Profesa John Mbele akiwa baa. Anasema "Kwa siku kadhaa sasa, nikiwa katika kutumia dawa nilizoandikiwa na daktari, ni marufuku kukata ulabu. Badala yake, kinywaji changu ni maji tu. Nikikaa mahali, hata baa, kinywaji changu ni maji tu".
Kwa siku hizi ambazo nimekuwepo hapa Dar, nimekuwa nikitinga kwenye baa hii au ile, ingawa sinywi ulabu. Watu wengi hapa nchini wananifahamu kutokana na kuona taarifa zangu mtandaoni. Huko kwenye baa, wengine huambiwa na wenzao mimi ni nani.

Wadau wakishagundua kuwa mimi ni profesa, hupenda kuanzisha mijadala nami. Wanadadisi mambo mengi, yakiwemo yale ya Marekani. Nimejikuta nikilumbana na wadau wa aina aina, wakiwemo wale ambao wamelewa chakari. Ni burudani ya aina yake kuwashuhudia hao waliolewa chakari wakijibidisha kutema umombo ili ijulikane kuwa nao wamo.

Sasa, katika hizi siku zijazo, nataka kuanza kuwaambia hao marafiki zangu kuwa kwa kweli, mahali ambapo profesa anapaswa kuwepo ni maktabani, darasani, au sehemu ya utafiti wake. Anapaswa kuwa anatumia muda wake mwingi katika kusoma na kuandika makala na vitabu, si kukaa kaunta akitema cheche kwa wadau wa konyagi, Tusker, na Kilimanjaro za baridi.

Wadau kwenye baa hawatambui hilo. Hatari mojawapo ni kuwa watu wanadhani mtu kwa vile alishasoma sana na kumaliza shahada za vyuo, basi ameelimika kabisa na hahitaji wala kuwajibika zaidi ya pale. Wanaamini kuwa mtu aliyefikia cheo cha uprofesa amemaliza. Kwa hivyo hawaoni tatizo kuwa naye baa kila siku na kulumbana.

Kwa mtindo huu, Tanzania hatutafika. Tutashindwa kutoa mchango wa maana katika taaluma hapa ulimwenguni. Kiwango cha maprofesa kitaporomoka, kama hakijaporomoka tayari. Mimi mwenyewe, kwa siku chache hizi ambazo nimekuwa nikitinga baa badala ya kusoma vitabu na makala, najisikia kabisa kuwa nimedidimia kitaaluma kiasi fulani, kwa maana kwamba sijaandika lolote la maana kwa siku hizi kadhaa, wala sijasoma kitabu na makala katika taaluma yangu. Mihandara na malumbano yangu yote yamehamia baa. Nikiendelea namna hii kwa miezi au miaka, nitadidimia zaidi, ingawa bado wadau mitaani na kwenye baa wataendelea kuniona ni profesa maarufu. Hili ndilo tatizo la Tanzania. Kwa mtindo huu hatutafika kabisa.

Sio vibaya kwa profesa kuingia baa mara moja moja na kupata moja baridi. Lakini kukaa masaa humo baa, mara kwa mara, au kila siku, ni balaa tupu, wala tusidanganyane. Vile vile, kwa sisi tunaotafiti masuala ya jamii, baa panaweza kuwa sehemu moja muhimu ya kutafiti na kujifunza mengi. Ila, nadhani ili kufanikisha hilo, na kwa vile sisi ni waelimishaji, tunaopaswa kuwa mfano, tusiwe tunakata ulabu kama wadau wengine. Bia moja mbili sio mbaya.



Chanzo: HAPA KWETU

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. Prof, just enjoy it, si kwamba utafanya hivyo kila siku. Na isitoshe unakunywa maji tu. Kwa nini usiandae mjadala rasmi sehemu ya heshima? Hapo utajifunza mengi mbali na kuchangia.

    Ila unalosema ni kweli japo si kwa maprofesa au wanataaluma tu bali watu wote. Si vema kutumia muda mwingi sana baa, ni bora hata ukae tu na familia yako nyumbani muangalie vichekesho kwenye TV au uwasaidie watoto na shule.

    Kuna watu kila wakitoka kazini wanaenda moja kwa moja baa, siku za mwisho wa wiki wanaanzia baa asubuhi hadi baa inafungwa.

    Prof, huwa nakuhurumia sana watu wanapokushambulia kwani najua huwa huna ubaya nao ndani yako. Wakitaka wasome wakitaka waache.

    ReplyDelete
  2. Inasikitisha Kuona professa anajigamba namna hii! Anaongelea hapendi malumbano ila tayari hapa anatafuta malumbano sasa ila uzuri wa huyu Professa anahimiza sana watu kusoma. KWANI ALIYESOMA AKAWA HASOMI VITABU NA KUJIENDELEZA HUWA HANATOFAUTI NA ASIYEJUWA KUSOMA KWA MAONI YANGU. PANDU

    ReplyDelete
  3. Kuwachambua kama karanga hao unaowaita rafiki zako wa baa sio ustaarabu hata kidogo. Unapokaa na watu jichanganye tu, sio kwa vile wewe ni prof. wa vitabu basi unawaona wengine wote hamnazo. Kuna wakati wa kazi, wakati wa familia na wakati wa burudani, Sio kila wakati unaprofess tu. Na kila mtu ni prof. kwenye anga zake, hivyo acha kuwabugudhi watu kwa uprof. wako! Na sio kweli kuwa kila aliye bar analewa, wewe ulilewa kwa kunywa hayo maji? Na ni hao hao walevi wanaokunywa soda pia, au haziuzwi hapo bar?

    ReplyDelete
  4. WaTZ wanatakiwa kuanza kufanya mambo kwa vitendo. Uvumbuzi ni muhimu sasa sio kusoma vitabu vya nadharia. Tuchukue uvumbuzi ulikwisha fanywa na wengine ili tujiendeleze kwa vitendo. Mmasai tangu babu wa babu ng'ombe ni hao hao wakati sasa kuna magombe yanatoa maziwa na nyama kwa wingi, ng'ombe mmoja wa kisasa anatoa maziwa sawa na ng'ombe kumi wa mmasai. Vitabu vya Grammer na history havitusaidii sasa.

    ReplyDelete
  5. Mdau Kweli Tunasoma Vitavu vya History ndomana mashuleni watoto wakifika juu wanachelewa kuelewa shule za Kata, Shule za kata zinatakiwa kubadili mfumo wa masomo tizama wanayosoma ndio hayo wanakuja kukutana nayo sekondary ila kutoka Kiswahili kuwa English na hasa masomo ya Historia ni uzushi mtupu.

    ReplyDelete
  6. Mdau wa Machi 30, 11:30am unayesema ninawachambua wadau wa baa, samahani kama nimekukera. Nilidhani ninawachambua zaidi ya hao, tena zaidi maprofesa waliohamia baa, nikijikumbusha pia mimi mwenyewe wajibu wangu. Katika haya mazingira ya Tanznia, ni rahisi watu kujisahau, na naamini tumejisahau. Siamini kama uchambuzi wangu umeegemea upande moja. Naamini nimetoa angalizo muhimu kwa jamii yetu. Amani iwe kwako.

    ReplyDelete
  7. Pole Prof. John Mbele kwa kuumwa!

    Isipokuwa unajigharimu wewe mwenyewe kwa kukaa Bar wakati umeshauriwa usinywe muda huu wa Dozi !

    Kukaa kwako Bar kunaweza kukutamanisha na 'Masanga' halafu ukaanza kuzichapa kama kawaida !

    ReplyDelete
  8. usiuseme tu umeanza kuwa mlevi,maoni yako hayeendi na wakati,hao wanaokuja baa sio wote walevi,ni sehemu za makutano pia za biashara na mengineyo,maprofesa bwana wanadhani wao ndio zaidi,kila mtu ni profesa ktk anga yake.Natoa hoja

    ReplyDelete
  9. mimi mwenyewe proffesor,sema vitu vishanasa kichwani na havitoki,hata nilale bar

    ReplyDelete
  10. usituletee habari ya mangombe wa ajabu wewe hao ngombe wa mmasai ndio tunataka sisi sio hao wa kisasa magonjwa matupu wazungu wenyewe wanachukua mbegu ya ngombe wa mmasai kwenda kuwazalisha kwao nakupata maziwa halisi kuna maziwa yanaitwa amasai marekani na ni ghali kweli kwa sababu ya uhalisi wake. kwenye maswala ya vyakula tuacheni na ushamba wetu ongeleeni vitu vingine.

    ReplyDelete
  11. Huyu jamaa jina lake anaitwa Joseph Mbele na sio John (ninacho maanisha jina la kwanza SI SAHIHI tafadhali fanya marekebisho)

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...