Ndugu zangu,
Kwenye Uchina ya Kale kulikuwa na mwanafalsafa kwa jina la Comfucius. Katika mafundisho yake mengi aliyopata kumpa mwanafunzi wake Tzu Kung mojawapo linahusu dhana ya utajiri na mahusiano yake na umasikini.
Comfucius anasema; ukimwona mtu tajiri (aliyefanikiwa kimaisha),basi tamani kuwa kama yeye, lakini, ukimwona aliye maskini, basi, jitafakari wewe mwenyewe.
Kwa mwanafalsafa Comfusius, dhana ya utajiri haikuwa na maana kuwa na mali pekee, bali, pamoja nazo, ni uwezo wa mtu kuishi maisha adilifu na yenye fadhila (virtues). Na katika fadhila zote, ile ya unyenyekevu na ukweli ndio chanzo cha fadhila nyingine zote.
Umaskini vilevile, yumkini unaweza kuwa na maana ya kukosa mali na uadilifu. Ndio, mwanadamu waweza kuwa na mali lakini ukakosa uadilifu. Ni dhahiri, katika hali hiyo, hata mwenye mali naye ni maskini sana.
Ndugu zangu,
Nayaandika haya baada na huku nikiendelea kusoma alama za ukutani.
Kuna kitu kinatokea katika jamii yetu. Wengine wanakiona, wengine hawakioni. Na kuna wanaoonyeshwa , lakini wanashindwa kukiona. Tunafanyaje?
Ndugu zangu,
Hakuna kitu kingine bali ni watu ndio wenye kuifanya nchi. Kuna kitu kimetutokea waTanzania. Kinaendelea kuota mizizi. Na kwa vile kitu ndicho hufanya vitu, basi, mimi naviona vitu vya hovyo hovyo vikitokea katika jamii yetu. Na pengine, kwa vile tumeanza kuwa na hulka za hovyo hovyo, basi, vinavyotokea hatuvioni kuwa ni vya hovyo hovyo.
Naam, vinatokea kila leo, na kuna wenye kusimama kuvitetea vitu hivyo vya hovyo hovyo. Ni kuanzia namna tunavyouza rasilimali zetu na wenye kuuza, ni viongozi wetu waliogeuka ’ madali’ wa kutanguliza tenipasenti. Hawa wa kundi la pili ndio matajiri wetu wapya waliopungukiwa chembe nyingi za uadilifu, hivyo basi, nao ni masikini.
Na tumeimbiwa sana, kuwa nchi yetu ni maskini (japo wanamaanisha kipato pekee) na wanasahau au hawaju kuwa sisi ni maskini zaidi kwenye maadili.
Ndugu zangu,
Na tunavyoelekea sasa kwenye miaka hamsini ya Uhuru , tujifunze kutoka kwa mwanafalsafa Comfusius . Kwamba katika umasikini wetu huu kama taifa, basi, walau tujitahidi kujitafakari tulivyo huku tukiwaangalia wenzetu waliopiga na wanaondelea kupiga hatua za mafanikio ya kiuchumi.
Ndugu zangu,
Oneni kule Marekani. Hawa ni matajiri wa kipato. Wanafanya kazi usiku na mchana kutimiza ndoto ya taifa lao. WaMarekani wanaijua ndoto yao na huungana dhidi ya yeyote anayetaka kuikwamisha. Ni pengine ni katika kutimiza ndoto hiyo sisi tunalalamika kuwa Marekani ni taifa baya.
Tujiulize; ni taifa gani litaishi bila kuwa na ndoto na haja ya kuwa na maslahi ya kudumu? Hivi, ni nini ndoto na maslahi ya kudumu ya Tanzania? Je, ni WaTanzania wangapi wakiwemo viongozi wanaijua sera ya Tanzania inapohusu uhusiano wake na mataifa mengine?
Fikiri, tumepeleka majeshi yetu kuzikomboa nchi nyingine, lakini, ni vigumu kuona tumepata nini kiuchumi ukiacha sifa ya kuwa ni taifa karimu.
Angalia Rwanda. Ni kanchi kadogo sana lakini kameshajua ni nini maana ya kuwa na ndoto na haja ya kuwa na maslahi ya kudumu . Ndio maana hukusikia Rwanda ikitafuna maneno katika kuitambua Serikali ya Mpito ya Libya.
Leo Rwanda wako ndani ya DRC na wana maslahi ya migodi ya madini ya huko. WanyaRwanda wale wamepenya hadi Uganda na Burundi. Na nani atabaisha, kuwa WanyaRwanda wamepenya hata kwenye uchumi wetu.
Ndugu zangu,
Tumekuwa ni watu wa hovyo hovyo. Tupo kama hatupo. Tunayakimbia mambo ya kimsingi kwa taifa letu. Tumejikita zaidi kwenye hoja nyepesi nyepesi ikiwamo fitina na majungu. Ndio, WaTanzania tunabaguana kisiasa na kuna ambao, piga ua, watahakikisha tunapata Katiba Mpya ya hovyo hovyo ili tuendelee na mambo yetu ya hovyo hovyo.
Hatujachelewa, na tujifunze kutamani kuwa kama walio matajiri(katika maana ya mwanafalsafa Comfucius).
Ndugu zangu,
Naomba kuwasilisha hoja.
Maggid Mjengwa
Iringa.
Nakuunga mkono, ni maoni ya kizalendo kabisa. tuanze na katiba, halafu tutengeneze maslahi ya kudumu na ya msingi kwa Taifa letu ili kiongozi yeyote anayetaka kututawala (bila kujali chama chake) afuate na kutekeleza hayo kwanza. Tupo pamoja.
ReplyDeleteMjengwa umeongea vizuri.Lakini viongozi wetu si wanakwenda sana kwenye ziara huko kwenye nchi zilizoendelea?Hawaoni wanapokuwa wanapita.sisi watu wa kawaida utatulaumu bure..Ni kushambulia hao viongozi walioko madarakani.Kitu kingine ambacho naona ni ugonjwa ambao utatupeleka kubaya ni matumizi mabaya ya vyama siasa..Viongozi wanafanya kazi kwa matakwa ya vyama vyao vya siasa na si kwa ajili ya TANZANIA kwa ujumla
ReplyDeleteDavid V
Sera za Cameron ni za chama chake cha Tories na ndio maana ananganinia ushoga, ndio sera, mashoga wengi wamewaunga mkono. Huwezi kuwa na kiongozi ambaye hana mihimili ama ya chama ama ya kikundi kinachomuunga. Someni siasa (za kibepari) mujue hilo. Katiba hii inaelekea kila mtu atakua na yake. Itakuwa katiba ya wachaga hivyo mbege lazima iwepo, wazanzibari marufuku pombe n.k. Uingereza hawana katiba, mpaka leo wanatumia katiba za barabarani. Kwanini waulizeni.
ReplyDeletehata mimi naunga mkono. Ila hili la kuwasifu Wanyarwanda kwamba wapo mpaka DRC naomba tuliangalie kwa ungalifu sana na sio juu juu tu. Wakongo waishio karibu na Rwanda bila shaka watatushangaa tukishabikia hili maana machungu waliyoyapata kwa Wanyarwanda kuingia Kongo hayasemeki. Mtakumbuka Rwanda na Uganda ziliwahi kupigana ndani ya ardhi ya Kongo, mnafikiri walikuwa wanapigania nini? Kwa nini wasipiganie Rwanda au Uganda? Mtakumbuka pia kuwa Larent Nkunda aliendesha vita kwa muda mrefu ndani ya Kongo akiungwa mkono na Rwanda, ilikuwa kwa maslahi ya nani? Wakongo? Ukizungumza na watu wa maeneo kama ya Goma, Bukavu na maeneo yote ya Kivu ya kaskazini.
ReplyDeleteUmenena ukweli. Tunakwamishwa na fikra potofu (inappropriate mindsets)zilizoko miongoni mwa watanzania wengi. Tunahitaji kubadilisha hizi mindsets
ReplyDeleteKaka Mjengwa ujumbe ulioleta ni mzuri nafikiri nakuelewa unachotaka kusema, lakini mifano miwili uliyotumia katika ujumbe wako wa 'Marekani' na 'Rwanda' kwa mtazamo wangu ni problematic.
ReplyDeleteNitafocus ku-critic mifano yako ulioitoa.
Kama kuwa na ndoto ya Tanzania ni kuiga Marekani au Rwanda nafikiri Men na women of conscientious hawatakubaliana na wewe. kama kutafuta ndoto ya nchi ni
1.Kuvamia ardhi za watu.
2.KU Massacre wamiliki halisi ya ardhi
3. Kutumia slaves kuijenga nchi
4.Kuiba utajiri wa watu
5. Kulazimisha nchi nyingine kupitia vitisho vya vita jufanya biashara on your terms.
Hivyo ndivyo Marekani ilivyojenga ndoto yake. Kwangu mimi haina credibility yoyote. Where is the justice for American red Indians. Kama Marekani nchi ya Haki kwanini wasiwape uhuru Red Indians after all it is their country. Kumbuka founding fathers wa Marekani wametoka bara la Ulaya.
Kaka Mjengwa inaoonekana umeshazoea injustice ndio maana wizi wanaofanya Rwanda nchini DRC unaona sawa.
Dunia yetu ya leo imepiga hatua nyingi lakini bado kuna matatizo mengi. Kama kila nchi ikifata wanavyofanya Marekani hii dunia itakuwa haikali na vita mtindo mmoja.
Maggid Mjengwa habari kaka!
ReplyDeleteMimi nimepata bahati kidogo ya kuvitembelea vijinchi vya wenzetu, kwa sasa nipo UAE nakumbuka nimewahi kuchangia maoni yako katika tasnia tofauti tofauti, kwa hili la utaifa na maslahi yake kaka Mjengwa mi nakuunga mkono lakini kwa hili la Dola fulani kuvuka mipaka na kufanya shughuli za kujiinua kiuchumi katika ardhi ya nchi nyingine siyo jema kaka. Hivi sasa United Arab Emirates (UAE) wanajiandaa kusherehekea miaka 40 ya kuundwa kwa umoja wao na mafanikio kama nchi chini ya uongozi wa Shaikh Zayed Al Nahyan kama Rais na Shaikh Rashid Al Maktoum kama Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mtawala wa Dubai, nimejaribu kusoma nakala za waandishi na historia ya mafanikio ya UAE kwa kweli unaweza kutoka machozi, kivipi? hawa jamaa miaka 40 iliyopita walikuwa sawa na sisi, yaani uchumi usiothimilika, baada ya kugundua mafuta, wakakaa na kujipangia njia bora ya kutumia rasilimali yao kujikomboa, Maggid! Maggid! leo hii hawa jamaa hatua waliyopiga ni nani asiyejua? tukubali tukatae jamani mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi! Tanzania tuna rasilimali ngapi ambazo kama tungeweza kutumia kiufasaha tungekuwa mbali jamani! leo hii karne ya 21 bado tuna tatizo la umeme, usambazaji wa maji safi na salama, tunashindwa kupeleka/kusomesha wanafunzi wetu, tunashindwa kuwa na miundombinu ya uhakika, tunashindwa kuwa na mashirika imara ya reli na airline ya maana! hebu tizama ramani ya nchi yetu! kijiografia tu tumebarikiwa vya kutosha! hebu niambia uliona wapi duniani nchi ambayo imezungukwa na maziwa matatu makuba, mito ya uhakika kipindi chote cha mwaka inatiririsha maji, milima yenye kila aina ya madini, misitu yenye mbao bora na samaki wa kila aina wa bahari na maji baridi! halafu mnajiita masikini! huku ni kumdhihaki mwenyezi mungu! eeh mungu tusamehe waja wako tusiojua maana ya kila ulichotupa. Wasaalam kaka Maggid Mjengwa. Eid Al Adha Njema kwako na familia yako!
Hamidu A. Mashaka
shark_ham@yahoo.co.uk
hmashaka@facebook