Chuo cha Muziki cha Zanzibar, DCMA, kinapenda kuwataarifu waandishi wa habari kuhusu Walimu wake ambao wanaendesha warsha ya Muziki wa Taarab asilia kisiwani Mayotte kama ifuatavyo: -

Walimu wanne kutoka Chuo cha Muziki cha Nchi za Jahazi (DCMA) cha Zanzibar, wameondoka nchini tarehe 7 Oktoba 2010 kwa safari ya kuelekea kisiwani Mayotte kwa ajili ya kuendesha warsha ya muzeka wa Taarab asilia. Warsha hiyo ambayo imeandaliwa na kufadhiliwa na Idara ya Utamaduni ya Mayotte itafanyika kuanzia tarehe 7 hadi 25 Oktoba, 2010. Walimu watayoendesha warsha hiyo kwa niaba ya Chuo cha DCMA ni Mohammed Issa ‘Matona’, Rajab Suleiman, Mohammed Othman na Kesi Juma.

Warsha hiyo itajumuisha mafunzo ya ala mbali mbali zinazotumika katika muzeka wa Taarab asilia zikiwemo Udi, Fidla (Violin) na Qanun. Zaidi ya mafunzo katika upigaji wa ala hizo, mengine yatakayofundishwa ni pamoja na mbinu za uimbaji wa tungo za Taarab pamoja na upigaji wa pamoja katika kundi yaani Taarab Ensemble Play.

Kwa mujibu wa waandaji wa warsha hiyo, washiriki kadhaa kutoka kisiwa cha Mayotte pamoja na visiwa ndugu vya Shirikisho la Komoro wamealikwa kushiki katika mafunzo hayo yatayotolewa bure. Zanzibar na Komoro zina mahusiano ya kitamaduni kutokana na sehemu zote mbili kuwa na historia zinazolingana kutokana na athari za karne za mahusiano na ulimwengu wa Kiarabu na wakiislamu.

Katika kipindi cha warsha hiyo, walimu wa mafunzo hayo watashirikiana na wanafunzi wao katika kufanya maonyesho mawili ambayo wanategemewa kuwavutia wapenzi wengi wa muzeka wa Taarab asilia ya Zanzibar wanaoishi Mayotte.

Hii ni mara ya pili kwa walimu wa DCMA kuendesha mafunzo katika maeneo ya visiwa vya Komoro na Mayotte, mara ya kwanza ikiwa mwaka jana ambapo mafunzo hayo yalifanyika katika kisiwa cha Moroni kupitia hisani ya ofisi ya UNESCO Tanzania. Mbali na mafunzo hayo, wasanii kutoka Zanzibar na Komoro wameshawahi kushirikiana mara kadhaa katika kazi za kisanii hasa katika muzeka wa Taarab asilia ikiwemo ushirikiwa pamoja katika Tamasha la Busara linalofanyika Mji Mkongwe kila mwezi wa Februari.

Taarab asilia ya Zanzibar ndiyo aina ya muzeka unaopendwa zaidi visiwani Komoro licha ya kuwa muzeka huo hujulikana kwa jina la Twarab na kujumisha ala za ziada kama vile Gambusi na Ndzendze. Mbali na muzeka wa Twarab, aina nyengine za muzeka unazopendwa nchini humo ni Sega wenye asili visiwani Mauritius na Reunion.

Tunaomba hisani ya kuchapishwa taarifa hii. Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana nasi kupitia anwani ifuatayo: -

Kheri A. Yussuf
Development, Marketing & PR Manager
Dhow Countries Music Academy, Zanzibar
Mobile:077.362 0202
E:press@zanzibarmusic.org

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. haya tena passport za kifaransa hizo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...