Ndugu Michuzi na wasomaji, hamjambo!
Kuna jambo katika jamii zetu za kiafrika, lahitaji kuongelewa na kubadilishwa kwani haliendani na wakati. Jambo hili ni lile la kumtoza mahari kijana anayeoa. Wengi mtakubaliana nami kuwa watu huoana kwa kupendana na kwa hiari yao (asilimia kubwa na siyo ile ya kulazimishwa, 'arranged marriage'), kufuatia  makubaliano yao wenyewe hatimaye kuwajulisha wazazi/walezi. Uamuzi huu huleta furaha kubwa katika jamii husika, tokana na kwamba wazee au wazazi na vijana wanao oana huongezewa heshima katika jamii zao kwa namna mbalimbali. Ingawa jamii zetu za Tanzania (Afrika kwa ujumla) hutofaautina ktk mambo ya kuozana, bado kuna mifano mingi ya kufanana; moja wapo kubwa ni hili la kumtoza mahari kijana anayeoa, 'dowry'.
Historia yatufundisha kuwa hapo zama za kale kijana mwenye heshima na adabu ktk jamii; aliweza kujipatia mke bila hata ya kutoa shilingi. Kuku au mbuzi alitolewa kwa wazazi wa binti kama shukrani kwa kupewa mke. Hii haikuwa na maana kuwa thamani ya binti/mke ni sawa na kuku au mbuzi aliyetolewa kwa wazazi wake, bali SHUKRANI. Hivi leo wazee wanawatoza vijana mang'ombe, na hata mamillion ya fedha, ili kujitajjirisha na kusahau sehemu muhimu ya kiapo cha mapenzi, 'Love'. Je huu ni utajiri wa halali?
Kitendo hiki cha kutoza mahali ni sawa na umilikishwaji wa binti kwa kijana aliyemuoa. Tafsiri nyingi mbaya na mateso makubwa kwa mabinti vinasababisha kurudisha nyuma maendeleo ya wanawake katika jamii zetu. 

Jogoo makunja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 44 mpaka sasa

  1. MAHARI KAMA MAHARI, HAINA TATIZO, NI VEMA IKAENDELEA KUWEPO, NI JAMBO ZURI, NI KIELELEZO CHA UTAMADUNI, NI ALAMA (SYMBOL) YA KUONYESHA SHUKURANI KWA WAZAZI WALIOMLEA BINTI, PIA MAHARI HULETA THAMANI YA BINTI KWAMBA AMEPATA BARAKA KUTOKA KWA WAZAZI WAKE. HEBU FIKIRIA BINTI ALIYEOLEWA BURE!! NI KAMA HANA THAMANI, KAMA HANA BARAKA - KUNA USHAWISHI MKUBWA SANA KUTOKA MAGHARIBI KWAMBA TUACHANE NA MAHARI, HAPANA, SIO KILA JAMBO KUTOKA MAGHARIBI NI ZURI NA NI LAZIMA TULIFUATE. TATIZO NI BAADHI YA WAZAZI NA FAMILIA KWA UJUMLA WANATUMIA VIBAYA MILA HII KWA KUGEUZA KITEGA UCHUMI. INAPASWA MAHARI ITOZWE KWA KIWANGO CHA KAWAIDA KABISA, ANACHOWEZA KUMUDU BWANA HARUSI BILA WASIWASI. UKIWEZA TOA ELIMU KWA JAMII NA KWA WAZAZI WASIGEUZE MAHARI KUWA KITEGA UCHUMI

    ReplyDelete
  2. Mahari ni upuuzi mtupu, wew waache tu wasubiri mahari, watadoda nakwambia.
    Jamaa yangu alimtosa demu kisa familia wanang'ang'nia mahari, baadaye wanambebembeleza jamaa, akakataa tatu, demu kadoda hadi leo.

    ReplyDelete
  3. MAHARI NI ZAWADI YA KISHERIA KWA MKE NA SIO MALIPO KWA WAZAZI, HIVYO MKE NA APEWE ZAWADI YAKE NA MUMEWE KWA KADIRI YA MAELEWANO. NA SI KAWAIDA MKE KUTAJA KIWANGO KINACHOMUELEMEA MUME MTARAJIWA.

    WAZAZI HAWANA HAKI YA KUCHUKUA CHOCHOTE KATIKA MAHARI YA BINTI YAO.

    MAMBO YANAHARIBIKA TUNAPOGEUZA UTARATIBU WA NDOA TUKAFANYA ETI MAHARI NI MALIPO KWA WAZAZI.

    ReplyDelete
  4. Kidini(Islam) mahari ni haki ya Bint muolewaji,yeye ndo ana haki ya kutaja mahari,na anajuwa mwenyewe kiasi gani ili asimkamuwe mchumba wake.....
    Mambo ya sasa hivi wazazi kuchukuwa mahari au kutaja sijui sukari,shuka,mbuzi,au Bint kuamua kuwagawia kidogo kidogo jamaa zake wa karibu,hayo ni mambo ya kitamaduni.

    Mimi naona hakuna ubaya kwa hilo,hata huyo Bint kama kweli ni mbana matumizi atakuwekea na wewe siku ukikwama atakusaidia.,,,Kama umetozwa mahari kaka katoe tu upate mke,kwani hao watu au yeye wanastahili shukrani kubwa hata zaidi ya hiyo,,,

    Ahlam ,,,UK

    ReplyDelete
  5. Tatizo ni mitizamo tofauti juu ya suala la mahari na ndoa. Watu wa jamii/makundi tofauti hutofautiana mitizamo. Mfano, Kwa waislam ndoa ni mkataba baina ya mke na mume kuishi pamoja kwa wema na kama ikilazimu, kuachana kwa wema. Mahari ni moja ya vigezo au masharti lililowekwa na Mwenyezi Mungu ili ndoa (mkataba) huu uwe halali.

    Kwa mujibu wa Uislam, mwenye haki ya kuamua kiasi cha mahari ni binti anayeolewa. Binti ana haki ya kutaja kiasi chochote anachoona kinafaa. Hata hivyo, Uislam pia unasema kuwa ndoa ambayo mahari yake ni ndogo huwa na baraka. Na msingi huu ikiwa binti kweli anampenda mwanamume anayetaka amuoe, bila shaka atataja mahari ambayo muoaji ataimudu bila shida.

    Mahari, kwa mujibu wa Uislam, ni lazima na si hiari na inaweza kuwa chochote, hata kama ni kijiko chatosha kuwa ni mahari. Hivyo ndoa pasi mahari si halali.

    ReplyDelete
  6. Ndugu yangu bado hujaenda kwenye mada inavyotakiwa, Mahari ni Muhimu kwenye dini na Mila na kote huko huwa zinatofautiana kama dini ya kiislamu ukisoma vizuri kwa undani utaelewa kwanini mahari inatolewa na nani anahaki ya mahari? Na pia mwanamke halazimishwi anaulizwa ila wazazi wanahaki pia ya kujuwa anaye muowa ni nani? Na wazazi wake wanatokea wapi na inakubalika kuchukua muda kabla waowane ila pande mbili zijuane. Kuhusu mahari ni ya mwanamke kwa dini ni laZima kumpa mkeo, kama huna dini fanya unavyopenda nijuu yako wewe, ukiwa huna dini na husomi utaiga mila za nje huko kuchukuana kama wanyama badae unaowa mtoto wa baba au mama bila kujuwa, mahari humpi mnaowana kama wazungu ikifika kugawana nusu nusu ndio nyie mnawaruka wake zenu sasa hunalolote. Hadhi ya Mwanamke mpe mahari yake kama utunzo ila wazazi sio lazima ukipenda na hujalazimishwa kutowa mamilioni ni mwanamke ndio anatamka, ndoa nyingi za hapa bongo ukitizama zimetoka kwenye mila na dini zimejichanganya mambo mengi mahari yake yamekuwa kama contract za kununuwa nyumba ni ndoa za Hollywood. Somesheni watoto zenu Elimu ya Dunia,Dini. Msiharibu ukweli wa ndoa zetu mnapenda haraka ya kuowana na kuachana mnakuwa haraka.

    ReplyDelete
  7. Mdau wa Kwanza kaongea point, mahari anataja mwanamke na pia sivibaya mzazi akipata kama alivyoelezea mdau wa kwanza, Tatizo linakuja ndoa zetu zimejichanganya kila tabia na mila za africa na nje na dini hapo sasa. Kama kweli wanafata mahari ya mila sizani kama pesa nyingi au vitu vingi havina garama, kama dini ndio kabisa inataka Elimu kwa wazazi na watoto, watu mnapenda ushauri wa magharibi wakati wao ushauri wa ndoa unawashinda, ndoa za hapa ni kweli imekuwa kama kitega uchumi, ndomana nikasema wakisoma Elimu ya mahari kwenye dini bila kuambiwa soma mwenyewe utaona urahisi, leo umeleta ushauri wa magharibi kesho utaleta pia wa ndoa za kutaka jinsia moja.

    ReplyDelete
  8. Mahari kama zawadi hata Magharibi wanatoa kulingana na uwezo wa Kijana anayechumbia ..Suala la kusema msichana 'kadoda' nikuonyesha mwandishi ni mtu anayeamini 'mfumo dume'! Kama kijana anajiamini na mapenzi yake kwa msichana ni mazito, zamani walikuwa 'anamsola' yanakwisha baada miaka kupita na wamejaaliwa kuzaa labda watoto watatu wanawaletea wajukuu wazazi wa pande zote mbili 'tambiko linafanyika' vijana watukutu wanasameheana..Mahari inaweza kuwa kikwazo lakini nasaba na kabila analotoka kijana linaweza pia kuwa kikwazo..! Mambo yanakwenda kwa kasi siku hizi katika 'dunia ya utandawazi lakini zawadi (mahari) baina wawili wapendanao hutolewa ..tuiite mahari au zawadi ya upendo kwa mchumba, utamaduni huu utaendelea ..hadi binadamu atakapo kosa ustaarabu!

    ReplyDelete
  9. Vijana wa enzi hizo walikuwa na ADABU. Vjana wa siku hizi HAWANA ADABU KWANI HULAZIMISHA NA KUSHAWISHI KUONJESHWA TUNDA kabla ya ndoa. kWA HIYO LAZIMA WALIPIE MAANA HIYO NI OFF-SIDE HARAM. Mzee wa Kibumaye

    ReplyDelete
  10. Huo ni utamaduni wa kiafrika! Wala hauna madhara yoyote.
    Katika hali ya kawaida mahari huwa haipangwi muoaji akashindwa kutoa kwa sababu ya ukubwa ukiona hilo linatokea basi ujue lipo tatizo kwamba wapangaji wamelenga kwenye uchumi badala ya kutimiza mila na desturi.

    Sasa hapa kuna hoja nyingine inazuka kwamba suala la mahari linategemea utamaduni katika kila kabila kwa mfano ukiangalia baadhi ya michango katika mada hii inaonesha hiyo tofauti ya makabila kuhusu mahali. Wakati makabila mengine mahari hupangwa na binti na yeye ndiye hupokea makabila mengine mahari hupangwa na wazazi na hao ndio wanapokea hiyo mahari na ni halali yao kutumia.

    kwa hiyo kama nilivyosema hili ni suala la mila na desturi na inafaa ziendelezwe kwa ajili ya kulinda heshima ya ndoa kama ilivyokuwa miaka nenda rudi haya mapungufu yanayojitokeza sasa kwa sababu ya kuchanganya tamaduni na kuonekana kama mahari imepitwa na wakati ndiyo yanyopaswa kurekebishwa badala ya kujadili kama mahari anafaa au haifai.

    ReplyDelete
  11. Wewe mleta mada na Jamii yako inayo kuzunguka kwanza mnatakiwa kujua nini maana ya MAHARI,hupangwa na kutolewa na nani na wakati gani hutolewa; ukishayaelewa hayo yote utafahamu nini umuhimu wake katika jamii zetu na sio hizo jamii unazoziona zimeendelea kwa kutokuwa na kitu hiki.

    ReplyDelete
  12. Nyie mnaosema mahali ni zawadi ya kisheria kwa mke, kwani mtoto wa kike ana tofauti gani na mtoto wa kiume?

    Basi kama ni kutoa zawadi zitolewe pande zote mbili. Mambo ya mahali yamepitwa na wakati na ndio maana wanawake wengi wanateswa na waume zao maana wanakuwa kama wanawanunua.

    ReplyDelete
  13. KIDINI 'YA KIISLAMU' MAHARI NI ZAWADI YA MTOTO WA KIKE NA WAZAZI HAWANA HAKI HATA KIDOGO. KIMILA NDIO MAHARI WANAGAWANA PALE PALE MJOMBA, SHANGAZI BABA NA MKAJA WA MAMA SIJUI HUYU KAMA ANAPEWA CHOCHOTE ILA KANIKI; WANAWEKA VIFUKONI HALAFU WANATEMBEZA VIKADI VYA KUOMBA MISAADA YA KUFANYIA HARUSI YA MTOTO WAO. HAPO NDIO TUNATAKIWA KUBADILIKA.

    ReplyDelete
  14. mahari ni samani kwa mwanamke sio umchukue tu kama umemuokota na mahari sio biashara ya kununua mwanamke

    ReplyDelete
  15. mleta post hii laiti ungelisoma maelezo yako kabla ya kumletea michuzi ungeliona ni namna gani unashangaza.

    unaposema kuwa mahari haiendani na wakati, unamaanisha kuwa unataka iwe kama watu wa nchi za ulaya, marekani na kwengineko. Kwa maana nyengine ni kusema unaona mfumo na utamaduni wa wazungu ni bora kuliko wa muafrika.

    Sijui mwenzangu unafata dini gani lakini katika dini ya uislamu, mahari imesisitizwa na ni sehemu ya ndoa. Mume humpa mke zawadi (mahar) mke kwa kukubali kuolewa naye. Kinachosisitizwa sana katika uislamu ni kuwa kutolazimishwa ua kutakiwa mahari kubwa mno.

    Laiti ungelisema kuwa jamii zetu tuwache mtindo wa kutaka mahari kubwa mno, turudi na kufanya kama ilivyokuwa huko nyuma hapo ningelikubaliana nawe, lakini kusema mahari imepitwa na wakati nakuona umekuwa miongoni mwa wale wanaokataa kwao, wanaowaita wenzi wao "waswahili" kwa kuwa tu bado wanafata mila na utamaduni wa dini na makabila yao.

    Paragrafu yako ya mwisho imenifurahisha sana kwa namna ulivyoanza "....hapo zama za kale kijana mwenye heshima....." naam, huon ndio wakati unaotaka tuisende nao kwani vijana wa kisasa hawana heshima!!!!!

    ReplyDelete
  16. Tutaendelea kuwa watumwa na mambo hayo ya kiislamu ati mahali hayo mambo yalikwisha pitwa long ago , nani siku hizi kijana anataka mbo ya kuoa mwanamke asiempenda au nani msichana anaetaka kuolewa na mumeambaye hayupo moyoni mwake?

    Tuache hio tabia ni nshenzi na utumwa tangu linio mke alinunuliwa kama watumwa waliokuwa wakiuzwa kwenda marekani na uarabuni na wengine kupelekwa huko kuwa wasenge wa waarabu hususan waunguja au wazanzibari wengi walinunuliwa kama watumwa na kuwekwa vimada huko ma uarabuni.

    Ina maana ukimchoka mkeo umeisha mchimbua kotekote na mitoto unamfukuza na hiyo Mahali urudishiwe? ACHENI UJINGA WA KIZAMANI MWANAMKE SIO MTU WA KUNUNULIWA AU KUUZWA KAMA MTUMWA

    ReplyDelete
  17. kwa nilivyo muelewa mtoa mada ametoa maoni kama matatu ingawa sikumelewa kua alikua anazungumzia culture, dini au maoni tu.
    Alielezea kua watu wanapendana wenyewe ni kweli lakin wakishapendana tu wanabidi wafuate misingi ya kisheria ili kuona. ameelezea swala la mahari hili kwa baadhi ya watu ni swala la kiitikadi na hikma yake ni ileile ya kuonyesha mapenzi ingawaje itikadi nyingi ziko dhidi ya mahari kua ghali.

    Alitaja vilevile kua mahari yanrudisha nyuma maendeleo, lakin hakusema vipi ni vizuri kama akifafanua. Watu kutiana mimba ovyo bila kufuata misingi au maadil ikiwemo mahari ndiko kunakorudisha nyuma maendeleo. watoto wengi ambao wana maadili mabovu yanatokana na family zenye back ground mbovu kama zile ambazo hazikufuata utaratibu mzima wa ndoa ikiwemo mahari.

    ReplyDelete
  18. MAHARI NI MALIPO YA MKE WALA SI WAZAZI NI KITU KAMA ZAWADI NDO WENGINE HUOMBA WACHONGESHEWE FURNITURE, AU MWENGINE ANAOMA ANUNULIWE DHAHABU....MAHARI INAKUWA MBAYA KWA UTARATIBU WA WAZAZI WA SASA KUTAKA PESA NYINGI NA KUFANYA MTOTO WA KIKE KAMA KITEGA UCHUMI..SIJUI NG'OMBE NA MIPESA TELE HUO UTARATIBU NDO UFE..NI BINTI NDO ANAPASWA ASEME ANATAKA NINI AU KIASI GANI?...NA KAMA BINTI ANAMPENDA MTARAJIWA WAKE HAWEZI KUMKOMOA KAMA NDUGU/FAMILIA INGESEMA WAO...KWAHIYO NI NGUMU HATA HAO WAOAJI KUTOROKA.

    ReplyDelete
  19. Mtoa mada hajullikani maoni yake kua ni ya dini, culture au kitu kingine. Lakin amezungumzia kua watu hupendana kwa hiyari ni kweli lakin wakishapendana ni lazima wafuate sheria ni sawa na kwenda kituo cha polisi ukasema nimeiba ukategemea uachiwe.
    Dini nyingi ziko dhidi ua ughali wa mahari lakin ni lazima yatolewe kama dalili ya mapenzi.

    mahari hayarudishi nyuma maendeleo kama muandishi alivyodai. kutiana mimba ovyo bila kufuata utaratibu sahihi wa ndoa ndiko kunakorudisha nyuma maendeleaodoa ikiwemo maendeleo.

    ReplyDelete
  20. Wanaotozana MANG'OMBE hawaiti hii mahali, wana maneno yao. Sisi waswahili hakuna mtu yoyote anayeoa kwa kutozwa Mbuzi, achilia mbali MANG'OMBE.

    Kama alivyosema mdau hapo juu kwamba mahali ni zawadi kwa mwanamke anayeolewa ingawa kuna familia zinaendekeza njaa na kudhania kwamba wanatakiwa wafaidike kifedha binti yao anapoolewa.

    ReplyDelete
  21. Jogoo Makunja:

    Kama ni mashambulizi umepiga Kwenye Makao ya Adui tena kwa Makombora ya NATO yanayoshuka ktk madege yasiyo na Marubani!.

    Hili suala limekuwa ni mgogoro tosha kwa jamii yetu kwa vile kwa sasa Mahari inachukuliwa kama MTAJI na Muoaji ni kama SACCOS ya kutoa Mapesa hayo.

    Ingefaa Mahari izingatie hali halisi ya Muoaji kiuwezo na sio akomolewe hadi Ndoa aione ni chungu, au aoe na akishatozwa Mahari ndefu alipize kisasi kwa Binti baada ya kumuoa.

    Kwa sababu Binti atakuwa anafahamu uwezo wa Muhusika hivyo angependekeza ni kiwango gani Jamaa anaweza kumudu.

    ReplyDelete
  22. Zaidi ya Mahari pana Jamii zingine ktk Makabila utasikia panatokea gharama zingine ambazo hazitamkwi kuwa ni Mahari lakini ukiangalia kimaana zinaingia ktk Mahari,Mfano:
    -Koti la Babu,
    -Mbeleko ya Mama,
    -Mkaje,
    -Kitanda cha Dada,
    -Jogoo la Bibi,
    -Pombe ya Wajomba,
    -Kapu la Shangazi, n.k

    Sasa ukija chukua Majumuisho unakuta pesa ndefu kabisa imetoka kama sehemu ya Mahari!

    ReplyDelete
  23. Ukiangalia kwa Upande wa pili suala la Mahari kuwa ya Tamaa limesababisha Thamani ya Mwanamke kushuka badala ya kupanda.

    ReplyDelete
  24. Baadhi ya watu anapotozwa Mahari ya Fedha lukuki, asalaleee,,,,,,, angalieni Binti yenu atakavyo fanyishwa kazi ngumu kama Punda huko kwa Mume aendako!

    Mtajiuliza Wazazi kwa nini tulimuozesha kwa hela nyingi?

    ReplyDelete
  25. Mtoa mada hajullikani maoni yake kua ni ya dini, culture au kitu kingine. Lakin amezungumzia kua watu hupendana kwa hiyari ni kweli lakin wakishapendana ni lazima wafuate sheria ni sawa na kwenda kituo cha polisi ukasema nimeiba ukategemea uachiwe.
    Dini nyingi ziko dhidi ua ughali wa mahari lakin ni lazima yatolewe kama dalili ya mapenzi.

    mahari hayarudishi nyuma maendeleo kama muandishi alivyodai. kutiana mimba ovyo bila kufuata utaratibu sahihi wa ndoa ndiko kunakorudisha nyuma maendeleaodoa ikiwemo maendeleo.

    ReplyDelete
  26. Mahari ni moja ya masharti ya ndoa katika tamaduni mbali mbali. Wengine wanatumia pesa, mifugo, pete, nk. Mahari ni alama ya penzi. Baada ya mahari wanandoa wanatakiwa wakubali masharti mengine ikiwemo tendo la ndoa, majukumu ya kuendesha nyumba, nk. Hivi sasa kuna wabongo wako tayari kumuhonga mwanamke gari au nyumba ili awe girlfriend wake lakini akiambiwa atowe mahari anaanza na kusema mambo ya kizamani. Kabla mahari watu walikuwa wakibakana tu sasa wewe unataka kuturudisha kwenye enzi za mwenye nguvu ndie anayepata penzi!!

    ReplyDelete
  27. Naungana nawe anonymous Tue Mar 20, 09:51:00 AM 2012 uliyenitanguliya. kwa kuengezea Mahari ni zawadi kwa kuonyesha shukran na upendo kwa binti au mwanamke unayetaka kumuowa.

    Tunapogeuza maana na kusudio lake ndio matendo na fikra mbaya zinapofuatia.

    ReplyDelete
  28. hivi kwani huko uklaya hakuna mahari? mbona katika lugha zao huo msamiati hupo? hilo neno DOWRY limetoka wapi kama hao wazungu hawana mahari?

    fikiria kwanza ndugu kabla ya kuandika.

    ReplyDelete
  29. Mdau uliyezungumzia kuwepo kwa neno DOWRY ulaya kunamaanisha kuwepo kwa MAHARI naomba uelewe kuwa kuwepo kwa neno THELUJI katika kamusi ya Kiswahili hakumaanishi kuwepo kwa SNOW katika nchi zinazozungumza Kiswahili. Mbona hata neno KANGAROO linatumika Ulaya wakati mnyama huyo anapatikana australia?

    ReplyDelete
  30. KAMA HUKO ULAYA HAWANA MAHARI BASI NDO MANA NDOA HAZIDUM, KWANI NI RAHISI KUOA NA KUDIVORCE KISHA KUOA MWINGINE. LKN KM UNAJUA GHARAMA ZA KUPATA MKE, BASI HAUTAOA TU KIRAHISI RAHISI, UTAIFIKIRIA HIYO MAHARI KWANZA KABLA YA KUTOA DIVORCE. MAHARI IDUM, WE UNATAKA BUY ONE GET ONE FREE

    ReplyDelete
  31. Anon #2, Kama huyo jamaa yako alimpenda huyo binti asingeshindwa kumalizana na familia kuhusu suala la mahari. Sijawahi kusikia mtu kashindwa kuoa kwa sababu ya mahari, kwani huwa ni heshima tu na sio lazima mtu amalize kwa mkupuo hiyo mahari, anatoa kwa uwezo alionao bila kuathiri maisha yake kiuchumi. Nimeishi kijijini na mjini, na hiyo ndiyo hali halisi. Huyo binti amshukuru Mungu huyo bwana aliachana naye, maana angekuja kujuta baadae.

    ReplyDelete
  32. Mahari ni muhimu acha ubahili tatizo isiwe kubwa sana iwe kiasi kinachoeleweka. acha kuiga maisha ya kizungu kunyanyasika labda wewe mie nimeolewa na ng'ombe kadhaa ninaishi kwa raha

    ReplyDelete
  33. TATIZO AKINA KAKA WA KILEO WANAPENDA MTELEMKO SANA NDO MAANA WANAOGOPA MAHARI. wako radhi wakahinde bar lakini mahari wasamehewe. nina watoto wa kiume watatu na wote wakioa tutatoa mahari...ni MILA NA UTAMADUNI!

    ReplyDelete
  34. Kama kulipa Mahari kunakushinda utawezaje kumhudumia huyo mke? Mahari inafanya kijana ajitume aweke mipango maalumu ya maisha yake sio kukurupuka. Leo hii vijana mnataka kukurupuka tu ndio maana matatizo hayaishi kwenye ndoa.

    ReplyDelete
  35. Mnahangaika na kukataa mahari ambayo ni heshima kubwa sana kwako mtoaji kwa wakwe zako na kwa binti unayemchumbia.

    Mimi ningeona ni muhimu kuzungumzia gharama za arusi ambazo zimekithiri mno Bongo.Michango mikubwamikubwa na kufuatiliana na michango hiyo ni kero.Hivi nani alisema arusi iwe ya mamilioni ya pesa na vikao vya vurugu kila kukicha kisa eti kuongelea gharama za harusi wakati hata wanandoa hao hawatapewa chochote.Mimi nilifurahi sana nilipotoa mahari na nilijisikia kuthaminiwa na mchumba wangu pamoja na wakwe zangu. Kama mtu huwezi kutoa mahari huna sidhani kama wakwe au huyo mchumba atakukataa.

    kama watu wanahonga vimada magari na kuwajengea nyumban na kuwagharimia kwa hili na lile, iweje wewe ushindwe kumgharimia mke wako ambaye ndio mpenzi wako wa kukuzalia watoto,kukujali,na kukutunza? Tusiige mambo ya hawa jamaa huku ughaibuni, na wao kuna mambo wanayafanya hamjui tu.

    ReplyDelete
  36. Kuna wachangiaje wengine bana,mabongolala kweli!

    Mimi,sitachangia chochote kuhusu 'mahari', kwasababu wachangiaji wengi waliopita,wamemaliza kila kitu. Hususan,wale waliozungumzia msimamo wa Uislamu na mila za kiafrika.Ambazo kwangu mimi,ndio zina-prevail,kuliko utamaduni wa kimagharibi!
    Kwa msingi huo,kulipa mahari,kama mahari, ni kitu kizuri na kina mantiki yake, ila tatizo litabaki kwenye kulipishwa mahari makubwa/mengi!

    Lakini la pili,kuna mchangiaji mmoja,amegusia kidogo historia ya utumwa na Z'bar. Inaonesha wazi kwamba, historia kwake imempita kushoto! Inafaa arudi kwenye vitabu vya historia ili ajue ukweli wa mambo.

    Z'bar,ilikuwa ni soko la watumwa na sio walikopatikana watumwa! Hivi ni vitu viwili tofauti!

    ReplyDelete
  37. Mahari ipo kila kona ya dunia ila inatumiwa au kuitwa jina tofauti.

    Ulaya, mke hapewi mahari wala familia yake haipati kitu kutoka kwa mume. Ila wakiachana, mke anapewa "mahari" kutoka kwa bwana ili aweze kujitunza au kama zawadi ya kuvuna matunda yao pamoja. Kwa kiingereza ni divorce settlement. Utakuta mke anapewa nyumba pamoja na pesa kila mwezi. Pia ana haki ya kuwaona watoto wake, joint-custody. Tanzania, watoto ni mali ya mume, mke anafukuzwa kama mbwa.

    Pia, ulaya watu wana wake wawili vile vile, ile wao wanawaita wachumba nje ya ndoa (mistresses) lakini watoto wa wachumba wana haki ya mali ya mume. Kila mume ana hamu ya kuwa na mke wa pili na wa tatu kwa sababu nyingi zinazoeleweka. Ndoa za Marekani kwa sasa zinaachika kwa asilimia 50%. Yaani, nusu za ndoa zote zinaharibika kwa sababu kadhaa. Katika chuo changu, nina rafiki mmoja tu kati ya 40 ambaye wazazi wake hawajaachana kwa mfano. Kuna milioni ya raia wa Kimarekani wanalelewa na mzazi mmoja au hata na bibi zao tu.

    Afrika, mahari inatumiwa na wazazi wa mke kama pensheni hasa kama hawana uwezo. Kama wanavyosema wadau, msichana ndio ana haki ya mahari lakini mara nyingi wazazi wanaingilia katika maswala haya. Ni sawa sawa na sheria za kiislamu zinazosema lazima mke wa kwanza akupe ruhusa kuoa mke wa pili, lakini kila mtu anajua kuwa hamna mke atatoa ruhusa hio. Lakini haiwazui wanaume kuoa mke wa pili au wa tatu.

    Nina mjomba wangu ambaye hajawalea watoto wake wa ndoa ya kwanza. Gharama zao zote za maisha na nyumba ilikuwa inalipwa na mdogo wake. Lakini msichana wake ilipofikia muda wa ndoa, kakurupuka na kuramba mahari yake yote. Mume wa msichana wake ni sawa na umri wa baba yake mzazi, lakini hakujali, kwa kuwa amempa mahari nono na msichana hajapata chochote na kawa mke wa pili.

    Tutafika lakini njia ni refu sana.

    ReplyDelete
  38. We we acha kukwepa mahali,katoe tu usitafute kuungwa mkono kwa kuharibu mila zetu.Katoe mahali usitake mteremko,halafu ukioa ndo tutafikiria kufuta,acha uoga na kuzoea dezo.Bia unadoea,sigara unadoea,ana mahali usilipe!! hee! ubwete gani huo.Basi kaoe kusiko mahali ni chaguo lako.Weee jamaa,Mpare anaafadhali!

    Nani aliwahi kushindwa kutoa mahali kwa kumbukumbu zako?Kwanza mahali haiishi.

    Mahali inaheshima zake na utamu wake.Kwanza katika mila zetu hakuna mwanamke anayekubali kwenda bure kwa mume.Mahali si kikwazo,sehemu nyingi ni ceremonial tu hakuna wanaotoza kiwango cha kununua nyumba, acheni kukuza mambo walongo nyie.

    ReplyDelete
  39. Hivi tunaposema tudumishe mira tuna maana gani/ hizi ndo mira zenyewe. Ila mahari inakuwa chungu unapokuta familia imeegamia kiuchumi zaidi kuliko mira.(ng'ombe ishirini tena bei ya mnada Pugu jana ilikuwa ............)) utakoma.

    ReplyDelete
  40. Mdau uliyezungumzia theluji na snow, umesahau kuwa mlima Kilimanjaro una theluji? Umefika Kitulo Mbeya usikute theluji katika kipindi cha baridi?

    Kwa mantiki hiyo hiyo mahari yalikuwepo au yapo huko Ulaya.

    Kama wadau waliotangulia walivyosema kwani lazima tuige vya Ulaya?

    Na wewe mdau unayetoka povu mdomoni kwa kusema eti mahari ni utumwa wewe ni maamuma tu hujijui hujitambui hata mila na silka zako ni zipi.

    ReplyDelete
  41. kuna watu humu masafihi na jawabu ya safihi ni SKUT. Mtu akitoa povu la ugonjwa wa kifafa huwa hawajijuwi wanasema nini. Siku moja mtu mmoja nilimwambia jawabu ya safihi SKUT alinijibu SKUT mwenyewe nilicheka kweli, maana ya SKUT ni kunyamaza, sio tusi na safihi ni mtu jeuri.

    ReplyDelete
  42. wilson kasimbiMarch 21, 2012

    afrika na uhoro sidhani kama mambo haya yako europe "eti eshima kwa wazazi wa binti kwani mtoto wa kiume hakulelewa? hii ndo inapelekewa hata kunyanyaswa na kuendekeza mfumo dume "mambo gani haya?

    ReplyDelete
  43. Mdau wa Tue Mar 20, 12:56:00 PM 2012
    Mada iliyopo ni mahari na sio utumwa lakini madhali umegusia mengine nami nitoe yangu.Hatahivyo ni vyema ukasome historia ya utumwa wa Afrika mashariki vizuri.

    Kwa kukumbushia tu watumwa walikotwa kutoka bara Afrika ikiwemo Tanganyika na kufikishwa Zanzibar kwa mauzo na kutumikia mabwana zao ndani au nje ya nchi ya Zanzibar.

    Kumbuka tu historia ya wazanzibar ipo tokea enzi za biashara ya utumwa kutokea.Hakuna pahali inayoeleza kuwa wazanzibari walikamatwa na kuuzwa ndani ama nnje ya Zanzibar.

    Nakama wapo hao wanajaribu kujinasibu na kujilinda kwa nasaba ya uzanibari. Nani walikuwa au wilistahiki kuitwa watumwa jibu ushalipata.

    Ancle isinibanie please, kwani mdau hapo juu amechokoa binaadamu na sio pweza.

    ReplyDelete
  44. Kwanza nataka kusema point nzuri kwa ANONY. wa Tue Mar 20, 03:54:00 PM 2012 kuhusu Snow na Theluji. Nimeipenda.

    Mchango wangu ni kwamba siye WaAfrika kwa nini tunakimbilia kukashifu Magharibi wakati huo huo tunakimbilia dini? Je dini ndio utamaduni wetu? Kabla ya watu wa Ulaya na Waarabu kuja, dini za Kristo na Uislamu zilikuwa zetu?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...