ndugu, jamaa na marafiki katika kumeremeta kwa cappo na mara ambapo michango yao iliyofikia euro 4,000 (kama milioni 7 hivi za madafu) ilipelekwa kusaidia yatima huko iringa katika kituo cha watoto cha makalala.
mtarajiwa alipokuwa makalala mwaka jana akipozi na watoto yatima

Cappo na Mara walimeremeta kikawaida kabisa. pesa ya kununulia nguo za kumeremetea walichangia watoto yatima makalala

SHEREHE YA HARUSI YA KAWAIDA KABISA NIA NA MADHUMUNI NI KUCHANGIA KITUO CHA WATOTO YATIMA CHA MAKALALA-IRINGA-TANZANIA. NAPENDA KUWASIMULIA WADAU KUHUSU HABARI HII KAMA IFUATAVYO.

Rafiki mmoja wa hapa Cesena Davide Capponcelli a..k.a (Cappo) ambaye aliamua kufunga ndoa na mtarajiwa wake Mara Tani, mnamo tarehe 15/08/2009 na kuifanya sherehe yake kuwa ya kawaida kabisa bila makuu, lengo lake lilikuwa ni kuchangia kituo cha watoto yatima cha Makalala Children's Home kilichopo Mafinga-Iringa.

Kabla ya sherehe hiyo waliamua yeye na mtarajiwa wake Mara, kuwatangazia wanadungu na marafiki zao wote kuwa; wasiwazawadie chochote bali zawadi na michango yao yote ielekezwe kwa hawa watoto yatima ambao kweli wanahitaji msaada sana, hasa wa afya bora, elimu bora, malezi bora, chakula bora, n.k. kwa kukosa wazazi wao na watu wa kuwatunza.
Cappo alifikiri jambo hili la kuwasaidia watoto hawa baada ya kuona haya mwaka jana alipo tembelea kituoni hapo Makalala, na alisema kwanini kufanya sherehe ya kifahari wakati watu wengine wanahangaika na kuhitaji misaada mbalimbali ya kimaisha? -Kwa bahati mbaya sana sikuweza kuhudhulia sherehe hiyo, kwasababu kipindi cha sherehe hiyo nilikuwa likizo nyumbani Tanzania.

Lakini nimemshukuru sana kwa kuonyesha upendo wake mwingi kwa hawa watoto yatima wa nchini kwangu wasio na wazazi, jambo hili limenigusa sana moyoni mwangu, na ndio maana nimependa hata wengine wajue, kwa kuchukua uamzi wa kuiandikia barua blog hii ya Jamii, ili kuwaelezeni wadau wote jambo hili lililo nigusa sana, ili nasi tulio wengi tuinge mfano huu, na kama wapo wengine tayari walishafanya hivi kama huyu jamaa, basi nawapongeza sana na kuwashukuru kutoka moyoni mwangu kwa ukweli.

Harusi ya huyu rafiki alifanikiwa kuchangisha Euro 4000 ( kama Shilingi milioni 7 za madafu) ili kuwawezesha hawa watoto kwa mambo mbalimbali, ni jambo la kushukuru sana.
Basi nasi tufanye sherehe zozote zile si za harusi peke yake, bali sherehe zote zile ziwe za kawaida nzuri bila kupitiliza kiwango kuliko kawaida, kwa kutumia fedha nyingi ili kujionyesha tu kwa watu, na baadae tunajikuta hata sisi wenyewe washerehekea kesho yake tupo kwenye madeni na matatizo mbalimbali, sasa faida yake ni nini?

Shukrani zangu nyingi kwa huyu rafiki na wadau wote hapa wa blog ya Jamii, na Tanzania kwa ujumla ambao labda tayari walisha onyesha tendo kama hili la upendo wao mwingi kwa kutumia sherehe zao muhimu kwa kuwakumbuka hata na wengine walio na shida za kimaisha ambao tunaishi nao humu humu mitaani na kila siku tonaona walivyo na shida kweli hata kunywa maji tu kunashindikana.

Wito wangu ni kwamba na tufanyage sherehe nzuri za kawaida, si za kupita uwezo wetu, na zakuonyesha ufahari, bali zinazo kubalika katika jamii na mazingira yetu.Kwa habari zaidi na picha zaidi unaweza kutembelea hapa:

Asante sana kwako Mkuu Michuzi na wadau wote wa blog ya jamii, ninawasalimu sana!

Ni mimi yule yule wa siku zote:
Mdau Baraka wa Chibiriti.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. Hakika Cappo na Mara wametuonyesha njia sisi Watanzania ambao kwa ujumla tunafanya mambo mengi ambayo yanakuwa kufuru hata kwa Mwenyezi Mungu. Hawa ni watu baki je sie wahusika wenyewe tumefanya nini kwa ajili ya jirani zetu na ndugu wenye shida kama wajane na yatima? Maharusi ya kifahari tuache hiyo pesa itumike kuboresha hali za maisha za jamii. Utakuta hata maharusi wenyewe wanachangiwa pesa tele zinaliwa siku moja kesho yake wako kwenye madeni makubwa bila sababu. Nadhani kuna haja ya kubadilika. Heko Cappo na Mara.

    ReplyDelete
  2. Hii ni nzuri sana. Changamoto nzuri saaana hii.

    Nilikua natafuta idea za birthday ya mwanangu mwakani na hii imenipa changamoto... Najua nikiandaa na kutangaza mapema, wazazi wa watoto wanaoenda preschool na mwanangu watajitolea kwa moyo sana...

    Thanks to Coppa and Mara...Mungu awazidishie

    ReplyDelete
  3. Job well done Chibiriti.Naamini ume-play part kubwa saana kwa huu msaada kufikia walengwa. Huu ni mfano wa kuigwa kwani huu ndo mwanzo wa maendeleo.

    Hongera Chibiriti.

    ReplyDelete
  4. poor us!
    inabidi watu watoke ng'ambo hata kutuonyesha hili tatizo la maharusi yetu ya kifahari yasiyokuwa na maana yeyote!

    ReplyDelete
  5. Coppa na Mara wamefanyajambo moja lakipekee ambalo sinabudi kuwapongeza sana, mungu awazidishie na awajaalie maisha mema na yaupendo.

    ReplyDelete
  6. SWADAKTA ! Kama ambavyo tuzo (michango)wakati wa harusi yetu tulivyoamua kuipeleka katika Chuo cha Uuguzi huko nyumbani. Mnuso wa harusi yetu ulikuwa na watu wasiozidi 25 na hakukuwa na matumizi ya kamati ya usafiri (mafuta ya magari ya kukodi)na sijui kulipia gharama za siku ya kuvunja Kamati kwikwi!!

    ReplyDelete
  7. Chibiriti,
    Asante kwa changamoto hii, kumbe si bure unatumia komptyuta ya 1947.

    Lakini sana Chibi ndo unataka sisi tufe na njaa, maana harusi sie ndo tunapata tenda na hela, ukiwabadilisha wadau itabidi tutafute mradi mwingine.

    Ila kweli tufanye sherehe kulingana na mazingira yetu, yaani pamoja na wanaotuzunguka tusijitizame sie tu wachache wenye uwezo.

    Mdau
    Mafoto.

    ReplyDelete
  8. hii imekaa vizuri jamani, mimi nimeangali hizi picha hadi machozi yamenitoka, jamani mimi nilikuwa nifunge ndoa na mchumba wangu tarehe hiyo hiyo ila ndugu zangu na mama yangu wakakataa kata kata mpaka nikanuniwa mimi nikaambiwa sina adabu kwa nini nifanye ndoa simple na wakati nina ndugu wengi? matokeo yake mimi nikaamua kuwaachia waandae shughuli yao wenyewe na hiyo shughuli budget yake wamepanga kuwa ni 7.m na mpaka sana hawajachangisha hata nusu yake, matokeo yake nasubiria siku wanialike ukumbini. Nimefurahi sana kuona kitu kizuri kama hiki, Mungu awabariki katka ndoa yenu idumu milele na milele, na mkono wa Bwana uwatangulie ktk maisha yenu mapya.

    Hongereni sana!!!!

    ReplyDelete
  9. kuna harusi bongo naikumbuka watu walichanga na kujionyesha sana ilikuuwa kufuru michango ilifika karibu million 20 watu walikunywa wakasaza saivi ni karibu 4 years bibi harusi mapepe hajatulia bwana harusi mhuni magomvi kila siku yaani we acha tu.bongo inabidi tujifunze kufanya maendeleo na kuacha ndoa za gharama ambazo baadae ni hasara tu

    ReplyDelete
  10. Mungu awabariki bw na bi harusi. Moyo mliouonyesha unafaa kuigwa. Watanzania tumekuwa malimbukeni kupita kiasi kwa hizi harusi za kifahari. Harusi zetu zinatumia pesa nyingi kuliko za watu walio ktk nchi zilizoendelea. Vipaumbele vyetu vimegeuzwa (inside out, upside down). Tujirekebishe. Utakuta mtu ana kadi 10 za michango kila mwezi. Mshahara ni 150,000/= kwa mwezi! Ndoa ni ya moyoni na wala si ufahari wa kuonekana ktk macho ya watu.

    ReplyDelete
  11. Mungu azidi kuwapa hawa wanandoa, ni mfano mzuri wa kuigwa! awashushie baraka tele na mafanikio lukuki! Chibiriti, nawe hongera, kwani kama sio wewe, wasingejua kuna watoto wanaohitajia misaada hapa home! God bless you all!
    nana

    ReplyDelete
  12. Swali la kizushi.
    Nikiiga hapa Bongo waliochnaga wanategemea wapate kadi za mwaliko waje wale, sasa nitawaambia nini???
    Hongera saba wadau wa Cesena

    ReplyDelete
  13. WABONGO MPOOOO...HARUSI SIO MASHINDANO..SIJAONA MTU KUPANDA NGAMIA WALA NINI..LAKINI NDOA IMEKUBALI.. HII NDIO TOFAUTI YA HAWA WENZETU NA SISI.TUTAENDELEA KUFUKUZA UPEPO MPAKA KIAMA KAMA BADO TUTAENDEKEZA UFAHARI.

    ReplyDelete
  14. Asante sana kwa hii post, yani umenipa wazo zuri saaana!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...