lakini wakifika huko wanatozwa tena na nchi zao na wanapodai kurudishiwa fedha zao inawachukua zaidi ya miezi sita kabla hawajapewa.

Waziri Mkuu Pinda alisema TRA ilianzisha utaratibu huo kwa sababu kuna baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakidanganya kwamba mali zao zinapitishwa tu Tanzania lakini hawazifikishi kituo cha mwisho (terminal point) na badala yale wanazishusha njiani na kuzirudisha tena Dar es Salaam kuja kuziuza.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameahidi kumuagiza Waziri wa Fedha aitishe kikao cha Makamisha Wakuu wa TRA kwa nchi zote zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam ili wakae na kutafuta njia bora zaidi ya kudhibiti ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya wafanya biashara bila kuathiri nia njema ya wale wazuri.

Mkutano huo wa ACP umemalizika leo jioni na Waziri Mkuu anatarajiwa kuwasili nchini kesho (Jumamosi) mchana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. swali langu moja tu ni hili kwanini serikali iingie gharama ya kuwatudisha na kurudisha mizigo yao? kwani walivyokuja walikujaje na nani aliwaingizia mizigo yao huku kwetu?

    Tunajitaji kuwa na laws nadhani kwa nchi yetu....kama hali imerejea kuwa nzuri kwa basi warudi nchini kwao. Tumeishi nchi za nje na kufuata sheria zao ...muda ukiisha tunajirudia kwetu sasa kwanini hawa nao wasipewe muda fulani wa kurudi kwao?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...