MV Serengeti ikiwaka moto bandarini Zenji
huku zimamoto wakiwa kwenye meli ingine wakijaribu kuuzima moto huo

MELI ya mv Serengeti imeteketea kwa moto ikiwa nangani katika Pwani ya Forodha Mchanga meta chache kutoka Bandari Kuu ya Malindi na mlango bahari wa kuingia bandarini.
Meli hiyo ya mizigo na abiria inayomilikiwa na Kampuni ya Jack Enterprises iliyosajiliwa Zanzibar, ilikuwa inajiandaa kwa safari yake ya kawaida kwenda Kisiwani Pemba.

Mv Serengeti iliyokuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa Pemba ambao sasa watakuwa katika wakati mgumu wa safari, ilianza kuwaka moto jana saa sita mchana. Mashuhuda wa moto huo wanasema meli hiyo ilikuwa imeegeshwa kando ya bandari na mabaharia wanane waliokuwemo ndani waliokolewa haraka muda mfupi baada ya moto huo kuwaka kwa kasi kubwa.

Moto huo ulikuwa ukiwaka kwa kasi kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma katika Bahari ya Hindi na kusababishia hali ngumu kikosi cha wanamaji na waokoaji ambao walikuwa wakijaribu kuuzima moto huo kwa takriban masaa mawili.

Hadi sasa chanzo cha moto huo bado hakijulikani na Mrajisi wa meli Zanzibar, Abdallah Mohammed amesema ni mapema mno kujua chanzo chake pamoja na thamani ya mali na mizigo iliyokuwemo ndani ya meli hiyo hadi hapo tathmini kamili itakapofanywa.

Habari ambazo bado hazijathibitishwa zinaeleza kuwa meli hiyo ilikuwa ikifanyiwa matengenezo madogo madogo nangani na kwa wakati huo ilikuwa ikichomewa.

Sehemu zote za ndani na nje ya mv Serengeti zimeungua moto na mwonekano wake kugeuka. Juzi Meli hiyo ilitokea Kisiwani Pemba ambapo baadhi ya abiria waliosafiri na meli hiyo walisema walichelewa kufika bandarini Unguja.

Mrajisi huyo amesema meli hiyo ilikuwa ina uwezo wa kuchukua abiria 1,000 na tani 100 za mizigo lakini kibali cha leseni kimeruhusu kuchukua abiria 850 na ilikuwa ikifanya kazi zake bila ya wasiwasi katika kipindi chote na kwa mara ya mwisho ilisajiliwa Januari mwaka huu.

Amesema meli hiyo haikuwa na matatizo na ilikuwa ikifanya safari zake ambapo tayari abiria kadhaa walikuwa wameshakata tiketi kwa safari ya kwenda Pemba usiku wa jana.

Chanzo cha habari

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Tunamshukuru Muumba hakuna maisha yaliyopotea.
    Ankal, ni kweli eti Zimamoto walishindwa kudhibiti huo moto mara tu walipowasili kwa sababu meli yao haikuwa na maji ya kutosha- ilibidi sijui maji yafuatwe kama maili mbili hivi?

    ReplyDelete
  2. hiyo zima moto mbona maji yanatoka ka mkojo wa mtoto

    ReplyDelete
  3. mara ndege imekatika mataili kwa kuteleza uwanjani mwanza na kuharibika, mara meli imeungua, maajali ya mabasi ndio usiseme..mhh tumechoshwa unaweza kukuta ni uzembe wa mtu fulani tu...

    ReplyDelete
  4. TUOMBE HURUMA YA MUNGU KAMA TAIFA. MAJANGA YA AJALI TANZANIA YETU MASKINI YAMEZIDI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...