- Kila timu yatamba kunyanyua kombe
MACHO yote na masikio leo yanaelekezwa Mjini Arusha ambapo vijana wa Ziwa Nyasa na wale wa Ziwa Victoria, Mbeya na Mwanza wanatarajiwa kushuka dimbani katika fainali ya Kili Taifa Cup 2011.
Fainali hiyo inatarajiwa kuanza saa tisa na nusu katika Uwanja wa Kumkukumbu ya Sheikh Amri Abeid Mjini Arusha.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) mgeni rasmi katika fainali ya leo ni
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Kassim Majaliwa, ambaye ndiye atakayekabidhi kombe kwa bingwa wa mwaka huu.
Wakizungumza jana makocha wa timu hizo zilizofuzu fainali, kila mmoja alitamba kulinyakua kombe na kulipeleka nyumbani.
Mbwana Makata wa timu ya Mbeya alisema wana uhakika na kikosi chao kucheza vizuri na kunyakuwa ubingwa huo kwani wamejiandaa vilivyo.
"Wachezaji wetu wapo vizuri tunajiamini tutafanya vizuri katika mchezo huo na kuondoka na kombe"alisema Makata.
Naye kocha John Tegete wa Mwanza alisema wana uhakika wa kulipeleka kombe Mwanza kwani wachezaji wake wana ari kubwa ya kushinda.
"Ubingwa ni wetu..wachezaji wetu wapo sawasawa kimchezo hatuna wasiwasi Bingwa ni Mwanza"alisema Tegete, Baba mzazi wa mchezaji Jerryson Tegete.
Mwanza imekuwa ikimtumia sana mchezaji Jerryson Tetege ambaye ndiye amekuwa kinara wa mkoa huo kwa kuweza kufunga magoli katika kila mechi waliocheza.
Kwa upande wa Mbeya kinara wake wa kupachika magoli ni Gaudence Mwaikimba, ambaye amekuwa akiisaidia timu yao kupata magoli kila mechi hivyo katika mchezo huo kutakuwa na vita ya wachezaji wawili Tetege na Mwaikimba, kila mmoja akipani kuwa mfungaji bora wa mashindano.
Mwaikimba anaongoza kwa magoli saba hadi sasa wakati Tegete ana magoli sita hadi mechi za juzi za nusu fainali.
Tayari wakuu wa mikoa ya Mwanza na Mbeya, Abbas Kandoro na John Mwakipesile wametambiana kuwa kila mmoja atachukua ubingwa.
Kandoro alisema juzi kuwa hatakuwepo kwenye fainali ya leo kwani ana majukumu mengine ya kiofisi lakini ametuma wawakilishi kwenda kuwapa vijana nguvu ya kushinda.
Kwa upande wake Mwakipesile amesema licha ya kutuma watu mapema kuwapa vijana nguvu, yeye mwenyewe atakuwepo kwenye fainali ya leo ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa mpira nchini.
Bingwa wa michuano hii atajinyakulia kitita cha sh.milioni 40,mshindi wa pili atajinyakulia sh.milioni 20 na mshindi wa tatu atajinyakulia sh.milioni 10.
wengine ni mchezaji bora wa mashindano sh. Milioni 2.5,mfungaji Bora sh.milioni 2,kipa bora sh.milioni2 na kocha bora sh.milioni 2.
Mashindano haya ambayo yamechukua takriban wiki tatu yamezua hamasa kubwa kote nchini huku mabingwa wa mwaka jana, Singida, wakiondolewa katika hatua ya robo fainali.
Mashindano ya Kili Taifa Cup yamedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premium Lager. Kampuni hii imedhamini mashindano haya kwa miaka minne sasa mfululizo.
Masuala ya habari yamedhaminiwa na
Kampuni ya Executive Solutions.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...