Ndugu zangu,

Kwa mujibu wa ratiba za Bunge Ijumaa ya leo ndio kimsingi itaamua mwelekeo wetu kama taifa. Kwamba ni njia ipi Wabunge wetu na hususan wa Chama Cha Mapinduzi wanataka kutupitisha WaTanzania katika jitihada zetu za kuandika Katiba Mpya kwa Tanzania ya sasa na ijayo. Na kuna njia mbili. Mtaziona kupitia maandiko haya.

Yumkini nchi yetu haina ukame wa nyimbo za muziki, lakini, nchi haiwezi kustawi kwa nyimbo tu. Ama, nchi haiwezi kuendelea kwa kauli za mipasho, bali, kauli kutoka kwa raia wenye hekima na busara. Na nchi yetu haijaishiwa raia wenye hekima na busara wakiwamo viongozi, walio kwenye utumishi na wastaafu.

Hakika, nchi yetu inapita sasa kwenye kipindi kigumu katika historia yetu. Huu ni wakati wa kuitanguliza busara na hekima. Na katika hili la Katiba wabunge wetu wasihangaike kuyauliza maswali haya; ” Katiba hii mpya itaunusuru ubunge, U-DC na U-RC wangu? Katiba hii mpya itamnusuru mgombea wangu urais ajaye? Katiba hii mpya itakinusuru chama changu?

Bali, wabunge wetu wajiulize; ” Katiba hii mpya itainusuru Tanzania yangu, leo, kesho na keshokutwa? Hivyo basi, swali kuu ni hili; ” Katiba Mpya italinda na kutetea maslahi ya kudumu ya nchi yangu?

Maana, tulimsikia Profesa Haule akitamka kwenye semina ya wabunge, kuwa: ” Kuna wabunge wameniuliza mchakato huu wa Katiba ukianza ina maana wataacha kuwa wabunge?”

Swali lile la wabunge walilomwuliza Profesa Haule lina tafsiri ya hulka ya ubinafsi. Na hapa kuna tatizo kubwa. Kuwa kuna hatari ya mjadala muhimu wa Katiba kutawaliwa na ubinafsi na unafiki uliochanganyika na hofu.

Kuna wabunge wanaosema wasichokiamini, lakini, wanasema kwa kutetea ulaji wao . Wanasema wakidhani wanamfurahisha aliyewapa ulaji wao, au chama kilichowapa ulaji huo. Inasikitisha, kuwa leo tuna hata wasomi wenye kuweka taaluma zao mifukoni na kufanya kazi ya ’ kuganga njaa’ . Nao wanasema wasiyoyaamini. Hawa wote ni watu wenye kutishia maslahi ya nchi yetu. Wenye uwezo wa kuchangia kutufikisha pabaya kama taifa, kwa ubinafsi na unafiki wao uliochanganyika na hofu.


Ndio, Ijumaa ya leo itakuwa ni ama ya tumaini kwa Watanzania au huzuni na hali ya kukata tamaa. Huzuni kwa WaTanzania wengi ni pale , Wabunge, walio wengi wa CCM, wataamua kuupitisha muswaada wa kuanzisha mchakato wa Katiba ulio mbele yao licha ya kilio cha wengi nje ya bunge kutaka uwepo muda zaidi wa kutafakari, kuelewa na hatimaye kujadiliana na kupata muafaka wa kiraifa wa namna bora ya kuanzisha mchakato huo. 

Furaha na matumaini ya WaTanzania yatakuwepo pale Wabunge hao na Serikali watakapotanguliza busara na kupendekeza kuahirisha zoezi hilo. Wajipe muda wa kujipanga upya na hivyo basi, kuwapa muda WaTanzania kuja na mapendekezo yao. Maana, Katiba hiyo inayotakiwa kuandikwa ni ya Wananchi.

Na wabunge wa CCM wakiupitisha, basi, tumaini la mwisho kwa WaTanzania litabaki kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yeye ndiye mwenye ’ Kura ya Veto’. Ana uwezo wa kuamua kusaini au kutosaini muswaada huo.

Na tangu mwanzoni, njia iliyotufikisha Ijumaa ya leo ilitutia shaka wengi wetu. Majuzi hapa niliangalia kipindi cha TBC1 kuhusu semina ya Wabunge juu ya mchakato wa Katiba. Nikiri, mara kipindi kile kilipomalizika, nami nilitingisha kichwa kwa masikitiko. Niliziona ishara za njia mbaya tunayokwenda kupitishwa. 

Kwa mtazamo wangu, Maprofesa waendesha semina wale wawili; Profesa Palamagamba Kabudi na mwenzake Haule walionekana zaidi kwa sura ya ‘ ukada’ kuliko utaaluma na uanazuoni , hivyo basi, kuthibitisha kauli ya Profesa Shivji anayesema mchakato huu wa Katiba umekosa uhalali na kuonyesha wazi hofu yake ya Rais kupewa mamlaka makubwa.

Mbunge David Kafulila ( NCCR- Mageuzi) naye alisema kile ambacho ndicho kitakachofanya mchakato huu uwe wa gharama kubwa bila matunda tarajiwa kwa umma. Kafulila amezungumzia juu ya IMANI ya umma kwa mchakato mzima akimrejea Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki- Moon aliyesema , kuwa tatizo kubwa la Serikali nyingi si nakisi ya bajeti bali nakisi ya imani ya Wananchi kwa Serikali hizo. Ndio, kupungua kwa imani.

Ndio, inahusu imani na ni wajibu wa Serikali na Chama cha Mapinduzi kuirudisha imani ya wananchi kwa Serikali na chama hicho. Maana, ilivyo sasa inaonyesha wananchi wana mgogoro na Serikali yao inayoongozwa na CCM. Na kwa hali ilivyo sasa hapa nchini, hata kama Chadema ikifutwa kesho, bado, kikitokea chama kinachoongozwa na manyani na manyani hao wakaongea yale wanayoongea Chadema kwa WaTanzania ikiwamo hili la Katiba, basi, chama hicho cha manyani kitapata wafuasi na kitajaza watu kwenye mikutano yake.

Tuwe wakweli kwa nchi yetu. Nionavyo, Sheria ya kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya unaojadiliwa na pengine kupitishwa na wabunge walio wengi wa chama tawala Ijumaa ya leo kamwe haiwezi kutuacha salama kama taifa. Na hapa wabunge wa CCM wasipoteze muda kuitazama Chadema kama mchawi. Zitafutwe njia za CCM na Chadema kukaa meza moja na kuutafuta muafaka. Nchi ibaki na utulivu na twende mbele kama taifa moja. Hata kama hatuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini, tuanze sasa kujenga Fikra za Umoja wa Kitaifa.

Na hofu ya mchakato wa Katiba wenye walakini imeelezwa pia na Chama Cha Wanasheria wa Tanzania bara katika taarifa yao ya siku moja tu kabla mjadala huo kuanza bungeni. Wanazuoni wetu hawa wa sheria waliweka wazi, kuwa si sahihi kwa muswaada huo kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu. Unawanyima wananchi wengi fursa ya kushiriki kuujadili. Wanazuoni wetu wanasema kinachotakiwa kutungiwa sheria ni Mchakato wa Maandalizi. Na kwa DHATI kabisa, walisema, hata kama Wabunge watapitisha muswaada huu wa mchakato, basi, wamemshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano asiusaini muswaada huo.

Na kwenye kipindi kile cha TBC1 Profesa Kabudi alisema; ” Katiba si Muharobaini”. Wengine sisi hata kama hatuna shahada za udaktari wa falsafa lakini tunauona ukweli pia, kuwa tunachohitaji ni mzizi wa muharobaini. Kwamba yumkini Katiba kwetu yaweza kuwa mzizi wa muharobaini. 

Profesa Kabudi anasema pia, ” What we are doing is Constutional building and not Constutional making”. Kwamba tunachokifanya ni Ujenzi wa Katiba na si Kutengeneza Katiba. 

Swali kwa anachokisema Profesa ni je; “ Ni kina nani wanaostahili kushirikishwa kwenye maandalizi ya ujenzi huo?”. Ndipo hapa hoja ya Profesa Shivji inapokuwa na mashiko pale anaposema huenda mchakato mzima umekosa uhalali.

Ndio, kinachojionyesha ni hiki; tunajenga nyumba moja lakini tunagombania fito. Na kibaya zaidi, tumefikia mahali pa kuchagua nani wa kuchangia fito kwenye ujenzi wa nyumba yetu. Hivyo basi, kubagua. Ni dhambi kubwa.

Na muswaada huu ukipitishwa utakuwa na maana hii; kumruhusu Rais kuanzisha mchakato kwa kuwateua wajumbe wa Kamati itakayoratibu mchakato , kuwateua wabunge 116 wa Bunge la Katiba. Wabunge hao wakiletewa mapendekezo ya Katiba Mpya wataijadili na hatimaye kuipitisha au la. Wakiipitisha itapelekwa kwa wananchi kupigiwa kura. Na kura za ndiyo zikitosha itakuwa na maana ya Katiba hiyo mpya kupata uhalali na kuanza kutumika. 

Na tafsiri kuu hapa ni hii; Watanzania tutakuwa tumepewa Katiba Mpya tunayoililia ndani ya juma moja. Na lifuatalo nina hakika nalo, kuwa Watanzania HATUTARIDHIKA nayo. Kwanini? 

Nilipata kuandika kupitia safu yangu kwenye Raia Mwema, kuwa; ” Nauona, mwelekeo mbaya wa upepo wa kisiasa nchini mwetu. Nina shaka kubwa. Naamini, tuko wengi wenye mashaka na mwelekeo wa nchi yetu tunayoipenda.” ( Mraba Wa Maggid, Raia Mwema, Aprili 6, 2011 )


Kwenye makala yangu ile niliweka wazi, kuwa katika hili la mchakato wa kupata Katiba Mpya tumeanza na mguu mbaya. Tumeyaona Dodoma na Dar es Salaam . Sikuhitaji kuwa na Elimu ya Unajimu kubaini hilo. Tulishaziona ishara.

Hakika, ikitaka, Serikali inaweza kurudi nyuma na kuanza upya. Wahenga walitwambia, ni heri nusu shari kuliko shari kamili. Katiba ni ya Watanzania, kwanini usiwepo ’ Mchakato Kivuli’- Shadow process utakayojumuisha makundi mbali mbali ya kijamii. Wajadili kwa uhuru kabisa, yote. Kisha nao waje na mapendekezo yao. Ingeepusha shari kamili.

Haiyumkini suala nyeti kama la Muswaada wa Mapendekezo ya Sheria itakayosimamia mchakato wa Katiba likajadiliwa na wadau kwa siku tatu tu. Ndio, chini ya saa 100. Maana, Katiba ya nchi ni kitabu nyeti chenye kuhusu maisha ya kila siku ya Mtanzania. Hauingii akilini, utaratibu wa wadau kujadili Muswaada huu kwenye kumbi za Msekwa Dodoma na Karimjee Dar. Halafu ikawa basi, imetosha. Urudishwe kwa Wabunge, waujadili, kisha waupigie kura, na zaidi kuupitisha.

Watanzania tuko zaidi ya milioni 42. Ni vema na ni busara kukawepo na wigo mpana zaidi wa kuwafikia Watanzania wengi zaidi kadri inavyowezekana. Hivi, inatoka wapi, ’ghafla’ na ’dharura’ hii ya wadau kutakiwa kutoa maoni yao ndani ya saa 72? Maana, hili ni suala nyeti kwa Watanzania na lenye kuhusu mustakabali wa nchi. Kwa nini tusipewe muda zaidi wa kutafakari?

Na wahusika wana nafasi ya kujisahihisha na kuokoa sura zao. Maana, tukubali, kuwa mchakato unaoendelea hautasaidia kupata Katiba itakayowapa imani Watanzania kuwa italinda maslahi ya taifa lao na yenye kukidhi matakwa ya wakati tulionao. Hayo ni mashaka ya kweli ya Watanzania walio wengi, yasipuuzwe. Na Watanzania wanajua, kuwa wanachokitafuta sasa walikuwa nacho, walikipoteza, kwa bahati mbaya. 


Na kuna kisa kutoka Uganda. Milton Obote, mbali ya mambo mengine, anakumbukwa na Waganda kwa tukio la kihistoria la ’ Kuchakachua’ Katiba ya nchi hiyo kwa kuifanyia mabadiliko kinyemela. Ilikuwa Aprili 15, 1966. Ilikuwa aubuhi moja. Wabunge wa Uganda, kabla ya kikao, walielekezwa kwenye masanduku yao ya makabrasha bungeni wakachukue ’ Muswaada wa dharura’ wa Marekebisho ya Katiba. 

Muswaada ule wa Marekebisho ya Katiba ukajadiliwa ’ kishabiki’ na kupitishwa ndani ya saa moja. Unakumbukwa kwa jina maarufu la ’ Pigeon-hole’ Constitution- Katiba ya Sanduku la Makabrasha. Ni kitendo kile cha Obote, ndicho kilichopelekea Uganda kupitia wakati mgumu kwa miaka miaka mingi zaidi baadae.

Obote alikuwa na ugomvi na chama cha KY- Kabaka Yekka. Hivyo basi, alikuwa na ugomvi na Mfalme Fredrick Kabaka na WaBaganda. Katiba mpya ikampa nguvu nyingi Obote na UPC yake- Chama chake. Kabaka na WaBaganda walimtambua haswa Obote. Aliwanyanyasa kwa kuwafunga na hata kuwaua. Ndio, aliwanyamazisha, kwa muda. 

Lakini naye, Obote, hakubaki salama. Idi Amin akaja akampindua na kushangiliwa sana na WaBaganda wa Kampala na kwengineko. Kosa alilofanya Obote ni hili; kubadilisha Katiba kukidhi mahitaji yake na ya Chama chake katika wakati uliokuwepo. Obote hakuiangalia Uganda ya miaka 50 hadi 100 iliyofuata. Na hilo ndilo tatizo la viongozi wetu wengi Afrika.

Tukirudi hapa kwetu, haitarajiwi Wabunge wa CCM walio wengi kuukwamisha Muswaada huo unaojadiliwa sasa bungeni. Na ikitokea wakafanya hivyo, kwa maana ya Wabunge hao wa CCM wakaukwamisha Muswaada huo wa sheria, basi, Wabunge hao wa CCM watakuwa wameanza kazi ya kweli ya ’ Chama kujivua magamba’ na baadhi yao kunusurika na adhabu ya wapiga kura ifikapo 2015.

Nchi yetu iko njia panda. Mbele yetu kuna njia mbili; moja inaelekea tunakopita sasa. Kwenye hali ya ’ kujifunga’ na kubaki tulipo bila kupiga hatua za haraka za maendeleo huku baadhi, wakiwamo viongozi, wakiwa na udhibiti mkubwa wa hali ya mambo. Njia nyingine inaelekea kwenye uhuru zaidi wa wananchi na uwezo wa kuwadhibiti na kuwawajibisha viongozi wao. Ni njia inayoelekea kwenye ustawi wa nchi. 

Watanzania wengi kwa sasa wana kiu kubwa ya kuianza safari ya kuipita njia ya pili. Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa. Njia itakayotufanya tuondokane kabisa na njia ya kwanza, njia inayotufunga na kutubakisha hapa tulipo. Kwa viongozi watakaochangia kutupitisha kwenye njia ya kwanza, nahofia, kuwa hao watakumbukwa kwa dhamira yao hiyo mbaya kwa Watanzania.

Kwa wale viongozi watakaochangia katika kutupitisha kwenye njia ya pili, basi, hao hawatasahaulika mioyoni mwa Watanzania. Watakuwa ni wanadamu walioamua kuachana na ubinafsi na kutanguliza maslahi ya taifa. Ni imani yetu, kuwa hata Wabunge wengi wa CCM wanaweza kuingia katika kundi la viongozi hao. Kutupitisha kwenye njia ya pili.

Na kama Bunge letu litabariki azma ya Serikali kuendelea kutupitisha katika njia hii ya kwanza kwenye mchakato huu wa Katiba, basi, ni dhahiri, kuwa tuendako kuna giza zaidi kulipo hapa tulipoanzia. Kuna watakaoikumbuka Katiba yetu ya sasa. 

Na hiki ni kipindi kigumu sana Nchi yetu inakipitia tangu tupate Uhuru wetu. 
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Maggid Mjengwa,
Iringa
Ijumaa, Novemba 18, 2011

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. Mustakabali wa taifa ni muhimu zaidi kuliko mustakabali wa CCM maana CCM inaweza ikafa kesho kutwa lkn KATIBA ni itabaki milele. Mimi ninachoshangaa, CCM inaharakisha muswada kwa nini? Wanakimbilia wapi? Kuna nini ndani ya muswada ambacho wananchi hutupaswi kujua? Katiba ni kwa maslahi ya taifa na sio chama, sasa haraka za nini? Mimi nilitegemea kwa kipindi hiki ambapo watu karibu wote wanajua kusoma na kuandika, ingekuwa ndio wakati muafaka wa wananchi kuanza kushirikishwa kuanzia kwenye hatua za awali kabisa za maandalizi ya Katiba yao ili waijue lakini CCM imeamua kwa mara nyingine kukimbiza muswada huku wananchi walio wengi wakiwa hawajui kilichoandikwa ndani yake. Ieleweke wazi kuwa Muswada ukiwa mbaya hata Katiba yenyewe haiwezi kuwa nzuri maana uimara wa nyumba ni msingi.

    Hii haiwezi kuwa Katiba ya nchi bali ya CCM kwa sababu utaratibu unaotumika ni sawa na ule wanaotumia CCM kuandika Katiba yao. Watanzania tuwe makini kwa vitu makini, tusifanye utani na vitu muhimu kama Katiba. Sisi tunaofanya madudu sasa hivi, ni madudu hayo hayo tunawaachia watoto na wajukuu wetu. Sisi tutapita Katiba itabaki.ANNOYED!

    ReplyDelete
  2. Asante sana Mjengwa. Huwa nafarijika sana na makala zako kwani zinagsa ukweli.

    Nakushauri uhakikishe makala hii inawafikia wabunge wote, mawaziri, Spika, na Raisi hata kama mjadala utakuwa umeshapitishwa. Pia ichapishe kwenye magazeti yote. Ni elimu nzuri sana umeitoa.

    Wenye kuona mbali tunakubaliana na wewe lakini wenye ufinyu wa kuelewa ambao wametawaliwa na ubinafsi (wa kidini, kikabila, kimkoa n.k.)watakuponda.

    ReplyDelete
  3. Aise..mimi siyo mtalaam wa masuala ya Katiba lakini haya makala yamenitoa tongotongo kidogo..Waandishi wa habari wengi hamkutumia kalamu zenu kutuelimisha kuhusu haya masuala ya katiba.Too late.Asante Mjengwa

    David V

    ReplyDelete
  4. KATIBA NI YA WATANZANIA NA INATUBIDI KUWA MAKINI KWA FAIDA YA WATANZANIA,KUNA VIBARAKA WANAOSHABIKIA BILA KUJUA MADHARA YAKE,KUNA VYAMA VINAVYO FAZILIWA NA MABEBERU VIKO TAYARI PUNDA AFE MZIGO UFIKE.WAZIRI WA MAMBO YA NJE UNAPASWA KUTOA TAMKO KUHUSU HAO MABALOZI WA NJE WAMEFUATA NINI DODOMA KATIBA NI YETU WAO KINA WAWASHA NINI,IKUMBUKWE TUNAINGIA MIAKA 50 YA UHURU WETU MARA BAADA YA UHURU MWALIMU ALITUAMBIA TANZANIA HAITAKUA HURU KAMA AFRIKA NZIMA HAIKO HURU,TUKAPAMBANA NA HAOHAO WALIOKUJA DODOMA UPANDE WA MADUI ZETU HAWAKUTAKA AFRIKA NZIMA IWE HURU.HAWA WATU WAMEWEKA VIKWAZO VYA UCHUMI NCHINI CUBA KWA FAIDA YAO NA WANAOTESEKA NI WANANCHI WA CUBA NA SIO FIDEL CASTRO,EMBU TUJIULIZE HAWA MABEBERU WANATUPENDEA NINI WANANCHI WA TANZANIA MPAKA LEO WAINGILIE MIPANGILIO YA KATIBA YETU,JUZI TU BALOZI WA MEREKANI NCHINI SYRIA ALIKUWA UPANDE WA WANDAMANAJI NA KUHAMASISHA UNREST YA TAIFA LA SYRIA LEO WANDAMAJI WANA SILAHA NZITO ZINAENDELEA KUPENYEZWA KUPITIA LEBANON.MPANGO WAO NA HASA HAWA CONSERVTIVE UK NI REGIME CHANGE,TUWE MACHO NA UKOLONI MAMBO LEO ALUTA CONTINUA.

    ReplyDelete
  5. naomba nikuulize swali kaka mjengwa maana mimi sijaelewa ni muswada wa kutunga katiba mpya au ni muswada wa kujadili kuundwa kwa katiba mpya?ukisema kila mtu atimize wajibu wake basi kweli tutimize wajibu wetu,waandishi mtakumbukwa kwa habari zenu za uongo na upendeleo na uchochozi,kuwenu wakweli tuambieni ukweli sio siasa na kila mtu sasa kujifanya mwanaharakati,since when mmeanza harakati?mbona kama mna uchungu hatukuwaona kipindi cha hayati mwalimu?unafikina kutaka umaarafu kutawaponza,kuweni wakweli na wa wazi.kuna watu wanataka umaarufu kwa vurugu na vitisho sio wanasiasa.mjengwa tupe picha kamili sio lawama na kumbuka katiba sio suluhisho la matatizo ya watanzania bali ni suluhisho la wanasiasa kuingia ikulu.hili lipo wazi.acheni majungu kuweni wa kweli na sio kila mshika pen na karatasi ni mwanasiasa au mwandishi nguli

    ReplyDelete
  6. Maggid Mjengwa, mimi ni mtanzania aishiye nje manenoyako uiyoandika yamenigusa muno. Hongera kwa uzalendo. Baathi ya wabunge wetu Mungu atuokoe na janga la Katiba isiyotupa matumaini.

    ReplyDelete
  7. Mjengwa sema kaka, na wenye kulamba sumu na wailambe. Anony mmoja hapa ana jazba za kijinga kakuuliza au kakuhusisha na enzi za Mwalimu? Hawezi hata kufikiri na kupambanua kuwa enzi za Mwalimu kwa umli wako inawezekana ulikuwa bado shuleni? Ama kweli kazi, mtu kama huyu kesho utamkuta ni mbunge anaesimamia mjadala wa kulekebisha katiba. Jamani!

    ReplyDelete
  8. Nakubaliana na Anonymous hapo juu wa Nov 18,03:00.
    Makala ni ndeeefu.
    Naomba kwa uchache unielezee mimi na umma wa michuziblog nini hasa matatizo ya muswada huu wa mchakato wa mabadiliko ya katiba!
    Naomba vilevile unieleze unalidefine vipi Bunge kwa itikadi (huku nawe ukitaja itikadi,ubaguzi unaanza kwa kutamka)
    Bunge ni chombo kinachoundwa kwa mujibu wa katiba na kinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa katiba(despite kwamba kimeundwa na wabunge wanaotokana na vyama)
    Ninachoona nchi inazidi kuwa "lawless" na kila mtu anaandika pages of porojo bila mashiko ya kisheria.
    Mimi sio mbunge,lakini katiba na sheria zinanitaka niheshimu Bunge na Rais.
    Na katiba na sheria zinaeleza wazi taasisi hizi zinafanya kazi zake kwa mujibu wa katiba na sheria. Na kama kuna taasisi inaenda kinyume,mahakama zipo(na hapa atatokea mtu atatusi mahakama bila hata kujua kisheria ni contempt of court).
    Kichekesho ni wale waliojiteua kuwa washauri wa Rais eti assign.Guys let's be serious,Kenya iliendelea bila hata katiba ya sasa,let's work in our Attitude and aggressiveness.
    Nakubaliana na Prof.Kabudi,katiba sio muarobaini,what have u done to yourself and your society kwa katiba ya sasa,kwa tulosoma hesabu,katiba mpya ikija na 50%leverage itampeleka mbele kila mtanzania kwa 50%!
    Na mwisho nakubaliana na Anonymous waandishi mnayoyafanya hamna moral authority ya kihivyooo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...