Timu ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (pichani)  wameomba kucheza mechi maalumu dhidi ya Twiga Stars kabla ya kuwasilisha mchango wao kwa timu hiyo.

Benchi la Ufundi la Twiga Stars kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekubali kucheza mechi hiyo ambayo itakuwa ni ya maonesho tu ambapo baada ya kumalizika ndipo Wabunge watakabidhi kile walichopanga kutoa kwa timu.

Mechi hiyo itafanyika Alhamisi (Januari 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume uliopo Ofisi za TFF kuanzia saa 10 kamili jioni.

Twiga Stars na Namibia zitapambana Jumapili (Januari 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni mechi ya marudiano kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.

GHARAMA ZA UWANJA- TWIGA STARS VS NAMIBIA
TFF imeiandikia Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuomba iondoe gharama za kutumia Uwanja wa Taifa ambazo ni fixed kwenye mechi kati ya Twiga Stars na Namibia.

Lengo la maombi hayo ni kusaidia kupunguza gharama za kuandaa mechi hiyo ambayo bajeti nzima ni sh . 74,660,000. Hiyo inajumuisha usafiri, posho kwa wachezaji, posho kwa benchi la ufundi, gharama za kambi, dawa na maji ya kunywa wakati wa mazoezi na mechi kwa Twiga Stars. Maeneo mengine ni usafiri wa ndege, usafiri wa ndani (magari mawili), posho na hoteli kwa kamishna na waamuzi.

Nyingine ni gharama za timu ya Namibia itakayokuwa na watu 25 ambazo ni usafiri wa ndani (magari matatu), hoteli (malazi na chakula) na maji ya kunywa wakati wa mazoezi na mechi.

Gharama ambazo ni fixed kwa matumizi ya Uwanja wa Taifa ni pamoja na usafi na ulinzi, umeme, maandalizi ya sehemu ya kuchezea, malipo kwa kampuni ya Wachina na asilimia kumi ya mapato.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Sawa tumekueleweni Whsh Wabunge kwa kupanga shoo yenu na wanawake. Ila msituumizie vijana wetu mkijapigwa chenga.

    TFF Wapangieni Twiga stars mechi za kirafiki zinazotambulika siku hiyo na sio kuwapotezea muda na kuwachosha hao Warembo Twiga.

    ReplyDelete
  2. wabunge kwenye kuchangia ujinga mko makini sana.kwanini hamchangii vitanda hospitalini?net hospitalini?nk tukamaliza hili tatizo kwenye hospital zetu?. mnataka vile vitu vinavyouza majina na sura zenu fasta kama kwenye mpira...mnapoteza hela kila siku maharambee kwaajili ya mpira mnaojua kabisa kuwa hamfiki popote zaidi ya kuja kusema tumetolewa kiume au wakitoka botswana south africa akafungwa sie tunasonga mbele.acheni ujinga na matumbo yenu makubwa.uncle hii ibanie ila wewe utakuwa umeisoma labda uibanie bila kuipitia aisee.

    ReplyDelete
  3. Sweetbert RwabutemboJanuary 24, 2012

    Nawapongeza sana Twiga Stars kwani mazingira wanayochezea ni magumu mno kiasi cha kujiuliza "hivi timu hii ni ya nani?" Nasema hivyo kwa sababu timu ikikabiliwa na michezo TFF inaanza kutembeza bakuli! Kwa nini hakuna mikakati ya kudumu ya kuiendeleza timu? Mabinti hawa wanajituma kuliko hata Taifa Stars lakini wametupwa kimaslahi! TFF tafuta wadhamini mahususi wa timu hii yenye hadhi kitaifa kama Taifa Stars lakini haina mahali pa kushika kimatumizi kwa ujumla wake.TBL,SBL na makmpuni mengine wako wapi kuunga mkono timu hii inayoonyesha maajabu kwa kushinda michezo yake mingi ya kimataifa bila hamasa? Ingekuwa hali ngumu hii iko kwa taifa Stars ingekuwaje? Wahusika hasa TFF mbuni mikakati ya kuweka timu hii iwe imara kimahitaji na si kutembeza bakuli ikikabiliana na michezo muhimu!

    ReplyDelete
  4. Sweetbert RwabutemboJanuary 24, 2012

    nimetoa maoni yangu mazuri tu mmeyafunika! siwaamini tena!

    ReplyDelete
  5. Ahsanteni Waheshimiwa Wabunge kwa Busara na kuokoa Jahazi hili!.

    Pia ingekuwa heri kama Shs. Milioni 90 alizoiba Ester Budili na wenzake wa Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu tungeizamisha hapa ktk gharama ya Bajeti Shs. Milioni 75 ya Timu ya Twiga Stars!

    Angalau ingebaki chenji ya Shs. 15 Milioni hivi na Maendeleo ya Soka Nchini yangekuwa bora kuliko wao akina Ester kuhongea pesa Wanaume, kupakia poda Saluni,kuchezea Taarabu Magomeni, kulewea pombe na kununulia magari!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...