Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA),Ezekia Wenje.

UKUMBI wa Bunge jana ulitawaliwa na maneno na misemo mikali kiasi cha kumfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kumshauri Spika wa Bunge, Anne Makinda aamuru askari wa Bunge wamkamate Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA),Ezekia Wenje na kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge kutona na kuchafua hali ya hewa wakati Bunge liliendelea.

Hatua hiyo ilikuja kutokana na kitendo cha Mbunge huyo kudai kuwa Kamati ya Bunge ya Uongozi, ilifanya uamuzi kinyume cha Kanuni za Bunge na kukiita kitendo hicho kwamba ni "dark market" (mambo yasiyofuata utaratibu).

Kauli hiyo ilitokana na hatua ya Spika Makinda kuwasilisha majina matatu ya wagombea wanaotakiwa kuchaguliwa kuwa wenyeviti wa Bunge, huku kanuni zikitaka kuwasilishwa kwa majina sita ili yapigiwe kura.

Majina yaliyowasilishwa yalikuwa ni ya George Simbachawene (Kibakwe), Jenista Mhagama (Peramiho) na Sylivester Mabumba (Dole) kwamba ndiyo wanaotakiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo.

Baada ya kutaja majina hayo, Wenje aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya kumi na moja akisema uamuzi huo unaonyesha kuwa Kamati ya Uongozi, haikufuata utaratibu. Alisema hayo kwa kutumia neno la Kiingereza, ‘dark market.’ Kauli hiyo ilionekana kumuudhi Makinda na wabunge wa CCM.

Kundi kubwa la wabunge wa chama hicho (CCM) lilisimama na kumtaka Spika kumfukuza Wenje ndani ya ukumbi wa Bunge.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Raya Ibrahim Khamisi alikoleza moto huo baada naye kuomba mwongozo wa Spika akimweleza kiongozi huyo wa Bunge kuwa alitaka kuendesha uchaguzi bila ya kufuata Kanuni za Bunge.

Raya aliomba mwongozo huo baada Makinda kuwaeleza wabunge kuwa uchaguzi wa wenyeviti wa Bunge ungefanyika kwa kupigia kura majina matatu ya wabunge waliopitishwa na Kamati ya Uongozi.

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, toleo la 2007 kanuni ya 11, uchaguzi huo utafanyika kwa kupigia kura majina sita na kati ya hayo, matatu yatakayopata kura za juu yatathibitishwa na Bunge kuwa wamechaguliwa. Kanuni ya 11 (1) (a) inasema: Karatasi ya kupigia kura itakuwa na majina sita ya wabunge ambao wamependekezwa na Kamati ya Uongozi kupigiwa kura kutoka miongoni mwa wenyeviti na makamu wa wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge.

Kununi ya 11(b) inasema: Kila mbunge atapiga kura kwa kuchagua majina matatu katika orodha hiyo; na(c) Wagombea watatu watakaopata kura nyingi kuliko wengine ndiyo watakuwa wamechaguliwa kuwa wenyeviti wa Bunge.

Makinda alisema walipitisha majina hayo matatu baada ya Kamati ya Uongozi ambayo inashirikisha kiongozi wa upinzani na naibu wake kujiridhisha kuwa wengine kwenye kamati hiyo hawakuwa na sifa.

Raya aliomba mwongozo wa Spika na akasoma kanuni ya 11 ya Bunge kifungu (a) na (b), vinavyoonyesha kupingana na wazo la Spika la kutaka wabunge hao wachaguliwe bila kuvunja kanuni hiyo kwanza.Hoja ya Raya iliungwa mkono na kambi ya upinzani huku wabunge wa kambi hiyo wakianza kusimama mmoja baada ya mwingine kupinga wenyeviti hao kuchaguliwa kwa kura ya ndiyo na hapana, au ikubalike kuwa kanuni ya 11 ivunjwe kabla ya kufanya hivyo.

“Raya, naomba unielewe kazi ya kukaa hapa mbele siyo mchezo na inahitaji mtu ambaye ni ‘very strong’ (madhubuti), kwa hiyo sisi tumekubalina hivyo na itakuwa hivyo halafu kitu kingine ni kwamba ninyi huwa mnakimbilia mbele zaidi hata kabla Spika hajafika huko,” alisema Makinda na kuongeza:“Tatizo jingine ninyi wa Chadema ni kwamba huwa mmejipanga kwamba huyu akazungumze hiki na huyu akazungumze kile kwa hiyo mnakurupuka sana wakati mwingine.”

Majibu hayo hayakuonekana kutuliza hali ya hewa katika ukumbi wa Bunge kwani wabunge waliendelea kutupiana maneno kama sokoni, hali iliyomlazimu Jaji Werema kusimama na kusema kwamba amevumilia kiasi cha kutosha na hivyo uvumilivu wake umefika mwisho.

“Mheshimiwa Spika, nimevumilia kwa muda mrefu na vya kutosha sasa ni wakati wa kuchukua hatua tena kali, hivyo naomba Sajent of Arms itumike hapa,” alisema Jaji Werema. Baada ya Jaji Werema kumaliza, Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Zitto Kabwe, alisimama na kutoa ufafanuzi wa maneno aliyotumia Wenje na kuomba mbunge huyo asiadhibiwe.

Kauli ya Zitto iliamsha hisia za wabunge wengi, kwa pamoja walisimama Livingston Lusinde, Peter Selukamba, Ferister Bura na Halima Mdee ambaye alipewa nafasi ya kuzungumza na kusema kambi rasmi ya upinzani bungeni haitakubali kupiga kura za ndiyo na hapana kwa nafasi ya wenyeviti hadi kanuni ya 11 itakapovunjwa hata kama Wenje atafukuzwa.

Wabunge wa CCM walianza kuzungumza bila ya utaratibu baada ya kuomba nafasi kwa Spika na kunyimwa, huku wengi wakipiga kelele za Wenje kuondolewa bungeni na wengine wakisema: “Apelekwe kwa Babu akanywe kikombe.”

Majibizano hayo yaliendelea kwa zaidi ya dakika 10, huku Spika akionekana kupandwa na jazba na wakati huo alikuwa akilumbana na kila upande, wakiwamo wabunge wa CCM ambao walikuwa wakipiga kelele za kutaka Wenje afukuzwe ndani ya ukumbi. Baadhi ya maneno yaliyosikika kutoka kwa wabunge wa CCM, ni: “Hawana adabu, wamezoea kukurupuka...” huku wengine wakisema kama wanamtetea Wenje basi watoke nje wote, lakini uchaguzi lazima ufanyike.

Kwa upande wa upinzani kulisikika maneno ya “CCM hawana adabu, CCM mnafanya fujo...” huku Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbles Lema, akizungumza kwa sauti ya juu na kusema; “Fungeni milango tupigane.”

Kwa upande wa upinzani, Zitto alisimama na kuanza kuwakemea wabunge akiwataka kunyamaza ingawa na yeye alitumia nafasi hiyo kuzungumza kwa jazba na kusema: “Hatoki mtu hapa.”

Baada ya kuona hali imekuwa tete, Spika alilazimika kukubaliana na hoja ya Raya na alimsimamisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ambaye aliomba Bunge likubali kuvunja kanuni ya 11 ili kuruhusu wenyeviti hao kuchaguliwa licha ya kuwa haki ya wagombea haitimii. Baadaye wabunge hao walikubaliana kuvunja kanuni hiyo na kupiga kura ya ndiyo au hapana kwa wabunge hao watatu.

Kufuatia hali hiyo, wabunge wa upinzani wakiongozwa na wabunge wa Chadema walipiga makofi kwa wingi wakiashiria ushindi kwani kile walichokuwa wakikihitaji ndicho kilichofanyika. Hata hivyo, Makinda kabla ya kutangaza kukubaliana na wazo hilo, alimwambia Wenje kuwa awe na adabu ndani ya vikao na kumwomba afute kauli yake huku akimbembeleza kuwa kufuta kauli siyo dhambi.

Wenje alisimama na kusema kauli aliyoitumia ya dark market anaifuta na badala yake iingie kwenye kumbukumbu neno white market.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Duh kaaazikwelikweli... nakumbuka nikiwa mdogo mdogo hivi nilifunzwa na mama kuwa kuchafua hali ya hewa ni ku*amba.... sasa ninapoona atii mbunge amechafua hali ya hewa bungeni huwa najaribu kuona jinzi gani ukumbi unakuwa na ki*ambo hicho na namna kinavyoweza kuleta tafrani kwa wadau humo ndani. Hoja yangu hapa - Je hatuna neno jingine hapo??? Tehe teh te..

    ReplyDelete
  2. Ukisoma vizuri utagundua kuna wabunge wa chama fulani wamewakamia wabunge wa chama kingine..hapa kuna hatari hawa wabunge waliwakamia wenzao wakafanya maamuzi duni na kwa maslahi ya chama chao badala ya Taifa na wananchi waliwachagua..Spika wa bunge asiwe na upande wa chama..na kuna wabunge wa chama kingine ambao wanajua wamekamiwa na wanajua kila issue watakayo fanya wa kipindi hiki ambacho wananchi wamechoshwa ni dili..Pia mwandishi angefafanua wajumbe wa upinzani walioko kwenye kamati iliyopitisha majina matatu ni upinzani upi..wa mlango wa kulia au upinzani wa mlango wa kushoto..kwani kuna wapinzani wako karibu na mlango wa chama tawala...

    ReplyDelete
  3. Ankal hii habari kama ungeipost na video yake ingependeza sana maana sio wote wanapata muda wa kuangalia vipindi vya Bunge.

    ReplyDelete
  4. Haya, Sijui mnagombania nini! Hawa wanataka kupitisha kinyemela kamati, wengine wanataka 'utaratibu' (na kamati hiyo hiyo ipite)! Kama Kamati mnaona inafaa, mnahangaika nini?

    ReplyDelete
  5. ahsante wenje kwa kuwashutua hawa jammaaa wanasahu sheria

    ReplyDelete
  6. Mtoto wa kabwela,SwedenApril 14, 2011

    Hawa wabunge na wanasiasa wanacheza na maisha ya WaTanzania.Tanzania inabidi kutawaliwa kidikteta kwa muda fulani hadi hapo maendeleo ya kweli yatakapopatikana.Bunge na siasa zimekuwa mzigo kwa walipa kodi.Vunja bunge na vunja vyama vyote vya siasa.Tanzania haitaki kuendelea,kama waengineer wote unakamata na kufungia chumba kimoja na kuwaambia waje na idea fulani na hapo ndio watafunguliwa.Na hiyo iwe kwa fani zote.

    ReplyDelete
  7. Bunge la sasa hivi limejenga chuki kati ya wabunge wa CCM na CHADEMA. Na huu ndo upinzani halisi kwani zamani watu walikuwa wanaogopa kusema lakini sasa watu hawadanganyiki tena wanaijua sheria ya bunge vilivyo.Hii inaonyesha ni jinsi gani CCM walivyokuwa wakivunja sheria nyingi za bunge hasa katika kufanya maamuzi na chaguzi mbalimbali. Wakati umefika kuwa na upinzani wa kweli kwa manufaa ya kutetea maslahi ya umma sio kwa wabunge kutafuta umaarufu bunge.
    Wabunge wote wa CCM na CHADEMA wanatakiwa wawe na hekima wanapokuwa Bungeni kwa kwa kusikiliza nini kilichokuwa kinaendelea bungeni jinsi walivyokuwa wakizozana utafikiri ni wanafunzi wa sekondari na dada mkuu wakizozana. Spika anatakiwa atawale bunge kwa mamlaka ya sheria inaonekana wakati mwingine anazidiwa na anashindwa ku-control wabunge na bado hajazijua sheria nyingi za bunge. Anatakiwa kuwa na mwanasheria pembeni mwenye kuvijua vifungu na kanuni mbalimbali za bunge ili kunapotokea tatizo kama la jana aweze kulishughulikia kisheria mara moja pasipo kuchemsha. Inavyoonekana asipofanya hivyo atakuwa anachemsha mara kwa mara na ataoneka kama vile kiranja mkuu akiongoza wanafunzi wa O level.
    Please ankal usiwe na nidhamu ya woga katika ku-post maoni ya wadau kwani pale watu wanapozungumza points za maana wewe huwa unatia kapuni. Hiyo ni nidhamu ya uoga na sio uandishi wa habari, kwani blog hii ni kioo cha jamii na viongozi lazima wapate maoni ya watanzania jinsi wanavyo fikiri ili waweze kujirekebisha. Hii itakufanya uchukue umaarufu na hautaonekana kana kwamba unaogopa chama fulani kwa maslahi yako binafsi hiyo sio demokrasia ya kweli! Kwahiyo please hata hajatukana mtu bali ni maoni ya mzalendo anayetegemea mabadiliko ndani ya bunge letu. Asante kwa kunielewa.
    Idumu Globu ya jamii!

    ReplyDelete
  8. Sasa mwanasheria wa serikali nae aende kwa babu akanywe kikombe jamani. Mbona hamna tusi hata moja hapa au ndio kubeleza vyeo. Eti nimevumilia mpaka uvumilivu umeisha basi ondoka nenda nyumbani ukapumzike, polisi wa nini bungeni kwani luna mwizi msiliomba kura wenyewe. Nyie ccm acheni komedi

    ReplyDelete
  9. Kama mnadhani watu wa upinzani walikuwa wajinga mnatakiwa mjifunze zaidi kuhusu "The Rule of Law"...sasa bunge lazima (kama chombo kinachotunga sheria) lionyeshe mfano wa kufuata sheria....!! Kwani nini kigumu hapa? Angalia speech ya Nyerere mwaka 1995 na Press Club..alisisitiza sana hilo: http://www.youtube.com/watch?v=5EaDI3sRqUU&feature=related

    ReplyDelete
  10. Hawa ccm wanachekesha kweli. Hawajui kama huu si wakati wa chama kimoja. Nafikiri hangover za kutoka chama kimoja bado zinawasumbua. Wataiyumbisha nchi wasipoangalia. Najua wanataka kuimaliza chadema. Hivyo ndio mnawajenga. Hamtawamaliza kwa mtindo huo. Na mwanasheria naye ni kimeo tu. Alishaonekana tangu alipochaguliwa kuwa anataka kujipendekeza kwa ccm badala ya kusimamia sheria. Sasa hapo kuna kosa gani kubwa mpaka polisi waitwe? Watu kama hawa ndio watatuletea matatizo. Mliona alivyokuwa anakataa kuandikwa kwa katiba akifikiri anamfurahisha raisi kumbe raisi alishasoma nyakati.

    ReplyDelete
  11. CHADEMA NAWAPA PONGZI NA WANANCHI TUWASIFU WABUNGE WA CHADEMA.BUNGENI SIO SEHEMU YA MCHEZO NI SEHEMU AMBAYO MWAKILISHI WAKO AKILALA SHERIA MBAYA IKIPITISHWA WEWE MWANANCHI UPO MATATANI KWA HIYO NAWAPA PONGEZI CHADEMA MUWE KARIBU NA WANANCHI CCM WAO NI KUWAONA WANANCHI WALIOWACHAGUA KUWA HAWANA AKILI.NAPENDA KUWAAMBIA WATANZANIA ANGALIA KWENYE WEB SITE BUNGE LA VENEZUELA WABUNGE WANAPIGANA KWA KUTETEA WANANCHI SIO SISI ETI BUNGE NI SEHEMU TAKATIFU ILI WATUIBIE

    ReplyDelete
  12. Hivi huyo kiranja wao alisikia yule aliyesema :funga mlango tupigane:'kama mapigano yangetokea ingekuwa ni yeye,maana kapindisha sheria ya bunge,kafikiria wamelala amesahau chadema ni wanasheria watupu,kiranja namsihi aache ghadhabu,ajifunze kupokea changamoto kwa uso wa matumaini,zingepigwa ingekula kwake,kweli awe na mwanasheria karibu, kiranja ngoja bunge la June,nitashawishi uwe unakaa na mwanasheria pembeni kama mkalimali,boss wako sita ni mwanasheria,halafu kichwa,ndo maana mafisadi wakamtosa wakaona ukae weye uwalee, pole sana mamie!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...