Ndugu Zangu:

Mwanasiasa Zitto Zuberi Kabwe anaandika; ” Kama kuna jambo moja ambalo huunganisha Taifa ni KATIBA ya taifa hilo. Katiba huweka misingi mikuu ya nchi na namna ya kujenga na kuendesha Taifa. Hivyo, Katiba inapaswa kuwa ni matokeo ya mwafaka wa kitaifa kwenye masuala yote ya msingi ya nchi husika.” (Zitto Kabwe, gazeti Raia Mwema, Nov 9-17, 2011)

Kwa maandiko hayo ya Zitto Kabwe, Katiba yaweza pia kutafsiriwa kama Mkataba wa Kijamii- Social Contract . Na katiba iwe ni msingi wa utawala bora. Kwamba Katiba ni muafaka pia wa Serikali na Wananchi. Na hapa ndipo falsafa ya Shaaban Robert ya Merikebu na nanga inapokuwa na maana kwetu.


Madai ya Watanzania kupata Katiba Mpya ni madai muhimu, ya haki na ya kihistoria. Nimepata kuandika, kuwa Watanzania wenye mapenzi na nchi yenu, msikae mkafikiri, kuwa madai ya kupata Katiba Mpya ni kazi nyepesi.

Ni kazi ngumu sana, hata kama mnaowataka wawasaidie kupata Katiba hiyo ni Waafrika wenzenu na si wakoloni. Ilivyo Afrika, kwanza mtaletewa na walio kwenye mamlaka, ’Katiba Mpya’ iliyofanyiwa marekebisho madogo kwa maana katiba iliyoongezewa viraka. Haitapelekea mkawa na chaguzi salama.

Kuna kuandamana na hata watu kufa kutakakofuatia. Kuna akina Ocampo wa Mahakama za Kimataifa watakaokuja kuwanyofoa wahusika wa vurugu zitakazopelekea mauaji ya raia. Kisha itakuja Katiba Mpya. Ni njia mbaya na ya kusikitisha, lakini inaepukika, kama kuna utashi wa kisiasa. Ndio, Afrika kudai Katiba Mpya yaweza kuwa ni kazi ngumu kuliko kudai uhuru kutoka kwa mkoloni.


Nakumbuka, Prince Bagenda, Mwakilishi wa CCM kwenye Kongamano la Katiba pale Chuo Kikuu Mlimani alipata kukaririwa na gazeti la Mwananchi akitamka; ” Msifikiri kila kitu mnapewa tu, lazima mdai”. (Mwananchi Aprili 3, 2011). Ndio, Prince Bagenda alitamka; kuwa hoja ya Katiba haikuwa ya CCM. Kwamba CCM ilikubali kwa kuwa Serikali huongozwa kwa maoni ya wananchi.


Na Afrika safari ndefu huamuliwa na hatua ya mguu wa kwanza. Ukiianza safari na ’ mguu mbaya’, basi , hiyo haitakuwa safari njema. Ina maana moja kubwa, namna ulivyojipanga na safari yako kuanzia mwanzo. Nilivyofuatilia Kongamano lile la Katiba pale Chuo Kikuu Mlimani, nasikitika kusema, hata wakati ule, tuliianza safari yetu na mguu mbaya.

Tafsiri yangu juu ya alichokitamka Bagenda ni hii; Katiba ni suala la ’ Sisi na Wao’. Ni mapambano. Hapa kuna tatizo kubwa. Maana, kuna hali ya kutafuta mshindi na mshindwa. Ndio, unatafutwa ushindi na ufahari, le prestige, kama wasemavyo Wafaransa. Ninachokiona, kama tutachagua njia ya kushindana katika kuifanyia marekebisho katiba yetu, basi, hakutakuwa na mshindi. Sote tutashindwa.

Na hilo ni Neno La Leo.

Maggid

Iringa,
Jumamosi, Novemba 12, 2011

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Magid upo sahihi na nakupongeza kwa kusema ukweli. Lakini Watanzania alio wengi bado hawajajua ni nini wanachokihitaji katika maisha yao. Ndi maana wanawashangaa wamachinga na kuwaita wwenye vurugu. Ndio maana wanawashangaa CHADEMA na kuwaita wenye fujo. Siku watakpojua wanachokihitaji ndio watasema; alaah kumbe wamachinga na CHADEMA walikuwa sahihi. Pengine wakati huo inaweza ikawa too late!

    ReplyDelete
  2. Ankari Michu.. naomba uweke link ya hilo tangazo la Mganga kutoka Sumbawanga (Dr.Mkombozi), kwani tuki-click juu yake haitupeleki kwenye site yake.
    Please, saidia ili wenzangu nao wanufaike hususan kwa huduma ya kuongeza ukubwa wa sehemu za makalio.

    Aunt Fiona

    ReplyDelete
  3. Ndugu zangu.. ndugu zangu... ndugu zangu!!!!!!!?????????

    ReplyDelete
  4. huyu mjengwa ni scrap na anaongea crap tupu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...