Gari la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) likiwa linazunguka nje ya Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Arusha kukanusha huwepo kwa Muafaka wa baraza la Madiwani Jimbo la Arusha Mjini.
Hali ilivyokuwa nje ya Lango la Manispaa ya Arusha yakiwa yamebandikwa mabango yaliyoandikwa na Madiwani wenyewe kushawishi wananchi kuwa muafaka umepatikana.
Na Ripota wa Globu ya Jamii,Arusha
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, jitihada za kuubariki Muafaka wenye utata uliofikiwa hivi karibuni Mjini Arusha baina ya Vyama vya CCM, TLP na Madiwani wa Chadema zimeshindikana baada ya kujitokeza watu wachache mno katika tukio hilo lililokuwa limepangwa kutokea leo katika Jengo la Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Katika tukio hilo, yalipangwa Maandamano ambayo yangeanzia Sombetini na kuishia katika Ofisi hiyo kwa kupokelewa na Diwani wa Gaudensi Lyimo ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwaeleza watu walioandamana kuwa Muafaka umefikiwa bila kujali itikadi hivyo wawaunge mkono wadiwani wao.
Hali ilianza kuvurugika asubuhi wakati gari la matangazo lililokuwa likitangaza kwa niaba ya Meya lililopokuwa linahimiza wakazi wa Arusha kukusanyika katika Ofisi za Halmashauri ya Jiji la Arusha ili kushuhudia muafaka huo kukumbana na vikwazo vya gari la Chadema lililokuwa likitangaza hakuna muafaka uliofikiwa na watu wasiende kushuhudia.
Hali hiyo ilipelekea baadhi ya wananchi ambao walikuwa wameanza kwenda katika eneo hilo kuahirisha na hata wale waliokuwa wamekodishiwa mabasi kutoka katika Kata ya Sokoni One inayoshikiliwa na Diwani Michael Kivuyo (TLP) na kata nyingine kushuka kwa nguvu katika mabasi hayo kwa madai kuwa lazima haki itendeke kwanza.
Hata hivyo Mgeni rasmi katika Sherehe hiyo Diwani Gaudensi Lyimo hakutokea kama ilivyokuwa imepangwa na badala yake hafla hiyo ambayo haikuzidi watu thelathini ilihutubiwa na Diwani wa Sombetini Alphonse Mawazo ambaye aliwaambia wajumbe hao waliletwa na basi moja kuwa kwa sababu MAALUM Meya hakuweza kufika katika hafla hiyo na anaongea kwa niaba yake na niaba ya Madiwani kuwa muafaka umepatikana na ni kwa faida ya wananchi hivyo waende wakahimize ushirikiano, hutuba yake haikuzidi dakika tano.
Habari kutoka ndani ya Manispaa hiyo zinasema wakati hutuba hiyo ikitolewa kwa niaba ya Diwani Lyimo, Madiwani wengine waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo ambao baadhi yao waliingizwa katika eneo la Manispaa kwa Ulinzi wa Jeshi la Polisi wakiwemo Madiwani wa Chadema walikuwa wamejifungia katika baadhi ya Ofisi za Manispaa hiyo kwa kuhofia usalama wao baada ya kupata taarifa kuwa vurugu zinaweza kutokea kufuatia kauli za magari ya matangazo katika Kata zao.
Mmoja ya watu waliohudhuria hafla hiyo kutoka katika Kata ya Sokoni One ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema amesikitishwa na mipango mibovu ya tukio hilo na anamlaumu sana Diwani wake na viongozi wote wa Chama na Serekali waliohusika kuandaa tukio hilo kwa kumlaghai kuwa Muafaka umepatikana hali ambayo ni kinyume na mazingira aliyoyakuta katika Jengo la Manispaa.
Amesema licha ya kusikitishwa na Mipango hiyo mibovu ameshangazwa ni kwa nini Meya aliyewaita hapo hakujitokeza hata kama walikuwa wachache angalau awapongeze kwa moyo wao wa upendo waliouonyesha, Mwananchi huyo amesema binafsi hafurahishwi na mgogoro huo na anakilaumu kitendo cha Kiongozi aliyehutubia hafla hiyo kunuka harufu kali ya Pombe aina ya Konyagi nyakati za asubuhi.
Jitihada za kumpata Diwani wa Sombetini Alphonse Mawazo kumuuliza juu ya malalamiko kuwa alihutubia akiwa ananuka harufu kali ya Konyagi hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya Mkononi kuwa imezimwa, hata hivyo Jitihada za kuwapata kwa simu Diwani Lyimo (CCM - Meya) na Diwai Mallah (Chadema - Naibu Meya) kuwauliza wamepatwa na nini na kushindwa kuhudhuria hafla hiyo ingawa walikuwepo katika Jengo la Halmashauri ya Jiji la Arusha pia hazikuzaa matunda kufuatia simu zao za Mkononi kuzimwa.
Hivi karibuni kulizuka utata mkubwa kufuatia muafaka wenye mashaka baina ya Madiwani wa CCM, Chadema na TLP uliolenga kumaliza Mgogoro wa Umeya katika Jimbo la Arusha. Muafaka huo umekuwa ukipingwa na viongozi waandamizi wa Chama cha Chadema akiwemo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema kufuatia mgogoro mkubwa wa Kikanuni katika uchaguzi uliomuweka madarakani Meya wa Arusha aliyepo sasa Diwani Gaudensi Lyimo hali iliyosababisha pia mauaji yaliyofanywa na Polisi ya raia watatu mmoja akiwa ni raia kutoka Kenya januari 5 mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...