.Mkuu wa Mkoa wa Manyara Erasto Mbwiro akifungua mkutano wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoani Manyara leo.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,Mwanaidi Mtanda akitoa salaam za Bodi kwa wadau wa Mfuko katika Mkutano uliofanyika Mkoani Manyara leo.
Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji, Deusdedit Rutazaa akitoa mada kwa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoani Manyara leo.
Wadau wa NHIF mkoani Manyara wakifuatilia mada katika mkutano wa siku ya wadau.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,Hamisi Mdee na Mjumbe wa Bodi Mwanaidi Mtanda wakiwa na wadau wakifuatilia mada.
Wagonjwa wakiwa wamefunikwa mashuka yaliyotolewa na NHIF katika Hospitali ya Maunt Meru,Arusha muda mfupi baada ya kutolewa kwa msaada huo.

Na Mwandishi Wetu, Manyara

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema hauna jukumu la kusambaza dawa na hauwezi kuingilia majukumu ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hivyo ukavitaka vituo kutumia fedha zitokanazo na vyanzo vingine kununulia dawa ili kuziba pengo lililopo.

Umesema kuwa endapo fedha zitokanazo na Mifuko ya NHIF, CHF na fedha za papo kwa papo zitasimamiwa vyema na kutumiwa katika ununuzi wa dawa, tatizo la ukosefu wa dawa vituoni litapungua na kuondoa malalamiko kwa wananchi.

Akijibu maswali ya wadau wa NHIF, Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji, Deusdedit Rutazaa mkoani Manyara ambao walielekeza lawama kwa Mfuko huo hasa katika suala la ukosefu wa dawa vituoni na kutaka kujua ni namna gani Mfuko huo utamaliza tatizo hilo.

"Jamani Mfuko wetu hauna jukumu la kusambaza dawa na hatuwezi kuingilia kamwe majukumu ya MSD, ila tunachowashauri ni kutumia vizuri fedha za vyanzo vingine kununulia dawa wakati kunapoonekana upungufu wa dawa kutoka MSD," alisisitiza Rutazaa.

Aidha Rutazaa alisema kuwa mchango mkubwa unaofanywa na NHIF katika kuhakikisha huduma za matibabu zinakuwa bora ni utoaji wa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ambayo itaviwezesha vituo kuboresha huduma zake ambazo zitakuwa ni kwa wananchi wote na si kwa wanachama peke yake.

"Lengo letu kubwa ni kuboresha huduma za afya ili hatimaye kauli mbiu yetu ya Huduma bora vijijini na afya kwa wote ionekane kwa vitendo na kulitimiza hilo ndio maana tunatoa fursa kama hizo za mikopo na kuzihimiza hospitali kuwa na maduka ya dawa ili wanachama na wananchi wasiondoke hospitali bila ya kuwa na dawa lakini viongozi hasa madiwani tusaidieni kusimamia fedha hizi zinazotokana na mifuko hii ili zitumike kuboresha na kupunguza matatizo kama ya dawa," alisema Rutazaa.

Wadau hao wakichangia mada zilizowasilishwa na viongozi wa NHIF, walisema kuwa moja ya mambo yanayokwamisha wananchi kujiunga na CHF ni ukosefu wa dawa na huduma mbovu vituoni ambapo walishauri kuwa wakati uhamasishaji ukiendelea ni vyema na matatizo hayo yakashughulikiwa ili wananchi wawe na imani zaidi.

Pamoja na kuonekana kuwepo kwa changamoto zinazokwamisha suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bw. Erasto Mbwiro wakati akifungua mkutano huo wa wadau, alizitaka Halmashauri kujipanga na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo lakini pia kuweka sheria itakayowalazimisha wananchi kujiunga na CHF.

"Halmashauri jipangeni, uboreshaji wa huduma ndio utakaowavutia wananchi kujiunga na Mfuko huu na kwa Mikoa ambayo imeweza kutumia vyema fedha za CHF imefanikiwa sana na tatizo la dawa hakuna...angalieni hilo na mlifanyie kazi ili wananchi wetu wawe na uhakika wa matibabu," alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...