Na Khadija Khamis-Maelezo Zanzibar
Mkurungenzi Mkuu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Alhalil Mirza ameeleza kuwa sekta ya utalii imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika Visiwa vya Zanzibar na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika sekta nyengine.
Hayo ameyasema leo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali kuhusu hali halisi ya sekta ya utalii inavyoendelea na kuimarika kiujumla .
Ameeleza kuwa Sekta hiyo imekuwa ni msaada wa kuhamasisha maendeleo katika sekta nyingi nchini ikiwemo Bandari, Uwanja wa Ndege pamoja na Miundo mbinu ya Barabara.
Aidha Mirza ameeleza kuwa katika msimu mpya wa Mwaka 2011 kumekuwepo na ongezeko kubwa la watalii ambao wanaitembelea Zanzibar ambapo zaidi ya Watalii 125,000 wameitembelea Zanzibar kuanzia January kulinganisha na watalii 97,000 walioitembelea mwaka jana.
Mkurugenzi mkuu amesema kuwa ili Sekta ya Utalii izidi kuimarika zaidi jamii inapaswa kuwajibika na kufahamu kwamba utalii ni wetu sote na sio sekta ya utalii peke yake ambayo ina wajibika na utalii huo.
Aidha amesema kuwa katika kusaidia kukuza sekta hii Wazanzibar wana wajibu wa kudumisha amani na utulivu katika nchi ili watalii waweze kuja kwa wingi na kuweza kuwekeza katika nchi Visiwa vya Zanzibar.
Amesema watalii wanapokuja kuwekeza katika visiwa vya Zanzibar wataweza kusaidia kutoa fursa za ajira kwa wananchi wengi jambo ambalo litapelekea kupunguza umasikini.
Hata hivyo amefahamisha kuwa utalii ni biashara kama biashara nyengine hivyo wadau mbalimbali wanapaswa kuitangaza Zanzibar nje na ndani ya nchi kutokana na utulivu na amani, na historia ya utamaduni wa Nchi hii.
Sambamba na hayo Mkurugenzi Mirza amesema kuwa ifikapo Novemba 4 mwaka huu wanatarajia kuondoka kwenda nchini Uengereza kushiriki katika tamasha la maonyesho kwa nchi mbali mbali ikiwemo nchi za afrika mashariki kwa muda wa siku nne.
Amesema kuwa katika maonyesho hayo nchi tofauti zitapata fursa za kuonyesha maenesho yake ambapo kwa upande wan chi za Afrika ya Mashariki zinatarajia kuonyesha maonyesho yake siku ya tarehe tisa Mwezi huu.
Ameeleza kuwa pamoja na maonyesho hayo kutakuwa na Kongamano na Semina ambapo Wahadhiri mbali mbali wataweza kutoa utaalamu wao wa kuitangaza biashara ya sekta ya utalii na kubadilishana mawazo kwa wafanyabiashara wa sekta mbali mbali ili kuweza kuengezea ujuzi na kujipatia masoko kiurahisi .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...