Spika wa Bunge la Tanzania
Mh. Anne Makinda
Na Mwandishi Wetu

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda amekubali ombi la kuwa mgeni rasmi wa sherehe za miaka 100 za shule kongwe ya Sekondari ya Wasichana ya Ndwika iliyopo Lulindi, Masasi mkoani Mtwara.

Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa shule hiyo ya bweni, Aluna Bakari alipokuwa anazungumzia maandalizi ya sherehe hizo zinazotarajiwa kufanyika Jumanne ya Oktoba 25 mwaka huu.

“Tunamshukuru sana Spika Mama Anne Makinda amekubali kuwa mgeni rasmi katika sherehe zetu za kihistoria zinakazokwenda sambamba na harambee ya kukamilisha miradi kadhaa kwa ajili ya ustawi wa elimu shuleni na jamii inayotuzunguka,” alisema Bakari aliyezungumza kwa njia ya simu jana kutoka Lulindi.

Alisema kwamba, uongozi wa shule hiyo ambayo kwa sasa ina wanafunzi 360 una kila sababu za kuadhimisha miaka 100 ya shule hiyo kutokana na mchango mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii, hasa kwa watoto wa kike.

“Hiki si kitu kidogo. Tuna kila sababu za kuwaenzi waasisi wa shule, ndiyo maana tumeandaa sherehe hizi. Miaka 100 ya kumpa elimu mtoto wa kike si mzaha, lazima tujipongeze na kuweka mikakati zaidi ya kuwakomboa wanawake kielimu,” alisema huku akimpongeza Spika Makinda ambaye kati ya mwaka 1965 na 1968 alipata elimu ya Sekondari katika shule ya Wasichana Masasi.

Pamoja na ugeni mzito wa Spika Makinda, mkuu huyo wa shule amewataka wadau, wakiwamo watu waliowahi kusoma, kufanya kazi au kuwa karibu na taasisi hiyo na wakereketwa wa maendeleo ya elimu nchini kujitokeza kwa hali na mali kusaidia kufanikisha sherehe hiyo ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa kituo cha maarifa shuleni hapo.

Mbali ya fedha, aliitaja michango mingine inayokaribishwa kutoka kwa wadau mbalimbali kuwa ni pamoja na saruji, mabati na hata ushauri.

“Tunawaomba waliosoma, kufanya kazi au kuwa sehemu ya Ndwika kwa namna moja ama nyingine kuungana nasi kwa hali na mali katika shughuli yetu ya kihistoria. Umbali si tatizo, tuna akaunti ya maendeleo ya shule yenye namba 705 120 0111 katika Benki ya NMB tawi la Masasi,” alisema Mwalimu Bakari.

Mkuu wa shule hiyo iliyopo katika Jimbo la zamani la Anna Abdallah, ambalo kwa sasa linaongozwa na Jerome Bwanausi aliongeza kwamba, wakati shule ikiwa katika joto la sherehe hizo, shule yake pia inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa pamoja na uhaba wa walimu, uchakavu wa majengo na pia uchakavu wa miundombinu ya maji na umeme.

Sekondari ya Ndwika ilianzishwa na Kanisa la Anglikana kupitia shirika lake la UMCA na ilikabidhiwa kwa serikali mwaka 1970, ikiwa chini ya mkuu wa kwanza wa shule mzalendo, Magdalena Sonje. Ilipoanzishwa ilikuwa chini ya Janeth Dalton, raia wa Uingereza.

Miongoni mwa waliosoma katika shule hiyo ni Thecla Mchauru, mmoja wa wauguzi na walimu wa kwanza wa kike nchini ambaye baadaye alishika nyadhifa kadhaa katika chama na serikali, akiwa pia mmoja wa watu waliokuwa washauri wa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mbunge wa sasa wa Masasi, Mariam Kasembe pia alisoma shuleni hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...