Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi, Omar Yussuf Mzee mara baada ya kuwasili Mkoa wa Kaskazini Unguja katika kikao cha majumuisho ya ziara yake Mkoani humo.Picha na Yussuf Simai,MAELEZO Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein amewataka Viongozi wa Mkoa Kaskazini Unguja kufichua vitendo vya ubakaji na udhalilishaji watoto katika Mkoa huo.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Kaskazini Unguja jana, Dk. Shein alisema kwamba amekuwa akipokea taarifa juu ya matukio ya ubakaji,lakini taarifa hizo hazitolewi na Viongozi wa Mkoa.
Rais Dk Shein amelaumu tabia ya Viongozi na Watendaji wa Mkoa kutokuwa wazi katika kueleza vitendo hivyo kwani katika mazungumzo yake wamekuwa wakigusia tatizo hilo,lakini alipotembelea katika Mkoa huo, hakuna taarifa yoyote rasmi.
“Nimekuwa nikipokea taarifa kutoka kwa wananchi wakilalamikia tabia ya ubakaji na udhalilishaji watoto…sasa nawaagiza Viongozi wa Mkoa kuchukua hatua za haraka kukomesha vitendo hivyo” Aliagiza Rais Dk. Shein.
Dk Shein alisema kushamiri kwa vitendo hivyo hakutoi taswira nzuri katika jamii, hivyo alitaka kuwepo kwa mpango mkakati katika kukomesha kabisa wimbi hilo akitaka pia wazazi na walezi nao kuchukua hatua madhubuti kusaidiana na Serikali kukomesha vitendo hivyo.
Akizungumzia utunzaji wa mazingira, Dk Shein amewakumbusha viongozi na Watendaji wengine katika Mkoa huo kuhakikisha kwamba wanafanya kila lililo katika uwezo wao kupambana na wachafuzi wa mazingira.
Rais Dk. Shein amesema Serikali itajitahidi kuona kwamba suala la mazingira linaendelea kupewa kipaumbele na hivyo, kuwahimiza wananchi kuhifadhi mazingira kwa muktadha wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumzia migogoro ya ardhi, Dk Shein alisema kwamba suala hilo linapaswa kushughulikiwa na Serikali ya Mkoa kwani mambo mengi yamekuwa yakifanywa na Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Rais Dk Shein amemaliza ziara yake katika Mkoa wa Kaskazini Unguja jana ambapo anatarajiwa kuanza ziara kama hizo katika Mikoa ya Kaskazini na Kusini Pemba wiki ijayo.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...