![]() |
| Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Shariff Hamad |
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inahitaji kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 123 kuweza kumaliza tatizo la maji safi na salama kwa Mikoa ya Unguja na Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Shariff Hamad ameuambia ujumbe wa viongozi wa Jumuiya ya Madhehebu ya Khoja Shia Ithinashir kwamba tatizo la maji safi na salama linafanyiwa kazi na kwa sasa zinahitajika fedha hizo kuweza kukamilisha miradi ya maji. “Kama mnavyofahamu Zanzibar kuna tatizo la maji, Serikali haijakunja mikono, mipango mbalimbali inafanywa kukabili tatizo hilo” Alisema Maalim Seif.
Maalim Seif amesema ikiwa fedha hizo zitapatikana basi matatizo yanayowakabili wananchi wa Visiwa vya Zanzibar kukosa maji safi na salama litakuwa historia hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kuwa na subira. Akizungumzia suala la umasikini,Makamu huyo wa kwanza wa Rais amesema Serikali imedhamiria kuwakwamua wananchi wake katika dimbwi la umasikini kwa kubuni mipango mbalimbali yenye tija kwa umma.
Maalim Seif amesema kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazoendelea ambazo zinakabiliwa na hali ya umasikini, lakini pamoja na hali hiyo, bado kuna matumaini ya kupunguza kwa kiasi kikubwa hali hiyo chini ya mpango mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini(MKUZA) Sekta kadhaa zimetajwa chini ya mikakati ya kupunguza umasikini katika
Visiwa vya Zanzibar huku kiwango cha elimu kikitarajiwa kuimarishwa sanjari na ukuzaji wa Sayansi na Teknolojia.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais, amesema masuala ya afya ya jamii yamekuwa wakipewa kipaumbele ili kujenga jamii yenye afya bora ambayo itashiriki katika uzalishaji mali. Alisema kwa kuwa na watu wenye afya bora kunasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wan chi kwani muda mwingi utatumika katika uzalishaji mali na sio kwenye matibabu, hivyo aliwahakikishia msimamo wa Serikali kuimarisha sekta ya afya Zanzibar.
Maalim Seif amepongeza uamuzi wa Jumuiya hiyo kujenga kituo cha afya ambacho kinatumika na wananchi wote ambacho kinazingatia zaidi utoaji huduma kwa njia isiyo ya kibiashara.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...