Na Pascal Mayalla.
Tanzania itafaidika na uzoefu wa nchi ya Uingereza katika fani ya utoaji wa mafunzo ya Ufundi Stadi kwa lengo la kuboresha viwango vya mafunzo yatolewayo na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi nchini, kufikia viwango vya kimataifa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Harrow, cha nchini Uingereza, Bw.Tony Medhurst, baada ya kumaliza ziara ya mafunzo nchini ambapo wakufunzi toka nchini Uingereza, wamebadilisha uzoefu na wakufunzi wa Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini (Veta) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Bw. Medhurst amesema Tanzania ina fursa nyingi za kujifunza kutoka nchini Uingereza, kwa chuo chake kutoa fursa kwa Walimu wa VETA kupatiwa ziara za mafunzo nchini Uingereza, na Walimu kutoka Chuo Kikuu cha Harrow kuja nchini kutoa mafunzo hivyo kuboresha mafunzo yatolewayo na VETA.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ufundi katika Veta, Bi. Leah Dotto, Lukindo, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za mamlaka katika kuboresha mafunzo kwa wanafunzi wa ufundi stadi wa vyuo vya VETA, hivyo kuboresha stadi hizo ili kuendana na wakati.
Bi. Lukindo amesema, walengwa wakuu wa ushirikiano huu na Uingereza, kwa kuanzia ni wanafunzi wa Chuo cha VETA cha Mikumi kinachotoa mafunzo ya huduma za utalii na hoteli.
Naye Mkufunzi wa Kozi za Utalii wa Chuo hicho cha Veta Mikumi, Godfrey Mnjeja, amekiri chuo chake kufaidika sana na mpango huo wa kubadilishana uzoefu kati yao na uingereza, na kusema, wafaidika wakuu ni Watanzania kwa ujumla wetu, maana wanafunzi wa VETA, ndio watekelezaji wa huduma hizi kwa watanzania wote.
Ziara hii, inafuatia ziara nyingine kama hii, iliofanywa na uongozi wa juu wa VETA, iliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Eng. Zebadiah Moshi, na wakufunzi wa Chuo cha VETA cha Mikumi, kutembelea Chuo Kikuu cha Harrow, mwezi Januari mwaka huu, ambapo waliridhishwa sana na maendeleo ya kiteknolojia ya utoaji mafunzo ya ufundi stadi waliyoyakuta.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...