Na Mwandishi Maalumu, Turkey
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa msukumo wa sasa wa kuwapo kwa uhusiano wa karibu zaidi kati ya nchi za Afrika na China unatokana na mahitaji halisi na maslahi ya kweli kweli ya Bara la Afrika na wala siyo na itikadi.

“Bara la Afrika linatafuta masoko kwa bidhaa zake. Bara la Afrika linatafuta mitaji na uwekezeji katika chumi zake. Bara la Afrika linatafuta teknolojia kwa ajili ya maendeleo yake. China iko tayari kutoa hayo yote. Sasa nongwa iko wapi?” Rais Kikwete amewauliza waandishi wa habari wa Uturuki.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza leo, Jumamosi, Februari 20, 2010, na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya Uturuki baada ya kuwa amefungua Mkutano wa Pili wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki kwenye Hoteli ya Grand Cehavir mjini Istanbul.

Kiasi cha wafanyabiashara 55 wa Tanzania wanaandamana na Mheshimiwa Rais Kikwete katika ziara yake ya siku tatu nchini Uturuki ambayo rasmi imemalizika leo. Mheshimiwa Rais Kikwete anatarajiwa kuondoka Uturuki kesho, Jumapili, Februari 21, 2010, kwenda Jordan kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili.

Rais Kikwete ametoa majibu hayo baada ya kuwa ameulizwa nini hasa nia ya nchi kama China na Uturuki ambazo ghafla zimeonyesha hamu kubwa ya kushirikiana kwa karibu zaidi na kujenga mahusiano makubwa zaidi na Bara la Afrika ambalo kwa miaka mingi limekuwa karibu na nchi za Magharibi, na hasa zile ambazo zilizitawala nchi hizo za Afrika.

Rais Kikwete amesema kuwa hamu ya Bara la Afrika ni kuona maendeleo ya haraka kwa watu wake, na nchi yoyote duniani ambayo iko tayari kusaidia azma hiyo ya Afrika inakaribishwa kwa mikono miwili kufanya shughuli na Bara la Afrika.

“Tunaendesha mahusiano yetu kwa misingi ya ushirikiano (partnership) siyo kwa misingi ya nani alitutawala wakati gani. Hakuna nongwa katika hili,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Watawala wa nchi mbali mbali wamebadilika. Sera za nchi mbali mbali zimebadilika. Lakini mahitaji na maslahi ya Afrika yamebakia pale pale. Mahitaji yetu ni masoko kwa bidhaa zetu, uwekezaji katika chumi zetu, upatikanaji wa teknolojia kwa ajili ya maendeleo yetu na nafasi za kuendeleza uwezo wa Bara la Afrika kwa njia mbali mbali na hasa kupitia elimu.”

Rais Kikwete amesema kuwa Bara la Afrika linayo haki ya kutafuta majawabu ya mahitaji yake kutoka nchi yoyote katika pembe yoyote ya dunia na bila kuwekewa masharti kama zinavyofanya baadhi ya nchi.

Amewakumbusha waandishi hao kauli ya kiongozi wa zamani wa China, Hayati Deng Ziyao Ping, ambaye kuhusu maendeleo na nani wa kushirikiana naye katika kutafuta maendeleo, alipata kusema:

“Sijali paka anayo rangi gani ili mradi awe na uwezo wa kukamata panya.”

Rais Kikwete amesema kuwa wakati mwingine ni jambo la kushangaza kuwa baadhi ya nchi ambazo zimewekeza sana katika uchumi wa China na kuifanya nchi hiyo jambari la uchumi duniani, ndizo zinalalamikia nchi za Afrika kushirikiana na China.

Amesema kuwa ni jambo la ajabu kabisa kuwa nchi hizo hizo ambazo zinapiga kelele kuhusu ukaribu wa nchi za Afrika na China, ndizo hizo hizo ambazo zimeshirikiana kwa karibu sana na nchi hiyo ya China.

“Kama nchi hizi kweli zina wasiwasi kuhusu China kuwa na uhusiano wa karibu na Afrika, kwa nini hazina wasiwasi kwa nchi hiyo kuwa karibu na nchi hizo. Kwa nini iwe sawa kwa China kushirikiana na wakubwa hawa, lakini iwe siyo sawa kwa China kushirikiana na nchi za Afrika?”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 13 mpaka sasa

  1. wadhungu ni wanafiki jamani wapo kama panya buku kazi kuuma na kupuliza safi sana JK bora umegundua hilo

    ReplyDelete
  2. Kwanza nampongeza Rais JK kwa kuvunja kiu! na kuwambia ukweli wanahabari wa uturuki,kuwa uhusiano wa China na Afrika ni kwa maslahi halisi ya Afrika,huu ni ukweli mtupu ambao baadhi ya nchi duniani hazitaki kuelewa!nyingi ya nchi hizo ni za ulaya.
    Zinajaribu kuleta hoja za ajabu ambazo ikundani ukizunchungulia hazina maslahi kwa afrika bali zina maslahi kwa wazungu wa ulaya na viwanda vyao.

    Uschina imekubaliana na baadhi ya nchi za kiafrika katika maswala ya kiuchumi na kubwa zaidi ni soko la bidhaa za afrika uchina,china inahitaji maligafi kama mafuta kutoka sudan,madini n.k nasisi tunahitaji madawa,majengo kama vile shule,zahanati,viwanda vidogo na vikubwa,pembejeo za kilimo,ambazo uchina hipo tayari kutoa bila ya mashariti magumu.
    Nchi za ulaya haziwezi kutupa msaada wafrika bila kutuwekea mashariti ambayo ukiyaangalia ni ukoloni mpya!SASA TUNASHUKURU KUWA RAIS JAKAYA KAWEKA WAZI KUWA UHUSIANO WETU NA CHINA NI CHAGUO LETU!kwa nini? tuchaguliwe nani? wakufanya biashara.
    Kudondoka kwa soko la fedha katika nchi za ulaya na amerika,zinazifanya nchi hizo kutapa tapa kama vile mtu anakufa maji

    ReplyDelete
  3. mheshimiwa rais kikwete,uhusiano na china tunauhitaji.lakini mbona hao wachina wanafanya tanzania jalala?kuna vitu feki kuanzia majumbani hadi maofisini,inawezekana hata jeshini kuna vifaa feki vya kichina.je unahakikisha watendaji wako wanakuwa makini na vitu vya china??
    China wanatufanya sisi jalala kwasababu vitu vya china vinavyoenda ulaya na marekani ni vya viwango vya hali ya juu na bei yake ni nafuu kuliko vifaa feki wanavyotuletea tanzania.je huu ndio uhusiano unaousema??wanaleta hadi hygenic pad fake zinazotumiwa na dada/mama wa watoto wetu hadi wanapata magonjwa ya kansa/uti je unajua hili??kuna vitu vingi kama sio vyote kutoka china ni feki na vinadidimiza uchumi wetu kwa njia moja au nyingine.mfano kuna simu feki nyingi tu kutoka china zinauzwa 150,000-200,000 lakini simu hizo hizo gunuine zinauzwa UK kwa £30-50,angalia mfano wa TVs kuna LCD feki tz inauzwa kuanzia tsh mil 1.5-4mil lakini LCD original UK zinauzwa kuanzia £200-500 ingawa zipo za bei ghali zaidi,hio ni mifano michache,mheshimiwa rais uhusiano tunautaka lakini sio wachina kutufanya sisi ni jalala la takataka zao.

    ReplyDelete
  4. Msafara wa Rais + wafanyabiashara 55!!!!!

    No comment.

    ReplyDelete
  5. HAPA NAKUBALIANA KWA ASILIMIA ELFU MOJA NA MAJIBU MWANANA YA RAIS WETU, HAKUNA NONGWA KABISA KUSHIRIKIANA NA NCHI AMBAYO INATAKA KUKUSAIDI KUSIMAMA KWA MIGUU YAKO MIWILI ILI MRADI HIYO AU HIZO NCHI ZINAFUATA TARATBU NA SHERIA ZA NCHI WANAZOTAKA KUZISAIDIA. WAKATI UMEFIKA WA NCHI ZA MAGHARIBI HASA ULAYA KUBADILISHA SERA ZAO ZA NJE NA ZA UHAMIAJI, KWANI NI WAZURI KWA KUZUNGUMZA TU LAKINI NDANI YA MIOYO YAO NI WABAYA SANA. MOST OF THE TIME THEY KEEP ON CHANGING THEIR POLICIES TO SUIT THEIR PEOPLES'NOISES KWA MFANO SASA ZERA ZOTE ZA UHAMIAJI ZA ULAYA HAZITAKI WAHAMIAJI TOKA NJE YA EUROPE WANAWEKA MASHARITI MAGUMU WAKIJUWA FIKA KWAMBA WA-AFRIKA HAWATAZIWEZA ILI KIWE KIZUWIZI CHA WA-AFRIKA KWENDA KATIKA NCHI ZAO. NCHI KAMA CHINA YENYE POPULATION KUBWA YA OVER BILLION PEOPLE WALA HAINA MASHARITI MAGUMU KWA WA-AFRIKA KWENDA KWAO AMA KWA KUSOMA, KUISHI AU KUFANYA BIASHARA NAO SASA NONGWA IKO WAPI HAPO KAMA WANATUKARIBISHA SISI MANYANI WAPELEKA MAGONJWA ULAYA, WAZUNGU NI WANAFIKI WANASAIDIA PALE WANAPOONA WANA MASLAHI NAPO. WAKATI UMEFIKA WA SISI NA VIONGOZI WETU KULIONA HILO NA KUANZA KUFANYA BIASHARA NA URAFIKI WA KWELI NA WALE TU WANAOTUTAKIA MEMA. NA VIJANA NENDENI MASHARIKI YA MBALI KWA ELIMU NI NZURI TU KAMA YA WEST, KWA MFANO ELIMU YA KOMPUTER YA KOREA YA KUSINI NI BORA ZAIDI YA ILE YA ULAYA, NENDENI MKAPATA ELIMU NA KUANZISHA BIASHARA NAO NA TUTAENDELEA TU, NAJUWA MTAKUWA VIONGOZI WETU WA BAADAYE MUWE NA MSIMAMO WAKISASA WAZUNGU HAWATAKI SISI TUENDELEE WANATAKA TUWE TEGEMEZI KWAO NA SOKO LA HUDUMA NA BIDHAA ZAO, SI WATU WAZURI HATA KIDOGO, HASA WAKIONGOZWA NA UNITED KINGDOM.

    ReplyDelete
  6. Mdau uliezungumzia TZ kuwa jalala la bidhaa feki, nakuhakikishia 100% waagizaji na waingizaji wa bidhaa feki ni WaTZ wenyewe wanaopenda dezo na kupata faida kubwa.

    Badala ya hawa wafanyabiashara kwenda kununua vitu genuine huko China, wanabeba catalogues na kwenda nazo kwenye viwanda vya uchochoroni kuburuziwa feti feki. Wao wanaonyesha kuanzia mabegi na vitu kibao vingine unavikuta kwenye Boutiques za maana tena vinauzwa bei kubwa kumbe vimeburuzwa uchochoroni India.

    Wako wanaotengeneza viberiti, mabetri na kuingiza makontena ya bidhaa hizo feki nchini mwetu, achilia mbali hizo bidhaa nyingine za electoniki kama simu za mkononi na kadhalika.

    Siku hizi hata ulaya hakuna made in UK au EU au US, viwanda vyote vilihamishiwa China, kuanzia viatu na vitu vinginevyo ama vinatoka China au India. Nyie wenyewe acheni kwenda kutengeneza bidhaa feki huko China ili kupata faida kubwa.

    ReplyDelete
  7. kwanza kabisa nampongeza rais kwa kumfunga paka kengele. hii inafanana kidogo na ya Ahmednedjad (sijui nimelipatia?) wa jamhuri ya Iran na nukes enrichment program zake.
    muda umefika kwa Afrika kujiamulia mambo yake kwa faida yake na watu wake. nakubaliana na aliyesema wafanyabiashara wetu ndio chanzo cha bidhaa feki kutoka china.tena viwanda vingine china vipo kwenye maboti kabisa!! ni juu ya mamlaka zinazohusika kusimamia hili. kila jambo linahitaji udhibiti hata kula chakula kunahitaji kipimo.
    tukijadili uozo wa sera za ulaya na afrika inatia uvivu bora niishie hapa.

    ReplyDelete
  8. Mzee JK asante sana kwa nia yako nzuri ya kutaka kutuletea maendeleo ya haraka. Lakini naona huna washauri wazuri. Wale wotw waliokuzunguka hawana lolote. Sijui kama unalitambua hilo. Hao unaowaita wafanyabiashara unaoongozana nao ndio hao wanaingiza bidhaa feki, kwa kutumia maajenti wao. Hawa wafanyabiashara ndio wamechagia kiasi kikubwa katika ajali za barabarani, milipuko ya moto n.k .Ni bora ukae nao kitako kwanza, wapewe maadili hapo ndipo utatuambia ushurikiano wa kibiashara na china tukakuelewa.

    Angalia Mama Salma alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kichina juzi juzi.Wachina hao hao ndio wanauza vitu feki mama Salma anajua. Ndio hao wanaotaka kuua watoto wetu na dawa feki za malaria walizotangaza kutoa bure, baada ya kupimwa na wachina wasio wataalamu pale SINO-TANZANIA FRIENDSHIP HOSPITAL.Mama anajua. Lakini katika hotuba aliwasifu sana kwa ushirikiano mzuri. Wala hakutoa ushauri kwa wachina kuwa na ushirikiano wa kweli.
    Kwa hiyo watanzania tuombe Mungu tu.Tunauawa na watu wa kwetu TZ. wanaojali maslahi yao binafsi na jamaa zao.

    Tusiwaogope hawa wenye rangi. Ni wa kukemea tu. vinginevyo tutauawa soote na wachina watajichimbia.

    ReplyDelete
  9. Uhusiano wetu na China ni kwa maslahi yetu wenyewe??????? This is a joke.... faida gani tunapata kuletewa takataka na kubanana na wachina hadi kariakoo.... na siku hizi wanauza hadi maji ya viroba.... watu walio nje know nothing msiseme tu, vile nyie mko mbali hamuoni hustle tunazopata na hawa jamaa

    ReplyDelete
  10. Biashara ni demand and supply. Kuna watu wangapi Tanzania wako tayari kununua bidhaa genuine? Uwezo wetu mdogo ndio unawafanya wafanyabiashara wanunue bidhaa za hali ya chini kwa kuwa vile vya bei juu hawatapata soko. Mpaka hapo mishahara itakapopanda, bidhaa feki an ya hali ya chini itaziid kuja Tanzania.

    ReplyDelete
  11. annon 06:03:00pm umenichekesha?

    1.mimi naitaji tu iyo list ya wafanyabiashara 55 lol,ndege gani walipanda ile jeti au???
    2.afu selection ilikuweje mbona wengine hatujasikia ilhal twaweza wekeza tu?

    khaaaaa

    ReplyDelete
  12. Msafara wa Rais + wafanyabiashara 55

    Hata ingekuwa wafanyabiashara 1000 kwani wanalipiwa na serikali? Mi sina uhakika wa hilo ila katika hali ya kawaida hawawezi wakawa wanalipiwa na serikali.

    ReplyDelete
  13. Wafanya biashara 55 unahoji?? mbona wachache mno, mimi nadhani business delegation ilitakiwa kuwa kubwa mno ili hatimaye watu wengi zaidi waweze kunufaika na fursa mpya zitakazoibuliwa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...