Mstahiki Meya wa Iringa aliyemaliza
muda wake Mh. Amani Mwamindi
Na Francis Godwin, Iringa


ALIYEKUWA mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa awamu iliyopita na diwani mteule wa kata ya Mlandege Mheshimiwa Amani Mwamwindi amejitokeza kuchukua fomu ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) kuomba ridhaa ya kuwa mmoja kati ya wagombea wa nafasi hiyo ya umeya huku akiahidi kushughulikia kero ya michango katika shule za msingi .

Akizungumza na mwandishi huyu leo mara baada ya kutoka kuchukua fomu ya kuomba kugombea umeya katika mchakato wa ndani ya CCM,Mwamwindi amesema kuwa moja kati ya kero kubwa ambayo madiwani wa Manispaa ya Iringa wamekuwa wakiombwa na wazazi kuishughulikia ni pamoja na baadhi ya shule za msingi kudai wazazi michango mingi na kuwafukuza watoto wanaoshindwa kulipa michango hiyo .

Mwamwindi amesema kuwa iwapo atabahatika kuteuliwa na chama kuwa mgombea wa nafasi hiyo na madiwani wenzake wakamchagua kuwa meya wa Manispaa ya Iringa kwa kipindi cha pili atahakikisha anashirikiana na madiwani hao kupitia vikao vya baraza la madiwani ili kuondoa kero hiyo ya shule kuendelea kutoza michango mingi kuliko hata awali kabla ya ada kwa shule za msingi kufutwa.

Kwa upande wao wananchi wa Manispaa ya Iringa pia wamepata kumpongeza Mwamwindi kwa uamuzi wake wa kujitokeza kuwania tena nafasi hiyo na kuwa bado wananchi wamekuwa na matumaini makubwa na uongozi wake japo wameomba iwapo atachaguliwa tena kusaidia kutatua kero mbali mbali ikiwemo ya michango isiyo na kikomo kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Mchakato wa ndani ya chama cha mapinduzi wa kumpata mgombea wa nafasi ya umeya wa Manispaa na naibu meya umeanza ndani ya chama hicho japo hadi sasa ni wanachama wawili pekee ndio ambao wamejitokeza kuchukua fomu akiwemo Bw Alphonce Mlangala ambaye alipata kuwa naibu meya miaka ya nyuma na kuongoza nafasi hiyo kwa kipindi kimoja pekee na kuangushwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. jee huyu ni mtoto wa Marehemu Mwamwindi yule tunayemkumbuka kwenye historia katika miaka ya sabini?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...