Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Stephen Nkondikaya akimuwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt Terezya Hufisa (hayupo pichani),katika mkutano na Waandishi wa Habari leo katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozone ambayo huadhimishwa kila mwaka September 16,kulia ni Afisa Mazingira Mkuu Bw. Salia Mangalili, Mwaka huu maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika mkoani Arusha.(Picha na Evelyn Mkokoi wa Ofisi ya Makamu wa Rais)

Na. Aron Msigwa –MAELEZO.

Watanzania wametakiwa kununua bidhaa zenye nembo ya rafiki wa tabaka la hewa ya Ozoni (Ozone friendly) ili kuungana na mataifa mbalimbali duniani kuhifadhi tabaka la hewa hiyo ambalo liko hatarini kutoweka angani kutokana na uchafuzi wa mazingira unaoendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuelezea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni yatakayofanyika kitaifa mwezi huu jijini Arusha, kaimu mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Stephen Nkondokaya amesema kuwa Tanzania licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali inaendelea kupunguza ongezeko la matumizi ya vifaa vinavyotoa hewa zinazoharibu tabaka la Ozoni angani .

Amesema hali iliyoanza kujitokeza ya kuruhusu kiasi kikubwa cha mionzi ya kikiukaurujuani kufika kwenye uso wa dunia inasabishwa na matumizi ya kemikali hatari zikiwemo “Chlorofluorocarbons”,Halons na Carbon tetrachlorides zinazotumika katika sehemu mbalimbali zikiwemo kwenye majokofu, viyoyozi , vifaa vya kuzimia moto, shughuli za usafishaji chuma, utengenezaji wa magodoro, kilimo cha tumbaku na maua pamoja na zile za kuhifadhia nafaka katika maghala zimekuwa chanzo cha uharibifu wa tabaka la Ozoni.

Bw. Nkondokaya amefafanua kuwa hali ya kuongezeka kwa magonjwa ya kansa ya ngozi , uharibifu wa macho unaosababisha upofu, upungufu wa kujikinga na maradhi na kujikunja kwa ngozi kuathirika kwa maumbile na michakato ya ukuaji kunasababishwa na ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabia nchi.

Ameeleza kuwa Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi 196 zilizoridhia mkataba wa kimataifa wa Vienna na Itifaki ya Montreal mwaka 1993 inaendelea kuweka mfumo wa udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya Ozoni ikiwemo kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi hizo kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwisha tumika na vinavyotumia vipoozi aina ya R 11 na R 12,kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani na vifaa vya kuzimia moto zinazoharibu tabaka la Ozoni aina ya CFCs na halon.

Kuhusu maadhimisho ya Kimataifa ya Tabaka la Ozoni ambayo kitaifa yatakayofanyika jijini Arusha amesema yataongozwa na kauli mbiu ya “Uondoshaji wa Matumizi ya gesi za “Hydrochrolofluorocarbons” (HCFC): Mchango muhimu katika kulinda Tabaka la Ozoni na kuzuia Mabadiliko ya Tabianchi” na kuambatana na zoezi la utoaji elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda tabaka la Ozoni pamoja na kugawa mitambo ya kutambua gesi zinazoharibu tabaka la hewa ya Ozoni kwa wadau wa usimamizi wa sheria ya mazingira nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...