Na Mwandishi Wetu.
Watanzania wataungana na mataifa mengine Duniani kote kuadhimisha ya siku ya mazingira duniani ambapo , Maadhimisho ya Siku hii kwa mwaka huu nchini, yatafanyika mjini Songea, mkoa wa Ruvuma na yataambatana na uzinduzi wa sherehe ya kihistoria ya kumbukumbu za Taifa letu za maadhimisho ya miaka hamsini ya Uhuru.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya makamu wa Rais Mazingira Mh. Dkt. Terezya Huvisa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Dkt Huvisa aliongeza kwa kusema kuwa, kupitia maadhimisho haya, serikali itapata fursa ya kutathmini hali ya Mazingira nchini, juhudi mbalimbali zinazofanywa katika kuhifadhi Mazingira, Mafanikio na changamoto za Mazingira kwa kipindi cha miaka hamsini ya Uhuru.
Aidha, Dkt Huvisa alisema kuwa, Maadhimisho ya mwaka huu yanaambatana na uhamasishaji wa wananchi wote kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhifadhi Mazingira, kupitia Mikakati mbalimbali na wananchi pia, wanahamasishwa kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji kwa kushiriki katika mashindano ya Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi vyanzo vya Maji, Kupanda na Kutunza Miti kwa kujaza fomu ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira ya mwaka 2012 ikiwa ni pamoja na pesa taslimu.
Dkt Huvisa alianisha kuwa, tangu nchi ipate uhuru miaka 50 iliyopita, matatizo ya mazingira nchini yameendelea kujitokeza akisema kuwa miongoni mwa matatizo makubwa ni pamoja na upotevu na uharibifu wa misitu ya asili kutokana na kilimo kisichoendelevu, matukio ya uchomaji moto ovyo na ufyekaji wa misitu ovyo kwa ajili ya shughuli za ujenzi, utafutaji madini na nishati ya mkaa.
Akifafanua zaidi, Dkt Huvisa alisema, taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba takriban hekta za misitu zipatazo laki nne, hufyekwa na kuharibiwa hapa nchini kila mwaka kutokana na sababu hizo na kusababisha uharibifu wa vyanzo vya maji na ardhi na aliongeza kuwa, ongezeko kubwa la idadi ya watu mijini na vijijini limesababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa taka na hivyo kusababisha kuzagaa kwa uchafu na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya mijini na vijijini.
Akifafanua zaidi Dkt Huvisa alisema, Katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru na Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu, wadau wote wa Mazingira ikiwemo Wizara za kisekta, mikoa, taasisi za Serikali, viwanda, mashirika yasiyo ya kiserikali, kamati za mazingira na kamati za afya za mikoa, serikali za mitaa na vyombo vya habari, zitumie fursa hii kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa maudhui ya ujumbe wa kitaifa wa maadhimisho haya, hususan kuhamasisha wananchi wote juu ya kupanda miti na kuhifadhi misitu na uoto wa asili pamoja na kuepuka uchafuzi wa mazingira wa aina yoyote.
Kitaifa kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Miaka Hamsini ya Uhuru, “Panda Miti na Kuitunza: Hifadhi Mazingira”.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...