Tasnia ya muziki wa injili Tanzania imezidi kukua na hatimaye kuzidi kufikia malengo yake ya kulitangaza neno la Mungu kupitia muziki. Hii imedhihirika wazi kutokana na kila kukicha kuibuka kwa watumishi wapya wenye vipaji machachali katika muziki huo.
![]() |
Bertha Samwel |
Bertha Samwel ni mmoja kati ya wanamuziki wapya wanaoibukia kwa kasi katika muziki wa injili . Mwanadada huyo anatamba na wimbo unaokwenda kwa jina la “NISAIDIE BABA” akieleza kuwa anapenda kutenda mambo mema lakini anajikuta lile baya analolichukia ndilo analotenda kwahiyo anamuomba Mungu amsaidie na amuongoze kwa maana peke yake hawezi. Ama kwa hakika ukiusikiliza wimbo huo unagusa sana mioyo na maisha ya watu ya kila siku.
Bertha ambaye asili yake ni Kyela,mkoani Mbeya ameanza kuimba muziki wa Injili tangu akiwa mtoto kipindi akihudhuria Sunday School huko Mbeya. Kwa sasa ni mwanachuo katika chuo cha Tumaini na anakaribia kukamilisha album yake ya kwanza ya muziki huo wa Injili ambayo bado hajaipa jina.
Anasema kuwa maneno yanayoimbwa na waimbaji wa muziki wa Injili ni mahubiri tosha, kwahivyo anawaomba mashabiki wa muziki huo wasikilize muziki wao kwa nia ya kupata habari njema za wokovu na si kuburudika tu kama baadhi yao wanavyofanya, “Ujue unaposikilizia muziki wa Injili utakuta kuna ujumbe fulani wa kiroho, ujumbe wa kuokoa na kubadilisha maisha ya mtu kwahivyo ninawasihi mashabiki ni vyema kusikiliza kwa umakini na kuyazingatia tunayoyaimba kwa maana ni ujumbe tosha ambao bwana anatupatia kupitia roho mtakatifu tuuimbe kuufikisha kwetu na kwao pia” alisema Bertha.
Hivi karibuni Bertha atazunguka kufanya maonyesho akimsindikiza mwanamuziki wa muziki wa Injili K BAZIL ambaye hapo awali alikua akiimba muziki wa Bongo fleva akitamba na wimbo wa RIZIKI aliowashirikisha Stara Thomas na Bizman katika uzinduzi wa album yake ya kwanza ya muziki wa Inili inayokwenda kwa jina la “YESU ANANIPENDA” . Crispin Challe ambae ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ufufuo Music & News Blog site (www.ufufuomusic.blogspot.com) ambao ndio waandaaji wa tamasha hilo amesema tamasha hilo litafanyika kwa mara ya kwanza katika mkoa wa Iringa siku ya Jumapili ya tarehe 5/06/2011 na baadae kuendelea kufanyika katika kila mkoa amabapo K BAZIL amewahi kufanya shoo akiwa kwenye muziki wa Bongo fleva kabla ya kuja kumalizikia Jijini Dar es salaam.
Safi sana Bertha, waambie hao wanaotafuta pesa ama kusikiliza kwa kuburudika, tumeona wengi wakiimba nyimbo za injili na wakizicheza kwa kama dansi la akudo lakini hawaangalii kilichoimbwa. Watu tusikilize ujumbe mungu akubariki
ReplyDelete