WAZIRI MKUU Mh. Mizengo Pinda kesho (Jumatatu, Oktoba 06, 2008) anaenda nchini Namibia kwa ziara ya kiserikali ya siku nne kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bw. Nahas Angula.

Waziri Mkuu ambaye anafuatana na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Celina Kombani, Mbunge wa Mpwapwa, Bw. George Lubeleje na Mbunge wa Gando, Bw. Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), mara baada ya kuwasili jijini Windhoek, atafanya mazungumzo ya kiserikali na mwenyeji wake na jioni atashiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Jumanne atakutana na Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Dk. Sam Nujoma na baadaye kutembelea kiwanda cha kukata almasi cha NamCot na kisha kiwanda cha kusindika nyama cha Meatco. Jioni atakutana na Watanzania waishio Namibia.

Jumatano atakwenda Walvis Bay kuangalia shughuli za uvuvi na usindikaji wa samaki katika kampuni ya Melrus Sea Food Processing na baadaye kuzuru miradi ya umwagiliaji maji.

Alhamisi atakwenda Ikulu ya Namibia kukutana na Rais wa nchi hiyo, Hifikepunye Pohamba halafu atatembelea makao makuu ya chama cha SWAPO na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho. Pia atakutana na wanafunzi ambao zamani walisoma Tanzania.

Waziri Mkuu na msafara wake wanatarajiwa kuondoka Namibia Ijumaa, Oktoba 10, mwaka huu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
DAR ES SALAAM
05.10.2008

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...