MhaririI Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda (45) (kulia), akiwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo pamoja na wakili wake, Juvenalis Ngowi (katikati) baada ya kuahirishwa kwa kesi inayomkabili ya kuchapisha habari za uchochezi. Kushoto ni Katibu wa Jukwaa la Wahariri, Neville Meena.
(Picha na Francis Dande).
(Picha na Francis Dande).
Na Ripota Wetu-Kisutu
KESI ya kuchapisha makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima Absalom Kibanda na Mwandishi wa Safu ya Kalamu ya Mwigamba, Samson Mwigamba leo imeahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Kesi hiyo ambayo jana ilikuja kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, wakili wa serikali Petronia Kisaka alieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na anaiomba mahakama hiyo iairishe kesi hiyo hadi tarehe nyingine.Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Lema ambaye aliarisha kesi hiyo hadi Februali 15 mwaka huu.
Desemba 21 mwaka jana , Wakili wa Serikali Eliezabeth Kaganda alidai kuwa washtakiwa hao wanaotetewa na wanakabiliwa na kosa la kuwashawishi askari na maofisa wa jeshi la polisi, magereza na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) kutoendelea kuitii serikali iliyopo madarakani kwa sasa ambayo inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete kinyume na kifungu cha 46(b),55(10(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wakili Kaganda alidai Novemba 30 mwaka huu,gazeti la Tanzania Daima la siku hiyo toleo Na.2553 lilichapisha waraka uliokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Waraka Maalum kwa Askari wote” ambao uliandikwa na mshtakiwa huyo kupitia safu yake ijulikanayo kwa jina la ‘Kalamu ya Mwigamba’.
Wakili huyo wa serikali alidai kuwa mshtakiwa huyo kupitia waraka wake huo kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwashawishi askari na maofisa wa jeshi la polisi, Magereza na JWTZ kutoendelea kuiiti serikali iliyopo madarakani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...