WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WATOTO


RAMBI RAMBI ZA WIZARA KUHUSU WATOTO WAWILI (2) WALIOFARIKI DUNIA KATIKA UKUMBI WA DISCO WILAYANI TEMEKE: 10 SEPTEMBA, 2010

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, inatoa rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watoto wawili (2) ambao ni Lilian Sango (8) na Amina Ramadhani (6) waliofariki dunia tarehe 10 Septemba, 2010 wakati wakicheza dansi katika ukumbi wa Luxury Pub Wilayani Temeke.

Inaelezwa kuwa, maafa hayo yalitokana na kukatika kwa umeme katika ukumbi huo na kusababisha kukosekana kwa hewa na hivyo watoto wakapatwa na mkanganyiko uliosababisha kukanyagana ukumbini wakati wakigombea kujiokoa.

Wizara imepokea taarifa ya maafa hayo kwa masikitiko makubwa kufuatia mazingira ya vifo kufanana na tukio lililotokea Oktoba Mosi, 2008 Mkoani Tabora na kusababisha vifo vya watoto 19. Wizara inatambua thamani ya maisha ya watoto hao waliopoteza maisha yao maana wangekuwa rasilimali kubwa na tegemeo kwa wazazi, jamii na Taifa kwa ujumla.

Wizara inasikitika kuona kwamba maisha ya watoto hao yamekatishwa mapema wakiwa katika umri mdogo kinyume na mategemeo yetu sote kwani haki yao ya kuishi imetoweka ghafla na kuzima matarajio ya wanafamilia na jamii kwa ujumla.

Tunaamini kwamba maafa haya yamesababisha simanzi kubwa kwa wazazi, walezi na familia za watoto hao. Wizara inawaombea wanafamilia wawe na moyo wa subira na ujasiri katika kipindi hiki kigumu.

Wizara inatoa wito kwa wazazi na wadau wote wanaohusika na masuala ya haki na ustawi wa watoto kuhakikisha kuwa, katika kuratibu matukio yanayohusisha ushiriki wa watoto; jamii itambue kwamba watoto ni kundi la watu ambao hawajakomaa kimwili na kiakili; hivyo wakati wote wanahitaji uangalizi madhubuti wanapokuwa katika maeneo mbalimbali.

Wadau wote wanatakiwa kuhakikisha kuwa katika suala la utoaji wa huduma kwa watoto jamii iwe makini kuhakikisha kwamba miundombinu iliyopo imezingatia maslahi ya watoto kwa ajili ya kuepuka maafa yanayoweza kuzuilika.

Aidha, ikumbukwe kuwa katika kuratibu shughuli zinazohusu maslahi ya watoto wetu, maamuzi na usimamizi wa wazazi, familia, na wanajamii ni muhimu kuzingatiwa ili kulinda na kuendeleza Haki na Usitawi wa Mtoto.

Marriam J. Mwaffiusi
KATIBU MKUU
13 Septemba, 2010

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. A mother-To-BeSeptember 13, 2010

    So what???Haya maneno yatamsaidia nini mtu aliyepoteza mtoto wake?

    Je mnapofananisha matukio haya mawili hamjioni kuwa mmeshindwa kazi kabisa? Ni njia na sheria gani ilichukuliwa baada ya tukio hilo la Tabora kuhakikisha hakuna watoto wengine hawayakuti haya?

    Je huyu mwenye hii bar amezingatia mambo yote ya safety?Je kulikua na emergency exist na ukumbi ulikua na idadi ya watu sahihi inayotakiwa?

    Sioni hata maneno yanayosema uchunguzi wa tukio unafanyika bali manacompare matukio and then what????

    Nyie watu nyie hii ingetokea mitaa ya Oyster bay, Masaki , msasani mngeact the same? Try to walk a mile on those parents' shoes and feel it...How would you feel if you loose your baby? Nyie watu nyie fanyeni kazi mlizotumwa kufanya. Nyie ndio watetezi wa hao watoto...Hizo biashara manaziachia ziendeshwe kiholela bila kujali lakini siku ya mwisho mtajibu maswali mengi sana kwa mwenyenzi Mungu. Hapa duniani you guys are fine, mnaishi sehemu nzuri, watoto wenu wanaenda kwenye kumbi zinazoeleweka lakini mkumbuke kuna siku ya mwisho hao watoto watawauliza maswali mengi sana na nyie siku yenu ikifika...

    Sioni hata sehemu moja inayosema upchunguzi wa tukio hili unaendelea ...Hatua gani zinachukuliwa yaani case closed maisha yanaendelea...Aghhhh I feel for my fellow citizens who have nothing....

    ReplyDelete
  2. Nawapa pole waliofiwa... pia namuunga mkono "A-Mother-to=be" juu ya hatua ambazo serikali ilipaswa kuchukua mapema kukagua hizi kumbi na kuhakikisha usalama... ila jamani pia wazazi wa watoto hawa.. hili disko toto lilikuwa usiku.. tena katika bar.. iweje umruhusu mwanao wa miaka 6 au 8 kwenda mahali kama hapo usiku pengine bila hata wewe kuwepo? Disko toto zimekuwepo tangu miaka mingi ila zilikuwa zinaanza saa 8 hadi 10 jioni. Ninawasihi wazazi kuwa makini kuwa na watoto wao wadogo hasa siku hizi za sikukuu.. Poleni mliofiwa ila wengine tujifunze kuwalinda watoto wetu.

    ReplyDelete
  3. HII SI HABARI NJEMA, TUNATAKA ITUELEZE HATUA ZA KISHERIA ZITAKAZOCHUKULIWA DHIDI YA WAHUSIKA KURUHUSU WATOTO CHINI YA MIAKA KUMI NA MINANE KUINGIA BAA WAKATI SHERIA YA VILEVI HAIRUHUSU WALA HAISEMI ENDAPO TU KUTAKUWA NA DISCO NDANI YA BAA BASI WATOTO WATARUHUSIWA KIINGIA. TUKIO LA TABORA MPAKA SASA LIMEACHA MASWALI BILA MAJIBU KWANI WAHUSIKA WAKO JUU YA SHERIA. Kwako Michuzi nenda Wizarani utuletee majibu ya kosa lililotendeka.

    ReplyDelete
  4. Katibu mkuu ni Mariam J Mwaffisi ua siye?

    ReplyDelete
  5. Wadau, hii inaonyesha ni kwa kiasi gani tusivyojali maisha ya watoto na kutenga sehemu maalumu za watoto kwa ajili ya kucheza na kufurahi hasa siku za sikukuu.Mimi binafsi yangu sioni kama ni lazima watoto waende kwenye disco la ndani.lakini hii inatokana na ufisadi uliokithiri unaopelekea kuuza hadi viwanja vya wazi ambavyo ndio vilikuwa vikitumika hapo zamani kwa ajili ya watoto kucheza na michezo ya watoto ya kiaskini ya huku kwetu kama bembea. nasema hivyo kwa uchungu kwa sababu wenzetu wana mipango mizuri ya watoto wao kupata sehemu za kuchezea zenye usalama na zinazoeleweka. Watoto etu hawana sehemu hizo na uwezo wa kupelekwa waterworld haupo wafanyeje? wanaishia kwenye makumbi ya disco na kufa. Wadau mnaopenda watoto nafasi bado ipo hebu tubuni michezo na sehemu za watoto kucheza kwa usalama hasa sikukukuu na muwekeze huko sio beach wala disco.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...