Meza Kuu wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu. kutoka kushoto ni Mhe. Ombeni Sefue Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Librani Cabactulan, Balozi wa Ufilipino katika Umoja wa Mataifa, Dr. Mutlag Al Qahtani aliyemwakilisha Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro, Balozi wa Sweden Mhe. Marten Grunditz na Katibu Mkuu wa mtandao wa ushirikiano kuhusu ulemavu na maendeleo Bi Maria Victoria Reina
Wanafunzi wenye ulemavu wa kutoona kutoka Taasisi ya Elimu Maalum ya Jijini New York, wakitumbuiza wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa wa watu wenye ulemavu. maadhimisho hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki ambapo mgeni rasmi alikuwa Dkt. Asha-Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum
New York
Licha ya serikali mbalimbali duniani kujitahidi kuweka sera zenye kutetea na kulinda haki za watu wenye ulemavu, bado kundi hilo la jamii linaendelea kuathirika kwa umaskini, ukosefu wa ajira , ubaguzi katika elimu na huduma nyingine za kijamii kama vile afya.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UM), Dkt.Asha-Rose Migiro, wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.
Katika maadhimisho hayo ambayo yalipambwa na kwaya ya wanafunzi wenye ulemavu wa kutoona, Migiro anasema kwamba, miongo mitatu imepita tangu yaliyopofanyika maadhimisho ya kwanza ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemevu na kwamba ingawa kumekuwa uelewa na ushirikishi mkubwa kwa watu wenye ulemavu lakini bado hali yao ni tete.
“Miaka thelathini baadaye tangu maandhimisho ya kwanza ya siku hii ya walemavu, tumeshuhudia mabadiliko makubwa, angalau sasa tunaishi katika ulimwengu tofauti ambapo kuna fursa zaidi kwa watu wenye ulemavu”. Anasema Naibu Katibu Mkuu na kuongeza
Akasema mafanikio ya safari hiyo ndefu ya utambuzi wa haki za walemavu kunatatokana na mambo mengi likiwamo la nchi wanachama wa UM kuridhia Mkataba wa Haki za watu wenye ulemavu.
Hata hivyo amebainisha kwamba pamoja na yote mazuri yaliyomo katika mkataba huo ya kuleta matumaini , kupiga marufuku ubaguzi, kutoa haki zote za binadamu na uhuru kwa watu wenye ulemavu lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
Kwa mfano akasema, migogoro mbalimbali inayoikabili dunia hivi sasa ikiwamo ya ukosefu wa ajira , kuyumba kwa uchumi, uhaba wa nishati, mabadiliko ya tabia nchi na kupanda kwa bei ya chakula. Matatizo haya yanakuwa na adhari kubwa zaidi kwa watu wenye ulemavu.
“ Watu wenye ulemavu ndio wanaoumia zaidi na changamoto hizi, ni wajibu wetu sisi sote kuwalinda. Kama inavyosema kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu. ‘ kwa pamoja kwa ajira ya dunia bora kwa wote ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu katika maendeleo” akasema Naibu Katibu Mkuu
Akasitiza kwamba ni vigumu kwa watu wenyeu ulemavu kukabiliana na matatizo hayo bila ya jumuia ya kimataifa, serikali na watu wenye mapenzi mema kuwasaidiana na kuwashikirikisha kukabiliana nayo.
“ kwa pamoja tuuchukue ujumbe wa mwaka huu na kuutekeleza kwa vitendo na usiishie tu kwenye maadhimisho. Na kama alivyowahi kusema Balozi wa amani na mtunzi mashuhuri Steve Wonder ambeye pia ni mtetezi wa haki za walemavu. Kwamba, ‘ hatuwezi kuendelea kuzungumza tu, ni lazima tufanye kitu’
Naibu Katibu Mkuu akabainisha kwaba yeye binafsi kwa kushirikia na jumuiya ya kimataifa, yuko tayari katika kuhakikisha kwamba jumuia ya kimataifa inaendelea kupaza sauti na kubadilishana mawazo ili kufikia malengo ya kuwapatia fursa shirikishi watu wenye ulemavu
Katika maadhimisho hayo Mabalozi wa Tanzania, Ufilipino na Sweden wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa, nao walipata fursa ya kuzungumza wakati wa maadhimisho hayo. Maadhimisho ambayo yalihusiaha pia mijadala ya mada mbalimbali zinazohusu masuala ya watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania katika UM Umoja wa Ombeni Sefue, yeye amesema kila mtu anawajibu wa kutambua na kuthamini uwezo mkubwa walio nao watu wenye ulemavu katika nyaja mbalimbali.
Balozi Sefue anafafanua hoja yake hiyo kwa kusema. “ kuna watu wengi wenye ulemavu huko nje ambao wanaonyesha ujasiri na uhodari mkubwa, wenyewe matumaini sawa sawa na watu wengine licha ya ulemavu wao”.
Akasema ni kwa kulitambua hilo ndiyo maana serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ubalozi wake wa Kudumu katika UM, imekubali kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Ufilipino kupitia ubalozi wake, kuaanda mkutano wa ngazi ya juu kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu.
“ Serikali yangu inajisikia fahari sana kufanya kazi kwa karibu sana na serikali ya Ufilipino ambapo Balozi zake hapa Umoja wa mataifa, zimesimamia na hatimaye kufanikisha kupitishwa kwa azimio ambalo limeliwezesha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio hilo, kuitisha mkutano wa ngazi ya juu, katika ngazi ya wakuu wa nchi na serikali, tarehe 23 Septemba 2013 ili kuzungumzia kwa kina matatizo ya watu wenye ulemavu”. Akasema Balozi Sefue.
Mwakilishi huyo wa Tanzania katika UM akasema, maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu ,yatumike kama fursa ya kurejea ahadi za kupambana na ubaguzi na kuunda fursa kwa watu wote na kujenga jamii ambayo watu wenye ulemavu hawatachukuliwa kama welengwa wa misaada tu bali kama watu wenye uwezo ambao wanatakiwa kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi.
Akaongeza kwa kusisitiza watu wenye ulemavu wanatakiwa kukumbukwa siku zote, kila wakati na kila mahali na siyo kusubiri siku ya siku ya maadhimisho tu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...