Meneja wa Benki ya Exim tawi Iringa mjini , Thomas Beatus (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya Sh. Mil 3.5/- kwa Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa,Gervas Ndaki mwishoni mwa wiki kama mchango wa benki hiyo kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali za uzoaji taka katika manispaa hiyo.

Na Mwandishi Wetu, Iringa

BENKI ya Exim Tanzania imetoa sh mil 3.5/- kuchangia gharama za jumla za usafi katika kufanikisha kampeni za kimkoa za utunzaji mazingira.

Akizungumzia msaada huo mwishoni mwa wiki mkoani hapa Meneja wa Tawi la Benki hiyo, Thomas Beatus alisema benki hiyo inatambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira nchini na kwamba hilo ni moja kati ya majukumu yake.

“Pamoja na benki yetu kujihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii lakini suala la usafi na uhifadhi wa mazingira tumekuwa tukiliwekea mkazo wa kipekee katika kuunga mkono kampeni za serikali dhidi ya utunzaji wa mazingira nchini”, alisema Beatus.

Aliongeza kuwa msaada huo utatumika katika kugharamia huduma ya ukusanyaji taka ngumu utakaofanywa katika kipindi cha mwezi mmoja na ni imani yao kuwa baada ya kipindi hicho hali ya uchafu katika manispaa hiyo itakuwa imepungua kwa kiasi kikubwa.

Akisisitiza kuhusu hilo Beatus alitoa rai kwa wadau wengine wa maendeleo nchini kuchangia katika shughuli za usafi hususani katika manispaa zetu mbalimbali nchini ambazo zimekuwa na mzigo mkubwa usiolingana na uwezo wao kifedha.

“Tumeona ni vyema tukatoa kipaumbele katika jukumu la utunzaji wa mazingira kama tunavyotoa kipaumbele katika majukumu mengine ya kibenki katika shughuli zetu za kila siku kwani uhai wa mazingira ni uhai wa benki yetu pia”.

“Hivyo ni vyema kwa kampuni, taasisi na watu binafsi kujitokeza na kuunga mkono jitihada za serikali katika hili hususani katika kuzipunguzia mzigo manispaa zetu ambazo nyingi hazina makusanyo ya kutosha ya fedha”, alisema.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Manispaa hiyo Gervas Ndaki alisema msaada huo ni nguvu ya kutosha kwao na kwamba watahakikisha fedha hizo zinatumika katika malengo husika katika kuhamasisha wadau wengine kujitokeza kuchangia.

Alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi katika usafi na uhifadhi wa mazingira kwa jumla kutokana na uwezo mdogo wa kifedha hivyo msaada huo umewafikia katika wakati muafaka.

“Tunawashukuru Exim kwa kujitolea katika hili, nasi tunawaahidi kuwa fedha hizi zitatumika katika malengo husika na si vinginevyo,asanteni sana”, alisema Ndaki.

Benki ya Exim Tanzania inayojumuisha wanahisa Wazalendo ilianza kutoa huduma zake mwaka 1997 ikiwa na tawi moja Dar es Salaam katika mtaa wa Samora ambapo sasa imeweza kupiga hatua kubwa ikiwa na matawi kadhaa nchini na nje ya nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...