Mwakilishi wa Jimbo la Bububu (CCM) Salum Amour Mtondoo (pichani) amefariki dunia katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja alipokuwa amelazwa. Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho aliwathibitishia waandishi wa habari juu ya kifo hicho na kusema kwamba kifo chake wamekipokea kwa huzuni kubwa.
Mtondoo ambaye alikuwa Mwakilishi kufuatia uchaguzi uliofanyika Octoba, 2010, alizaliwa tarehe 14/ 12/ 1962 huko Bububu , Wilaya ya Magharibi , Zanzibar ambapo alipata elimu yake ya msingi na Sekondari katika Skuli ya Bububu kuanzia mwaka 1969 hadi mwaka 1979.
Marehemu Mtondoo katika uhai wake aliwahi kufanyakazi ya Usimamizi wa Kiwanda cha COTEX mnano mwaka 1983 hadi mwaka 1985 na Baadae kufanyakazi za Ujenzi katika ushirika wa BBB 1986 hadi mwaka 1992. Mbali ya kazi hizo , Marehemu aliwahi kufanyakazi za biashara kuazia mwaka 1992 hadi mwaka 2010.
Aidha katika shughuli za kisiasa, Marehemu amewahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo mjumbe wa Kamati ya siasa ya Tawi na nafasi za ujumbe katika jumuiya ya Wazazi Wilaya hadi Mkoa.
Mheshimiwa Salum Mtondoo alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Bububu , kupitia Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Octoba, 2010.
Marehemu ameacha wake wawili (Vizuka) na watoto 10.
Tunamuomba Mwenyezimungu aijaalie familia ya Marehemu pamoja na wananchi wa Jimbo la Bububu, subira na utulivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Mwenyezimungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi.
Amin.
Chanzo: Zanzibar Yetu.
Chanzo: Zanzibar Yetu.
Poleni sana wafiwa wote kwa msiba huu. Inna Lillahi Wainna Ilayhi Rajiiun,
ReplyDeleteMarehemu alikuwa mstari wa mbele kukemea kashfa za watendaji na ubadhirifu unaofanywa. Pamoja na kuwa siku yake imefika, wadadisi wa mambo wanaweza kujiuliza kama kummwa kwake kunaweza kuhusishwa na waliomuona "mkorofi". Post moterm inahitajika