ZH POPE YATOA TIKETI KWA WAAMUZI
Kampuni ya ZH Hope Limited imegharamia tiketi za waamuzi na kamishna atakayesimamia mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Namibia itakayofanyika Januari 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mbali ya tiketi hizo za ndege, pia kampuni hiyo itagharamia hoteli (malazi na chakula) kwa kamishna na waamuzi hao wanne kwa muda wote watakaokuwepo nchini kwa ajili ya mechi hiyo.

Gharama za tiketi na hoteli kwa kamishna wa mechi hiyo na waamuzi hao watakapokuwa hapa nchini ni sh. 11,856,000.

Bajeti nzima ya mechi hiyo ni sh. 74,660,000. Hiyo inajumuisha usafiri, posho kwa wachezaji, posho kwa benchi la ufundi, gharama za kambi, dawa na maji ya kunywa wakati wa mazoezi na mechi kwa Twiga Stars. Maeneo mengine usafiri wa ndege, usafiri wa ndani (magari mawili), posho na hoteli kwa kamishna na waamuzi.

Gharama nyingine za timu ya Namibia itakayokuwa na watu 25 ambazo ni usafiri wa ndani (magari matatu), hoteli (malazi na chakula) na maji ya kunywa wakati wa mazoezi na mechi.

WAZIMBABWE KUICHEZESHA TWIGA STARS
Mechi ya marudiano kusaka tiketi ya kucheza fainali za Nane za Kombe Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Namibia itachezeshwa na waamuzi kutoka Zimbabwe.

Waamuzi katika mechi hiyo itakayofanyika Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam watakuwa Rusina Majo Kuda (mwamuzi wa kati) wakati waamuzi wasaidizi ni Stellah Ruvinga na Rudo Nhananga. Mwamuzi wa akiba ni Pamela Chiwaya. Kamishna wa mechi hiyo ni Beletsh Gebremariam kutoka Ethiopia.

MECHI YA TWIGA STARS KUONESHWA ‘LIVE’
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekipa Kituo cha Televisheni cha ITV haki ya kipekee (exclusive rights) kuonesha moja kwa moja (live) mechi kati ya Twiga Stars na Namibia itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Twiga Stars ambayo tayari imeingia kambini Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Ruvu iliyoko Mlandizi mkoani Pwani iwapo itafanikiwa kuitoa Namibia itafuzu kucheza raundi ya kwanza na mshindi kati ya Misri na Ethiopia. Twiga Stars ilishinda mechi ya kwanza ugenini mabao 2-0.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. TFF Jamani Pokeeni hiyo misaada lakini baada ya mechi mtuambie mapato yote mmeyatumiaje! sio mnaomba msaada halafu mapato mnagagawana,

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...