
Leo ratiba ya tamasha la 14 la ZIFF imetoka ikionyesha kuweko filamu 71 kutoka
nchi 39 zitakazoonyeshwa katika siku 10 za tamasha. Pamoja na maonyesho ya
filamu kutakuwepo vilevile warsha kubwa 8 zitakazofundisha utengenezaji wa filamu
za dokumentari na pia ufundi wa kutumia kamera za HD.
Zaidi ya hayo kutakuwa pia na dhifa kadhaa pamoja na maonyesho ya filamu vijijini
yanayodhaminiwa na The Cinema Mondial Tour ya Uholanzi. Filamu hizo pamoja na
za ZIFF zitaonyeshwa katika vijiji visivyopungua 15 hapa Unguja na Pemba.
Lakini cha kuvutia zaidi ni kuweko kwa mpiga muziki maarufu Shaggy katika ZIFF.
Mjamaika-Mmarekani huyu anajulikana zaidi kwa wimbo wake “It wasn’t Me”
uliowakoroga vijana akionyesha utundu wake kimuziki.
“Kwa kweli mwaka huu najisikia sana mimi” alisema Dr Martin Mhando,
mkurugenzi wa tamasha la ZIFF. “
Ukiacha Shaggy mwaka huu filamu itakayofungua
dimba ni filamu inayohusu muziki na wanawake itokayo Canada/Uganda
inayoitwa “Making The Band”.
Filamu hii na kuja kwa Shaggy kutatimiza sherehe za Mwaka wa Umoja Wa Mataifa unaosherehekea mahusiano kati ya waafrika walio barani na wale walio nje ya Afrika. ZIFF inahimiza sana mahusiano hayo”
Kwa upande wa filamu, mkazo utakuwa juu ya filamu za dokumentari ambapo
mtengenezaji mahiri Nick Broomfield wa Uingereza atakuwa mgeni mashuhuri
wa ZIFF. Mtengenezaji huyu wa filamu inayojulikana sana ya “Biggie and Tupac”
atakuja kufundisha akisaidiwa na watengeneza filamu wengine kama vile Donald
Ravaud (Constant Gardner).
Filamu mpya itakayoonyeshwa mwaka huu ZIFF ni ile inayohusu maisha ya makamu
wa rais Maalim Seif Sharif Hamad. Muasisi huyu wa amani na demokrasia hapa
nchini anazungumzia maisha yake tangu utoto hadi leo.
Wageni wengine watakaokuja ni Oliver Mutukudzi toka Zimbabwe, anayejulikana
kwa muziki wake wakuchezeka na kuliwaza. Filamu 6 zitaonyeshwa kwa mara ya
kwanza duniani pamoja na filamu Taka Takata toka Afrika Kusini na The Rugged
Priest toka Kenya. Filamu za Waaborijino wa Kiaustralia pia zitapewa umuhimu wa
juu katika tamasha mwaka huu, ambapo itatarajiwa kuwa watu wasiopungua 45,000 watapita Ngome Kongwe katika siku hizo 10 za tamasha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...