Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue akizungumza kwa niaba ya kundi la Nchi za Afrika wakati wa Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya mwakawa kujitolea. maadhimisho hayo yamefanyika siku ya Jumatatu katika ukumbi Mkuu wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali akiwamo Naibu Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro aliyowasilisha salamu za Katibu Mkuu, Ban Ki moon.
Na Mwandishi Maalum
New York
Umoja wa Mataifa jana jumatatu umeadhimisha kumbukumbu ya miaka kumi ya mwaka wa kimataifa wa kujitolea , huku wito ukitolewa kwa kila mtu katika nafasi yake kujitolea kwa ajili ya mtu mwingine.
Maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila Desemba tano yalikwenda sambamba na uzinduaji wa ripoti maalum ambayo kwa mara ya kwanza imeainisha pamoja na mambo mengine, nafasi na mchango mkubwa unaofanywa na watu wanaojitolea , umuhimu wake na changamoto zake.
Mwezi Novemba mwaka 1997, Baraza kuu la Umoja wa mataifa,liliutangaza mwaka 2001 kuwa mwaka wa kimataifa wa kujitolea ambapo kilele chake yaani miaka kumi kimefanyika siku ya jumatatu.
Katika maadhimisho hayo, Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue akizungumza kwa niaba ya nchi za Afrika, amesema hapana shaka kwamba Afrika ni kati ya mabara ambayo kwa kiasi kikubwa limenufaika sana na mchango mkubwa uliofanywa na unaoendelea kufanywa na watu wanaojitolea.
“Afrika inapenda kutambua na kutoa shukurani zake kwa wale wote ambao wamejitolea katika kuandaa , kuratibu na hatimaye kutekeleza miradi mbalimbali kwa njia ya kujitolea, miradi ambayo kwa kiasi kikubwa imesukuma mbele maendeleo ya bara letu” akasema Balozi Sefue.
Ameyataja maeneo ambayo maendeleo yake na serikali mbalimbali na kwa kushirikiana na wafanyakazi wa kujitolea imeweza kuwanufaisha wananchi wengi na kusukuma mbele maendeleo yao , kuwa ni elimu, afya, operesheni za ulinzi wa amani, utamaduni na uchumi.
Akasema , moyo wa kujitolea si jambo geni kwa waafrika kwa kile alichosema limo ndani ya mila, tamaduni na desturi zao. Na ni kwa sababu hiyo nchi nyingi za Afrika zilifadhili na kuunga mkono Azimio kuhusu mwaka wa kimataifa wa kujitolea.
“Kwa niaba ya nchi za Afrika tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa wafanyakazi wote wa kujitolea wanaotekeleza majukumu yao katika maeneo mbalimbali ya jumuia zetu barani Afrika. Lakini pia tunapenda kutambua mchango wa wale wote ambao wamepoteza maisha wakiwa katika harakati za kujitolea” akasema Sefue
Akabainisha kwamba kazi nzuri inayofanywa na wafanyakazi hao wa kujitolea siyo tu inasaidia kuboresha na kubadili hali ya wananchi wa eneo husika, lakini pia hata wafanyakazi hao nao wananufaika kwa kupata uzoefu na maarifa ambayo wasingeweza kupata katika nchi zao.
Na kwamba, hayo yote yanachangia sana katika kujenga na kuboresha mahusianao mazuri, kuheshimiana , kuthaminiana na hatimaye kujenga mazingira ya amani na maendeleo miongoni mwa wanajamii.
Akizungumzia ripoti iliyozinduliwa wakati wa maadhimisho hayo, Balozi Sefue amesema, ni matumaini ya Afrika kwamba , ripoti hiyo itahimiza utambuzi , uthamini na kuchagiza umuhimu na wajibu wa jamii kujitolea.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon katika salamu zake zilizowasilishwa na Naibu Katibu Mkuu Asha-Rose Migiro wakati wa maadhmisho hayo, amesema Umoja wa Mataifa kupitia kitengo chake cha kujitolea kila mwaka hupelea zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 8, 000 ambao hufanya kazi za kujitolea katika nchi 130. Kitengo hicho cha wafanyakazi wa kujitolea cha Umoja wa Mataifa kilianzishwa miaka 40 iliyopita.
Akasema wafanyakazi hao wakujitolea ingawa michango yao au uwepo wao hauthaminiwi sana , lakini wamekuwa na wameendelea kuwa kiungo muhimu sana katika kusukuma ajenda za maendeleo ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millennia.
wabunge na mawaziri wajao ndio wataonyesha mfano wa kujitolea pale ambapo mishaara yao itakuwa katika ujenzi wa miradi ya jamii..
ReplyDeletejamni aliyepiga picha, yaani Balozi anaonekana mdomo tu?
ReplyDelete