Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar,
Mh. Hamad Masoud Hamad
NA FAKI MJAKA - MAELEZO ZANZIBAR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa ujenzi wa Gati mpya huko Mpigaduri tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na Wachina na hivi sasa kinachosubiriwa kwa Wachina hao ni kutafuta fedha kutoka Benki yao ya Exim kwa ajili ya ujenzi huo.

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Hamad Masoud Hamad wakati alipokuwa akijibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia hoja ya Wizara yake.

Amesema kuwa Ujenzi wa Gati hiyo ulifanyiwa upembuzi lakini haukutosheleza lakini ikalazimika kufanyiwa upembuzi tena na hivi sasa umeshakamilika na fedha zimo mbioni kutafutwa na wachina ambao ndio waliofanya kazi hiyo.

Akizungumzia juu ya Mwekezaji Mzalendo Said Salum Bakhresa kunyimwa ujenzi wa sehemu ya abiria amesema kuwa Mwekezaji huyo sehemu hiyo alitaka kutumika kwa vyombo vyake tu na abiria wa vyombo vingine wasiweze kutumia jengo hilo.

Waziri Masoud amesema kuwa kwa hali ya Zanzibar jambo hilo halitowezekana kwa kuwanyima abiria wengine kutotumia jengo hilo kwani siyo busara wala haielekei kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema kuwa hivi sasa Wizara yake imeshawasiliana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) juu ya ujengaji wa eneo la kupumzikia abiria ambayo gharama yake inakadiriwa kuwa ni sh. Millioni 300.

Waziri alisema kuwa Fedha hizo siyo nyingi hata wao wakifanya mpango mzuri wa kutafuta fedha wanaweza kulijenga jengo hilo la abiria na abiria wa meli zote watafaidika bila ya kuwabagua abiria wetu.

Kuhusu ununuzi wa Meli mpya Waziri huyo wa Miundo mbinu amesema shirika la Meli Zanzibar litaweza kununua meli hiyo kwa njia ya ubia na tayari kampuni tatu zimeshajitokeza na ile watakayokubaliana nayo ndiyo itakayoshirikiana Serikali.

Akizungumzia juu ya hofu ya kampuni ya ZAT inayoshughulikia na upakuzi wa mizigo na shughuli nyingine za uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar amesema kampuni hiyo haitoondolewa isipokuwa itakuwa na ushindani wa kampuni nyingine zitazofuata ili kuwepo kwa ufanisi mzuri wa utendaji kazi katika uwanja huo.

Baraza la Wawakilishi hatimaye limepitisha Bajeti ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ya shs 13645,598,000/- kwa mwaka wa fedha 2011/2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 14, 2011

    nielimisheni wadau wenzangu hapa kidogo nimeshindwa elewa. Utafiti wamefanya wachina, pesa watatoa wachina, watajenga wachina, gati itakuwa mali ya nani? Jee haya si ndio yale yale tuliyoyaona katika ile clip chinese are coming?

    mzalendo

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 14, 2011

    michuzi tunaomba hela zikiwa nyingi kama hivi utuandikie kwa maeno maana tunashindwa kuzijua kiasi gani,halafu hivi Tanzania bara au Tanzania hatumiliki meli badala ya MV MAPINDUZI NA MV MAENDELEO SERIKALI HAINA MELI HEBU TUELIMISHWE AU BANDARI IMEBINAFSISHWA?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...