Balozi Johnnie Carson

Hotuba ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anayeshughulikia Masuala ya Afrika,
Balozi Johnnie Carson
Kwa Mabalozi wanaowakilisha nchi za Afrika
Katika Maadhimisho ya Siku ya Afrika

Ninapenda kuchukua fursa hii kuishukuru Kamati ya Maandalizi kwa kunialika kuzungumza katika hafla hii jioni ya leo. Ni heshima kubwa kwangu na kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kushiriki katika maadhimisho haya ya miaka 47 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU). Siku ya Afrika ina umuhimu wa kipekee zaidi mwaka huu kwa sababu nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Cameroon na nyingi ya nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa zinasherehekea miaka hamsini toka kupata uhuru kutoka kwa tawala za kikoloni.

Hili ni tukio mwafaka la kuendeleza na kusisitizia azma adhimu ya Afrika ya uhuru na umoja, lakini pia ni wakati wa kutathmini kwa dhati changamoto kubwa ambazo bara hili linaendelea kukabiliana nazo. Marekani ilikuwa mtetezi mkubwa wa Uhuru wa Afrika, na hivi leo bado inaendelea kuwaunga mkono wabia wake wa Kiafrika katika kukabiliana na changamoto hizi. Hata hivyo, kama ambavyo nitaeleza katika hotuba yangu ya leo, uwezo wetu wa kufikia malengo yetu ya pamoja ya muda mrefu ya kujenga demokrasia, utulivu na ustawi katika bara hili utategemea sana uadilifu na ufanisi wa viongozi wa Afrika.

Mwaka 1960, dunia ilikuwa ikihangaika kujiondoa katika historia yake ya matumizi ya mabavu na udhalimu na kuanza kuishi kwa kuzingatia misingi na maadili mapya yaliyo bora zaidi. Bara la Ulaya lilikuwa bado likijijenga baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na nchi nyingi za bara hilo zilikuwa nyuma kwa miongo miwili hadi mitatu kabla hazijawa nchi za demokrasia kamili. Dhana za nchi kujiamulia mambo yake yenyewe na usawa miongoni wa watu wa rangi mbalimbali ndiyo kwanza zilikuwa zimeanza kukubalika. Wakati huo, uhuru wa Afrika ulikuwa ni mojawapo ya hatua kubwa zilizofikiwa katika harakati hizo na jambo lililoleta matumaini makubwa. Baada ya miaka 80 au zaidi ya kuwa chini ya utawala kandamizi wa kikoloni, Waafrika wengi wakawa huru kujitawala na wakakubalika kama wahusika katika anga za kimataifa. Pamoja na kwamba harakati za kujitawala zilichukua muda mrefu zaidi na kugharimu maisha ya watu wengi zaidi katika baadhi ya nchi ikiwa ni pamoja na Afrika ya Kusini, Zimbabwe na nchi zilozokuwa chini ya utawala wa Wareno, msingi wa uhuru wa mataifa ya Afrika ulikuwa tayari umewekwa toka mwaka 1960 na kuimarishwa miaka mitatu baadaye kwa kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika.

Uhuru wa Afrika una umuhimu wa Kipekee kwa Marekani kwa sababu ya uhusiano wa kihistoria kati ya Marekani na bara hili na kutokana na msingi ya haki za binadamu na uhuru wa watu kujiamulia mambo yao wenyewe kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Marekani na Azimio letu la Uhuru. Takriban asilimia 12 ya Wamarekani wote, ni watu wenye asili ya Afrika na majirani zetu wengi katika nchi za Caribbean na Amerika ya Kusini wana idadi kubwa ya watu wenye asili ya Afrika. Ubadilishanaji wa mawazo na fikra za kisiasa kati ya wanaharakati wapigania uhuru wa Afrika na wanaharakati wa haki za binadamu wa Marekani ulianza toka mwishoni mwa karne ya 19. Aidha, Waafrika na Wamarekani wana mahusiano ya karibu sana katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na dini, muziki, utamaduni na sanaa. Hakuna ambaye amejengwa vyema na mahusiano haya kama Rais wetu wa sasa, ambaye amechanganya busara na uzoefu wa baba yake ambaye alikuwa ni Mkenya pamoja na harakati za utetezi wa haki za binadamu za Marekani.

Pamoja na mwanzo wao mzuri wa kutia matumaini, nchi nyingi za Kiafrika, katika miongo iliyofuata baada ya uhuru hazikuwa na uongozi mzuri. Watu ambao kweli walikuwa wamejitoa kwa dhati kwa ajili kujenga nchi zao kwa misingi ya haki, uadilifu na demokrasia, kama ilivyokuwa kwa Rais wa kwanza wa Botswana Seretse Khama na Rais wa Kwanza wa Senegal Leopold Senghor—walikuwa ni wachache sana. Katika nchi nyingi, matatizo mbalimbali ikiwemo rushwa, taasisi hafifu na zisizo za kidemokrasia, tawala za kikandamizaji na ukabila ulisababisha mapinduzi, serikali za kijeshi, vita, ukiukwaji wa haki za binadamu, ukatili na mauaji ya halaiki.

Viongozi wengi wa Afrika walikiuka misingi mikuu ya haki za binadamu na uhuru kama ilivyoainishwa katika Mkataba ulioanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika na wengine waliwatendea watu wao ukatili mkubwa kama au hata zaidi ya ule uliofanywa na wakoloni. Matumizi mabaya na ubadhilifu wa fedha na mali za umma na ukiritimba katika usimamizi wa uchumi ulisababisha kuporomoka kwa kasi kwa uchumi na miundombinu na kuzorota kwa huduma zinazotolewa na serikali. Uhasama wa Vita Baridi nao ulichochea vita na machafuko katika nchi mbalimbali kama vile Chad, Angola na Msumbiji.

Toka mwanzoni mwa miaka ya 1990, nchi kadhaa za Kiafrika zimeweza kujiimarisha kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha uongozi na kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa. Japokuwa bado zinakabiliwa na matatizo kadhaa, mataifa mbalimbali ya Kiafrika yaliyokuwa na vita na machafuko kama vile Sierra Leone, Liberia, Msumbiji, Rwanda, na Angola yameweza kwa kiwango kikubwa kurejesha amani na yapo katika hatua mbalimbali za mpito kuelekea katika demokrasia na kujiimarisha kiuchumi.

Nchini Ghana, serikali ya Rais Jerry Rawlings ilianzisha mageuzi ya kiuchumi na polepole kufungua milango kwa demokrasia ya vyama vingi. Rawlings mwenyewe aliang'atuka na kukabidhi madaraka kwa chama cha upinzani baada ya kumaliza kipindi chake cha pili cha utawala kinachoruhusiwa kikatiba. Mrithi wake, John Kuffuor, alifanya vivyo hivyo, kwa kukabidhi madaraka kwa chama cha upinzani baada ya chama chake kushindwa uchaguzi kwa kura chache. Huko Mali, Jeneral Amadou Toumani Toure alikabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia iliyochagulia kidemokrasia hapo mwaka 1992 baada ya kuupindua utawala wa mabavu wa kijeshi mwaka mmoja nyuma. Mrithi wake Alpha Omar Konare aliachia madaraka miaka kumi baadaye, baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili vinavyokubalika kikatiba. Nchi za Benin na Senegal nazo zimenufaika kutokana na viongozi wao kuwa radhi kuheshimu katiba na matokeo ya chaguzi zilizowaondoa madarakani.

Huko Afrika ya Kusini, Nelson Mandela na F.W. de Klerk walikwenda kinyume na matarajio ya wengi ya kuendelea kwa machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na ubaguzi wa rangi nchini mwao kwa kuwa na majadiliano ya amani kati ya mwaka 1990 hadi 1994 ambayo yaliwezesha kumalizika kwa utawala wa kibaguzi. Mandela aliweza kuondoa uhasama uliotokana na ubaguzi wa rangi na kukubali kwa hiari yake kuachia madaraka baada ya kipindi kimoja tu cha utawala wake. Mrithi wake, Thabo Mbeki, alikubali kushindwa kisiasa na kujiuzulu hapo mwaka 2008 kabla ya kumalizika kwa mhula wake wa pili wa utawala baada ya kutakiwa kufanya hivyo na chama chake.

Katika nyanja ya uchumi, tumeweza pia kuona hatua nzuri ambayo imepigwa na mataifa kadhaa ya Afrika, ambapo kabla ya kutokea kwa mgogoro wa fedha wa kimataifa tuliweza kushuhudia karibu muongo mmoja wa ukuaji wa uchumi. Kwa zaidi ya miongo miwili nchi za Mauritius, Ghana, Rwanda, Botswana, Tanzania, Uganda, na Cape Verde zimeweza kufanya mageuzi ya kiuchumi kwa kuruhusu soko huria na kuandaa sera zinazowezesha ukuaji wa biashara, ikiwa ni pamoja na kupunguza muda unaohitajika kuanzisha na kusajili biashara.

Japokuwa hatua hizi na nyingine zilizofikiwa ni kubwa, bado zinapimwa kwa kuzingatia kiwango cha chini sana cha maendeleo ambayo Afrika ilikuwa imeyafikia hapo awali. Kwa maoni yangu, bara hili kwa ujumla wake bado halijaweza kuondoa changamoto zinazolifanya lishindwe kutumia kikamilifu fursa na uwezo wake kama ilivyotarajiwa wakati wa uhuru. Baadhi ya nchi zinarudi nyuma na kurejea katika tawala za kimabavu huku zikiminya fursa za kisiasa na asasi za kiraia na vikundi vya upinzani vikikabiliwa na vitisho zaidi. Katika miaka miwili iliyopita nchi za Mauritania, Guinea, Niger, na Madagascar zimeshuhudia mapinduzi ya kijeshi. Nchi ya Cote d’Ivoire imeshindwa kufanya uchaguzi wa rais toka mwaka 2000 huku ikiendelea kuahirisha zoezi hilo. Nayo Jamhuri ya Afrika ya Kati hivi karibuni imesitisha uchaguzi wake kutokana na kushindwa kufanya maandalizi yake. Nchi ya Nigeria ambayo uchaguzi wake wa mwaka 2007 ulikuwa ndiyo uchaguzi uliogubikwa na udanganyifu na kasoro nyingi katika historia yake, haijaweza kufanya mageuzi yanayotakiwa ili iweze kuendesha uchaguzi mzuri hapo mwakani. Nchini Zimbabwe, maafisa wa serikali ya chama tawala cha ZANU-PF wanaendelea kukwamisha demokrasia kwa kuwanyanyasa viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani na jumuiya huru za kiraia na kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa watu wote wana uhuru wa kuendesha shughuli za kisiasa kama ilivyokubaliwa katika mkataba wa kuchangia madaraka (the Global Political Agreement).

Pamoja na ukuaji wa uchumi nilioutaja hapo awali, pato la jumla (GDP) la bara la Afrika lilikuwa ni asilimia 1.6 tu ya pato la jumla la dunia na kiwango cha biashara yake ya nje ni asilimia 1.8 tu ya biashara yote ya kimataifa. Hiki ni kiwango cha chini sana ikilinganishwa na kiwango cha juu kabisa cha asilimia 3 ambacho Afrika ilikifikia mwaka 1976. Wastani wa maisha ya mtu barani Afrika ni miaka 51, ikilinganishwa na miaka 64 kwa watu wa Asia ya Kusini na miaka 68 kwa watu wa nchi za Kiarabu. Katika maeneo mengi, utajiri mkubwa wa maliasili za Afrika haujaweza kuleta ustawi kwa watu wake. Kuna pengo kubwa katika maendeleo na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (digital divide) kati ya Afrika na mabara mengine jambo linalofanya makampuni ya Afrika yashindwe kushindana kikamilifu katika ulingo wa biashara duniani. Kila mwaka, Waafrika wengi wenye elimu nzuri na utaalamu wa hali ya juu katika nyanja mbalimbali huondoka katika bara hili na kuhamia katika mabara mengine jambo linaloongeza ugumu kwa Afrika kushindana na mabara mengine.

Japokuwa migogoro ya kivita barani humu imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka ya 1990, bado migogoro imeendelea kusababisha majanga makubwa ya kibinaadamu katika baadhi ya maeneo ya bara hili, hasa Somalia, Darfur na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kundi la waasi wa Lord’s Resistance Army linaendelea kuendesha shughuli zake kuvuka mipaka ya nchi kadhaa huku likitishia usalama na utulivu wa maeneo hayo, likivamia vijiji, likiwateka nyara wanawake na watoto na kufanya ukatili mwingi wa kutisha. Kuzuka kwa mara kwa mara kwa mapigano kati ya makundi hasimu huko Nigeria na mapigano kati ya vikundi vya wanamgambo vinavyopingana huko Sudani ya Kusini ni kielelezo cha migogoro iliyopo na inayoendelea chini kwa chini ambayo inaweza kuwa mikubwa nay a muda mrefu zaidi iwapo haitashughulikiwa kikamilifu.

Katika hotuba yake aliyoitoa mwezi wa Saba mwaka jana, Rais Obama alieleza bayana kuwa Marekani ipo pamoja na wabia wetu wa Afrika katika jitihada zao za kukabiliana na changamoto hizi. Katika eneo la utawala bora na demokrasia, tunakusudia kufanya kazi na jumuiya ya kimataifa na asasi za kiraia ili kuimarisha taasisi za kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na tume huru za uchaguzi na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni katika ujenzi wa demokrasia.

Tutaendelea kusaidia jitihada za kukuza uchumi na maendeleo, ikiwa ni pamoja kuendesha mpango maalumu wa kusaidia kuongeza uhakika wa chakula (food security) duniani utakaogharimu kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 3.5 ambao utazisaidia nchi 12 za Kiafrika katika kuongezea nguvu jitihada zao chini ya Mpango Maalumu wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Program--CAADP). Serikali ya Rais Obama imedhamiria kwa dhati kufanya kazi na wabia wake wa Kiafrika ili waweze kutumia kikamilifu fursa zitokanazo na mpango wa AGOA. Aidha, tunaendelea kutafuta mbinu mbalimbali za kuongeza ukuaji wa sekta binafsi na uwekezaji barani Afrika, hususan katika biashara ndogo na za kati.

Katika sekta ya afya ya jamii, tumedhamiria kuendelea kufanya kazi bega kwa bega na serikali za Afrika na jumuiya huru za kiraia katika kuhakikisha kuwa watu wote barani Afrika wanapata kwa urahisi huduma bora za kinga na matibabu. Serikali ya Rais Obama imeendelea na Mpango Maalumu wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) na kuendeleza kikamilifu mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI. Aidha, Serikali ya Rais Obama inaendeleza Mpango Maalumu wa Rais wa Kukabiliana na Malaria, ugonjwa unaoongoza kwa kuua idadi kubwa zaidi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano barani Afrika. Ili kukabiliana kikamilifu na changamoto zinazokabili afya ya umma barani kote, tumeahidi kutoa jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 63 kwa PEPFAR na miradi mingine inayohusu afya katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Rais ameonyesha dhamira ya dhati ya kumaliza migogoro ya kivita barani Afrika kwa kumteua Jenerali Scott Gration kama mjumbe wake maalumu huko Sudan na Mjumbe wa zamani wa Baraza la Congress, Howard Wolpe kama mjumbe wake maalumu katika maeneo ya Maziwa Makuu.

Marekani inashirikiana kikamilifu na viongozi wa Kiafrika, jumuiya huru za kiraia na jumuiya ya kimataifa katika kuzuia kuzuka kwa migogoro mipya. Tunaendelea kutoa mafunzo na vifaa kwa Jeshi la Kulinda Amani la Afrika kwa kupitia mpango maalumu wa kuzisaidia nchi za Kiafrika kuimarisha uwezo wao kushiriki kikamilifu kwenye operesheni za kulinda Amani (ACOTA) na mipango mingine chini ya Mpango wa Kimataifa wa Kulinda Amani (Global Peace Operations Initiative). Hali kadhalika, tunaunga mkono azma ya Umoja wa Afrika ya kuwa na utaratibu wake maalumu wa kulinda Amani na usalama ikiwa ni pamoja na kuwa na Jeshi la Afrika la Kulinda amani.

Tunashiriki pia katika kusaidia kutanzua changamoto za kimataifa kwa kuimarisha uwezo wa Afrika kulinda usalama wa maeneo yake ya bahari kwa kutoa vifaa na mafunzo na tunasaidia katika mapambano dhidi ya ugaidi kwa kupitia programu mbalimbali za kusaidia usalama wa kimataifa na kikanda kama vile Ubia wa Kupambana na Ugaidi katika nchi za Sahara (Trans-Sahara Counterterrorism Partnership) na Mpango wa Usalama wa Kanda ya Afrika Mashariki ( the East Africa Regional Security Initiative). Marekani imedhamiria pia kufanya kazi na Waafrika kutafuta suluhisho mwafaka katika kukabiliana na madhara makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi na inatafuta njia za kujenga uchumi endelevu wa dunia kwa kutumia vyanzo vya nishati zisizoharibu mazingira.

Miaka hamsini iliyopita, Marekani na dunia kwa ujumla iliona fursa kubwa ya Afrika, kwa maana ya maliasili zake na rasilimali watu iliyonayo. Bado tunaona vivyo hivyo. Kwa kufanya mageuzi sahihi, kuwa na uongozi mzuri na kuendelea kupata msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, Afrika inaweza kushuhudia mabadiliko makubwa kama yale yaliyoshuhudiwa huko Asia au Amerika ya Kusini katika miongo miwili iliyopita.

Lakini, kama alivyosisitiza Rais Obama katika hotuba yake ya Ghana, sera zetu zinajengwa katika msingi kwamba "Mustakabali wa Afrika upo mikononi mwa Waafrika wenyewe.” Bila kuwepo kwa dhamira ya dhati kutoka kwa viongozi wa Afrika ya kuweka na kutekeleza kikamilifu mageuzi na sera zinazohitajika kuleta mabadiliko ya kweli, hatuwezi kutarajia kufikia malengo yetu ya pamoja ya kuwa na Afrika yenye amani, ustawi na uhuru zaidi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...