Mwimbaji wa kundi la muziki la Jahazi Morden Taarabu, Mwanne Othman (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wenzake mara baada ya kula nondozzz ya Diploma ya uandishi wa habari katika mahafali ya 15 ya chuo cha uandishi wa habari (DSJ ) yaliyofanyika jijini Dar wikiendi ilopita. Shoto ni Mwajuma Njama na kulia ni Salama Saleh.
‘Waandishi msikubali kununuliwa’
Waandishi wa habari wametakiwa kuzingatia misingi ya taaluma na kutokubali kununuliwa ili kutimiza wajibu wao kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga wakati wa mahafali ya 15 ya Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mukajanga aliwahimiza wahitimu wa astashahada na stashahada kwamba wanatakiwa kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye tasnia ya habari, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

"Andikeni habari zilizokamilika, katu msikubali kununuliwa, fanyeni kazi kwa bidii na mjaribu kuthubutu," alisema.

Aidha, alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili jamii, wakiwemo wanahabari, ni tatizo la rushwa, na akaonya kwamba wasitumie kalamu zao kupotosha habari kwa shinikizo la fedha.
"Kuna changamoto nyingi mojawapo ikiwa ni rushwa, mnapaswa kutambua kwamba ingawa fedha ni nyenzo muhimu, lakini pia si kila kitu… kinachotakiwa ni utashi, dhamira, ustahimilivu na uvumilivu. Ndivyo vitu vyenye nafasi muhimu katika mafanikio ya mwanadamu," alisema Mukajanga.

Akaongeza; "Hiki ni kipindi mwafaka kwa waandishi wanaoingia sokoni kwani nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu. Kwa mwanahabari aliye tayari kujituma, kuna kila habari ya kufukuzia, na wakati huo huo kuna changamoto ambazo ukizipitia utakuwa umepita katika chungu muhimu kitakachokupika … lakini katu msidanganyike, msikubali kununuliwa, andikeni habari za kweli na sahihi na hapa atakayekuwa na bidii, atakayethubutu, kwa hakika, mbingu itaamua."
Kama alivyosema Mukajanga, habari ndiyo inayomfanya mwandishi awe mwandishi, na wataalamu wanasema; "Mwandishi ni mzuri leo!" Maana yake ni kwamba, habari uliyoichepisha leo ndiyo inayokupima kama umeiandika kwa umakini au vipi, siyo ile uliyoiandika juzi au jana.
Changamoto inayowakabili waandishi wa Tanzania hivi sasa ni kubwa sana , hasa kutokana na taifa kukumbwa na kashfa nyingi ambazo zinawahusisha watu wengi waliokiuka maadili.
Ingawa vyombo vingi vya habari, kila kimoja kwa nafasi yake, vinaripoti mambo mbalimbali kwa namna yake, lakini ukweli ni kwamba, hata waandishi wenyewe wako kwenye mkumbo huo huo wa mmomonyoko wa maadili.

Suala la mwandishi kuandika habari kwa shinikizo la mtu fulani mwenye maslahi fulani, au kuamua kumchafua fulani ili kumkweza fulani, siyo geni sasa kwa vyombo vya habari vya Tanzania, hali ambayo inatia hofu kwamba taaluma ya habari - ambayo kimsingi ni muhimili wa nne wa serikali - imepoteza mwelekeo wake.

Hali hii inatakiwa kudhibitiwa, kwa kuleta mabadiliko ya dhati kuanzia kwenye nafsi za waandishi wenyewe, ambao kwa kiasi kikubwa kama hawakubadilika wanaweza kuipotosha jamii na hata kuivuruga zaidi serikali.
Pamoja na changamoto nyingine zilizopo kama kutokuwepo na ajira za uhakika kwenye sekta hiyo, lakini bado taaluma ya habari imesimama imara katika kuhakikisha kwamba jamii inapata haki yake ya msingi, na vile vile serikali na mamlaka husika zinafikisha ujumbe maridhawa kwa jamii katika kiwango kinachotakiwa.

Vyombo vinavyosimamia taaluma ya habari, likiwemo Baraza la Habari, vinapaswa kuwasaidia waandishi kwa namna moja ama nyingine, na siyo kuwaangalia zaidi wamiliki wa vyombo vya habari.
Mukajanga anasema kwamba baraza lake linashughulikia kuondoa kero zinazowakabili wanafunzi wa fani ya uandishi wa habari wanapotakiwa kufanya mafunzo kwa vitendo, ambapo wengi wao hunyimwa nafasi kwenye vyombo vya habari bila sababu za msingi.

Lakini mafunzo ya vitendo ni sehemu tu ya changamoto hizo, zilizo kubwa ni kukosekana kwa ajira ama mikataba ya ajira hata kwa waandishi wazoefu kunakofanywa na wamiliki wa vyombo vya habari, huku waandishi wengi wakichukuliwa kuwa 'wa kujitegemea' hata baada ya kuchangia kazi kwenye vyombo hivyo kwa miaka kadhaa.

Jambo hili linawavunja moyo wale wanaotaka kuingia kwenye taaluma hiyo ambao wanaiona kama haina manufaa kwa sababu hatua ya waajiri kuwatumikisha waandishi kama vibarua kwa miaka mingi nayo husababisha baadhi ya waandishi kukiuka maadili na kuamua kujiingiza hata
kwenye vitendo vya rushwa.

Suala jingine ni kwa waandishi wa habari kung'ang'ania zaidi kufanyia kazi mijini badala ya kwenda vijijini ama kugeukia sekta nyingine ambazo ziko karibu na jamii zaidi.

Ndiyo maana Mkuu wa Chuo hicho, Mchungaji Wilson Chiduo, anasema kwamba wahitimu wa mahafari hayo ya 15 wakizingatia maadili ya taaluma na kuona umuhimu wa kuwa karibu na jamii, wanaweza kujikita katika kuandika habari juu ya umaskini, elimu, siasa, uchumi, mazingira, utalii na rushwa.
Katika risala yao , wahitimu hao nao wameahidi kutumia elimu waliyopata kuitumikia jamii kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.

Chuo cha DSJ kilianzishwa mwaka 1998, kilipata usajili wa kwanza na NACTE 2005 na kupata usajili wa kudumu mwaka 2007 namba REG/PWF/012. Mwaka 2009 kimepandishwa hadhi na NACTE na kuwa "Candidate of Accreditation".

Kozi zinazofundishwa chuoni hapo ni uandishi wa habari na utangazaji kwa ngazi ya stashahada (Diploma) na astashahada (advanced certificate), utangazaji wa Radio, picha za mnato (Photojournalism), Picha mwendo (Television), Talakishi (Computer), Mahusiano ya Umma pamoja na utayarishaji wa matangazo (Public Relations and Advertisement).

Source: TAIFA Tanzania , Desemba 18, 2009

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. HABARI YA MAJOHO HUKO BONGO MNALALAMIKA JUU YA UFALIWAJI WAKE MNASEMA YANATAKIWA KUFALIWA NA WAHITIMU WA DEGREE TU WA CHUO KIKUU, KWA KIFUPI HIYO ILIKUWA ZAMANI ZA ZAMA ZILE ZA ORTHODOX, JANA TU NILIKUWA KATIKA MAHAFALI YA UNIVERSITY OF LONDON NIKAONA WATU TOKA WACERTIFICATE HADI PhD WAKIWA WAMEFAA MAGOWN HAYO NA KUNA WENGUNE PIA HAWAKUVAA WALIVAA MA-JEANS YAO NA MASHATI YA KAWAIDA WALIKUWEPO KWENYE KUPOKEA DEGREE ZAO KITU AMBACHO HUKO NYUMBANI KAMA HUJAVAA JOHO HUTARUHUSIWA KUPOKEA DEGREE YAKO NA WENZAKO, HAPA NIMEONA WATU HAWANA MAJOHO WAMEPOKEA MASTERS ZAO NA KUNA WATU WAMEVAA MAJOHO WAKIWA WAMAMALIZA CERTIFICATE LEVEL, WE NEED TO FLEXIBLE WITH TIME,WE MUSY CHANGE WITH TIME, THERE IS NO RULE OR PLACE WRITTEN THAT THE GOWNS SHOULD BE WORN BY DEGREE GRADUANDS OLNY, OR IF SOMEBODY IS IN CIVILIANS ATTIRE THEN SHE OR HE SHOULD NOT BE ALLOWED TO PARTICIPATE IN A GRADUATION CEREMONY. AS ALL IT IS ABOUT MONEY, NOT ALL OF US WE CAN AFFORD THEM.

    ReplyDelete
  2. Hongereni sana, mimi hoi kwa make-up za dada mwimba taarabu!

    ReplyDelete
  3. Daah! huyo dada wa taarabu amenikuna sana kwa juhudi na hatua kubwa aliyopiga.. Hongera kubwa sana dadangu.
    Naomba hii itangazwe sana kwenye TV na magazeti pia ili iwe changamoto kwa wasanii hasa wa hiyo fani ya Taarabu ambao huonekana kama watu wasio na elimu na wenye kukukumbatia ngono na anasa, ili nao waweze kujiendeleza kielimu pia.

    USHAURI wangu ni nyinyi watatu hapo pichani muanzishe kikundi chenu cha Taarabu iliyoenda shule.

    Kwa kweli mtawavutia wakazi wa Masaki na Mikocheni pia na siyo kama ilivyozoeleka kuhudhuliwa na watu wa Manzese na Tandale pekee.
    Kila la kheri jamani!!

    ReplyDelete
  4. Hongera Mwanne kwa kupata diploma ya uandishi wa habari,waimbaji wengi wa taarabu hawana elimu ya kutosha,ndio maana nyimbo nyingi zimejaa mambo mipasho,matusi,and all staffs associated with tabia za uswahili.Waimbaji wengine waige mfano wa Mwanne,kwani kama utaendeleza fani yako ya uimbaji taarabu pamoja na uandishi wa habari au utangazaji , utaweza kupata wateja wenye elimu zao ,kwani wanajua msomi na huwezi kuwa na tabia za kiswahi,washauri na wenzio wasome ili kuondoa dhana iliyojegeka juu yenu hasa waimbaji taarabu wa kike,mfano jamii inawaoneje
    -washari -mnapenda sana ugovi
    -kwa matusi kama mumesomea-je unaweza kutukanana na mwimba taaribu,hope unaweza ukajiona upo uchi
    -Ni malaya/micharuko/mashangingi-mwanaume mwenye akili zao walikuwa wanaogopa kuwaoa
    -wanatabia za uswahili-kutetana,kusengejana,wivu,fitna,mavazi ya ajabu etc

    Big up -mwanne but kama unatabia hizo hapo juu badilika,

    Mdau
    Kissenga,

    ReplyDelete
  5. hongera kwa wahitimu wote. nina suali kidogo, hivi jamani degree hizi za uandishi wa habari pamoja na public relation ndio zimekuwa na demand kubwa tanzania? au ni kwa sababu sio ngumu kupatikana? nakumbuka huko nyuma branch za engineering pamoja na accounting ndio kila mtu alikuwa anakimbilia huko, sio kwa sababu zilikuwa rahisi kupatikana ila ndio ilikuwa "must have" degree yaani ukiwa nayo basi wewe ndio msomi!! :)

    ReplyDelete
  6. mdau wa kwanza kabisa. jambo la mwanzo hebu jifunze kiswahili sawasawa. kufaliwa ndio nini? kuvaliwa ndio neno sahihi. pili kuhusu university of london wanafunzi ku-graduate bila ya majoho na kofia, unataka kumdangabya nani hapa? university zote za uk are so proud of their traditions and there is no way they will let you graduate without a rob and a hat. unachovaa ndani ya joho ni shauri yako.


    tizama link hii hapa ya university of london
    http://www.london.ac.uk/fileadmin/documents/about/governance/ordinances/Ordinance_012_annex_06.pdf

    ReplyDelete
  7. Mimi ninachotaka sasa nikusikia mitungo na nyimbo atazoimba huyo mwimba taarabu baada ya kupokea hiyo elimu yake na joho kubwa ndipo tutakapo jua kama kweli elimu yake imemsaidia au ndio fuata mkumbo tu hajatengeneza tofauti ya kabla na baada ya elimu.

    ReplyDelete
  8. huyo mwimbaji taarab asifiki uandishi kuonekana kwenye TV ajue kuna kusaga lami na kichwa kiwe na akili asifikiri kutingisha viuno kama taarab. kama fani haiwezi atokomee kabisa hatutaki fani yenye kuongiliwa na wajinga wajinga waliokosa nafasi za masomo mengine.

    ReplyDelete
  9. yani nimecheka adi basi...dah

    joho izo...make-up izo dah

    mama hongere sana maana ni maajabu ya 9 ya duniani,umetoa mfano

    ReplyDelete
  10. wadau wanaoshambulia taarab kuwa na mipasho kwa taarifa tu ni kwamba 'mipasho' ni mojawapo ya 'moyo' wa utanzu wa taarab. ukitoa mipasho basi hapo utakuwa umeanzisha kitu kingine, na hakitakuwa taarab.
    mpenzi wa mipasho

    ReplyDelete
  11. Tafadhali ndugu Michuzi kama unaweza kupata contact za muhitu huyo wa upande wa kulia itakuwa bomba!

    ReplyDelete
  12. Fani imeingiliwa!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...