WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli amemuagiza Mkandarasi anayesimamia ujenzi wa barabara yenye kiwango cha lami kutoka Mission hospitali kwenda mjini Sengerema mkoani Mwanza, kuhakikisha anarudi mara moja kwenye mradi huo, vinginevyo atamfukuza kazi mara moja.

Waziri Magufuli alitoa agizo hilo, wakati alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Kome II, katika Kata ya Nyakarilo Jimbo la Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

Alisema anazo taarifa za Mkandarasi huyo kutoonekana katika mradi huo kwa muda sasa, kinyume na makubaliano waliofikiana na Serikali na pia kumtaka Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), mkoani Mwanza, Leonald Kadashi kuhakikisha anamwamuru mkandarasi huyo kujerea kazini haraka na kuanza kazi ya ujenzi huo wa barabara yenye kiwango cha lami kutoka Mission hospitali kwenda Sengerema mjini.

Kwa mujibu wa Waziri Magufuli, iwapo mkandarasi huyo hatafuata na kutekeleza masharti ya mkataba alioingia na Serikali, kamwe hataogopa kumfukuza kazi na kumpa kazi hiyo mkandarasi mwingine, na kwamba hadi sasa Serikali ilishawafukuza kazi makandarasi wapatao 2800, ambao walionekana kwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu katika makubaliano ya ujenzi wa barabara nchini.

"Wakala wa barabara Mwanza upo?. Nakuagiza mkandarasi tuliyempa kazi ya kujenga barabara hii ya Mission kwenda Sengerema mjini, arudi kwenye site (eneo la mradi), haraka sana. Vinginevyo afukuzwe kazi.maana hatuwezi kubembeleza mtu katika kazi.

"Kisiwepo kisingizio kwamba hakuna fedha. Njooni tuwape hizo fedha zipo...ingawa kilometa moja ya lami inachukua kama milioni 800 lakini tutawapa. Nataka barabara hii ikamilike haraka kama tulivyokubaliana kwenye mkataba wetu", alisema Waziri Magufuli huku akisisitiza kwamba haogopi kumfukuza kazi mtu kama atakwenda kinyume na sheria, taratibu na kanuni za nchi.

Hata hivyo, aliwaonya Wakala wa Barabara nchini, kuacha mara moja tabia zao za kusubiri Waziri aende maeneo yao ndiyo barabara zianze kutengenezwa usiku na mchana, na kusema, tabia hiyo ife mara moja, vinginevyo rungu lake litawashukia kwani hapendi kuona mambo yakifanyika kinyume na taratibu za nchi.

Akiliwekea mkazo swala hilo Waziri Magufuli alieleza kushangazwa na kitendo cha barabara ya kutoka Sengerema mjini kwenda Buchosa kuanza kufanyiwa matengenezo usiku na mchana wakati alipokuwa katika ziara wilayani humo akipitia barabara hiyo na kwamba ni heri wamuone mbaya kuliko kulea maovu kama hayo.

"Kuna mtindo mbaya sana wa kungoja hadi Waziri aje au Rais ndiyo barabara zitengenezwe. Tena kama kuna ugeni mkubwa, utakuta njia zinatengenezwa usiku na mchana. Mtindo huu ufe mara moja, maana nimeona hata leo kwenye barabara hii ya Sengerema kwenda Buchosa imejengwa usiku na asuhubi", alionya Waziri huyo anayesifika kwa misimamo mikali.

Hata hivyo, Waziri Magufuli alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Wakala wa Serikali wa TAMESA kuhakikisha kivuko cha Mv. Kome II kinawekewa paa la kuzuia jua na mvua kwa wasafiri, kuliko ilivyo sasa katika kivuko hicho ambapo kipo wazi, hivyo kuleta adha kubwa kwa watumiaji wa usafiri huo wakati wa masiki na kiangazi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. ndio tunataka viongozi wenye kufatilia kama hawa.

    ReplyDelete
  2. Big up Magufuli, we love you. Tungekuwa na viongozi angalau kumi tu kwenye serikari yetu nadhani watanzania tungekuwa mbali.

    MUNGU AKULINDE AKUEPUSHE NA HILA ZA WABAYA WAKO.

    ReplyDelete
  3. jamani huyu mzee anafanya kazi

    ReplyDelete
  4. Msizungushe maneno jamani, semeni tuu ndio 'products' za CCM hizo!..ukipenda boga,upende na mti wake.

    ReplyDelete
  5. ndyoo mze upo safi nakukubali sana magufuli wetu daimaaa

    ReplyDelete
  6. Sasa mpaka waziri akaongee jukwaani hela ipo mwambieni mkandarasi arudi kazini?kwanini hizo hela wanazodai kwa ajili ya ujenzi zisitolewe kwa wakati ili kazi isisimame...sio kila kitu lazima kujidai mtemi wakati unajua kosa la serikali kutokotoa hela kwa wakati...sikatai kuwa huyu jamaa ni mchapakazi bali vitisho havisaidii..vunja mkataba uone kama hawajaenda mahakamani kufungua kesi na kujichukulia mihela ya bure...muwalipe ontime na kufanya kama mkataba unavyowataka
    Ni hayo tu..utemi hausaidii

    ReplyDelete
  7. All in all, huyu jamaa jamaani anapiga kazi kishenzi! Mm binafsi ninamkubali. Kweli kungekuwa na watu kama hawa kama 20 hivi, Watanzania tungekuwa mbali sana! Big up Magufuli! We love u!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...