JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
TAMASHA LA KUMBUKIZI YA MASHUJAA WA VITA VYA MAJIMAJI KUFANYIKA SONGEA 25 – 27 FEBRUARI 2012
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna Tarishi atakuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Tamasha la Kumbukizi ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji litalofanyika Mkoani Ruvuma tarehe 25 hadi 27 Februari 2012.
Tamasha hilo ambalo limeandaliwa na Shirika la Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma litafunguliwa tarehe 25 Februari katika Makumbusho ya Vita vya Majimaji mjini Songea.
Madhumni ya tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka ni kuwakumbuka mashujaa 67 walionyongwa tarehe 27 Februari 1907 katika harakati za kupinga ukoloni wa Mjerumani Baadhi ya mashujaa hao ni Ndugu Mputa Gama, Songea Mbano, Mpambalyoto Soko na MajiyaKuhanga Komba.
Baada ya ufunguzi waalikwa watatembelea vivutio vya Utalii katika Wilaya ya Namtumbo.
Siku ya Pili, tarehe 26 Februarin 2012 itafanyika Warsha katika ukumbi wa Songea Club ambapo mada tatu muhimu zitawasilishwa. Mada hizo ni:
Uongozi na Maendeleo katika Sekta ya Utalii itakayotolewa na Frateli John Kasembo;
Mchango wa Dini katika maendeleo Kusini mwa Tanzania itakayotolewa na Profesa Betram Mapunda;
Utalii na Maendeleo ambayo itatolewa na Bwana Donatius Komba.
Siku ya Tatu na ya kilele mgeni rasmi atakuwa Mhe. Said Thabit Mwambungu, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Tamasha litahitimishwa kwa maandamano kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi mahali waliponyongewa Mashujaa hao 67 ambapo viongozi wataweka mashada ya maua kwenye Mnara wa kumbukumbu ya mashujaa hao
Hapo Mkuu wa Mkoa atayapokea maandamano na kukagua gwaride. Baada ya hapo atatembelea maonyesho ya wajasiriamali na kufungua onyesho maalum la Dkt. Lawrence Gama na kufunga tamasha kwa kuwahutubia wananchi.
Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wanakaribishwa kuhudhuria tamasha hilo la Kumbukizi ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji.
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
24 Februari 2012
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...