Haya mambo ya kupiga disko mahali pa makazi mpaka asubuhi yamekuwa yakitokea siku hadi siku. Ya leo ni funga mizigo na nimeshindwa kuvumilia! Haya yametokea TUNGI- KIGAMBONI!

Natoka kazini yapata saa 1:30 jioni mara nasikia ngurumo za spika zilizoshiba, nauliza naambiwa kwa jirani kuna harusi. Siulizi zaidi kwani nasikia mwenyewe kupitia kwa mshehereshaji, MC. Ni nyumba ya tatu kutoka nyumbani kwangu. Heko, jirani hongera.

Navuta subira nikidhani ikifika saa 6:00 usiku basi sherehe itakuwa imekwisha kama utaratibu ninaoufahamu. Lakini kutokana na maneno ya mshehereshaji inaonyesha ngoma si ya kitoto, inakesha hii! Mida ya saa 5 usiku nasogea karibu na eneo la tukio na kujionea watu wanaondoka watu wanaingia. Shughuli ilikuwa inafanyika nje, eneo la wazi.

Namwita kijana ninayemfahamu na kumuomba aniitie mwenye nyumba. Naitiwa mwana mama wa kiislamu amejiremba kapendeza mwenyewe kama mnavyojua wanawake hawa wanavyojipenda wakati wa shughuli. Sherehe ilikuwa ni harusi ya kiislam. Mwana mama huyu anaamua ‘kunipotezea’ labda kwa sababu ya mambo mengi ya shughuli.

Mara naona anatoka na baadhi ya wageni, nasikia wanaaga kwamba watakuja muda si mrefu, wanaenda sehemu karibu kufanya jambo fulani. Nawakimbilia, naomba samahani na kumuita mwenye shughuli kutaka kuongea naye.

Samahani dada mimi ni jirani yako, kwanza hongera kwa shughuli, naomba kuuliza shughuli mnamaliza saa ngapi? Nauliza.

Najibiwa, ‘asante, shughuli tunamaliza asubuhi’.

Eh! nashangaa; Je mnadhani mnalolifanya ni sahihi? Naomba niwashauri kama jirani mwema, kwanza ni kinyume na taratibu kufanya shughuli zinazohusisha mziki mkubwa kama huu majumbani lakini kutokana na maisha yetu huwa inaruhusiwa lakini inabidi mwisho uwe saa 6:00 usiku. Pili natumaini wewe ni mzazi ona watu walioko kwenye mjumuiko huu wapo hata watoto ambao inabidi asubuhi waende shule, na zaidi ya hayo majumbani kuna watu wenye hali tofauti wakiwemo wagonjwa ambao wangehitaji kupumzika.

‘Kwanza kabla ya kufanya sherehe majirani wote wanafahamu’, namjibu mimi sifahamu na ni jirani.’ Anajibu, labda wewe’.

‘Pili mimi ninakibali kutoka kwa mjumbe, nakala kwa mtendaji na polisi. Eh! Nashangaa. Nashindwa kujizuia na kusema basi wewe huna kosa, mimi nitaenda kwa mjumbe na kumuuliza kama huu ndio utaratibu. Miongoni mwa wasindikizaji mmoja ni mjumbe lakini kutoka eneo jingine. Ananifahamisha kwamba yeye ni mjumbe kwa miaka mitatu sasa na huwa wanatoa vibali vya sherehe kukesha! Nauliza jina la mjumbe aliyetoa kibali wanakataa kumtaja.

Nahisi watu kunipuuza kwani wana kibali. Nashauriwa kwamba tuvumiliane kama jirani na kama nina matatizo binafsi, mfano nina mgonjwa basi iwe hoja binafsi lakini hoja ya taratibu haina nafasi kwani wanafanya sherehe kwa taratibu zote.

Nauliza swali la mwisho; mbona maharusi wameondoka sasa kwanini kukesha? Hili halionekani swali la msingi. Asanteni; nikaondoka na wao hao wanaenda wanakopaswa kwenda. Nyuma yangu nawaacha vijana wa rika mbalimbali lakini nawaangalia kwa makini watoto wadogo wanafunzi wakifurahia kiduku wakipokezana na mama zao wakicheza mduara.

Naingia ndani nachukua simu natafuta simu ya mtendaji wa eneo langu maajabu siioni; ‘siku za kufa nyani hizi’. Kuna mtendaji mwingine eneo jirani, ninafahamiana naye na nina namba yake ya simu. Nampigia na kumueleza mkasa huku mziki ukiendelea ‘kutuburudisha’ mimi na familia yangu kutoka nje.

Majibu ni kwamba hayo yote ya kwangu ni sawa na ndio inavyotakiwa ila kwa taratibu za serikali za mitaa, baraza la madiwani wanapewa mamlaka ya kupitisha sheria ndogo ndogo za maeneo yao. Ni madiwani hawa hawa ambao wanaruhusu kitu hicho kwani ni jambo ambalo wapiga kura wao ‘wanapenda’. Nikahakikishiwa kwamba suala la kupewa vibali vya kukesha lipo na ni kweli watu wanapewa hivyo vibali. Hivyo ni busara tu ya mtendaji kukataa sherehe kukesha lakini akitaka ‘taratibu zinamruhusu’.

Nikakubaliana na matokeo kutokana na ushahidi niliokusanya. Basi nikaamua kwamba nitamuuliza mbunge wangu ambaye naye anashiriki vikao vya madiwani katika jimbo lake kuhusiana na haya. Ikabaki ‘adui muombee njaa’, ikiwa na maana TANESCO waingilie kati. Sala yangu ikafanikiwa kwa kiasi fulani, umeme unakatika na kurudi kwa vipindi vipindi kama mnavyojua hali ya umeme nchini. Lakini wapi, jamaa walikuwa wamejipanga, walikuwa na jenereta. Kutokatisha burudani wakaamua kuachana na TANESCO na kuendelea na jenereta kwenda mbele.

Haya yote kuanzia majadiliano na mwenye shughuli mpaka naanza kuandika taarifa hii yanatokea kuanzia saa 5:00 na saa 6:00 usiku. Kuanzia saa 6:05 hali ya umeme inatengamaa lakini maajabu saa 6:10 nasikia mshehereshaji, MC anatangaza kwamba wanaomba radhi kumetokea mabadiliko watapiga nyimbo tatu za mwisho na watu waende nyumbani. Saa 6:30 usiku mziki unazimwa kabisa na siusikii tena. Swali ni kwanini wamebadilisha mpango wao? 

Au wamewasiliana na mjumbe ambaye amekuwa na wasiwasi na ‘huyu jamaa’ mwenye kujiamini na kutaka kumjua kwa yeye kutoa kibali cha kukesha? Maskini angejua ‘jamaa’ mwenyewe ashakubali matokeo yuko anakosa usingizi akiandika kuwapasha habari watanzania wenzake jinsi jamii zinavyoishi isivyo na viongozi husika wasivyotumia busara katika kuongoza kwao.

Tafakari- kwa maisha haya hatufiki! Tubadilike, tulee jamii zitakazoweza kupambana na changamoto za maendeleo ya ulimwengu wa sasa. Je,kwa mpango huu wa watoto kucheza kiduku mpaka asubuhi kweli tutaweza kushindana hata kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki achilia mbali ulimwenguni?

Mungu na atubariki!

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 36 mpaka sasa

  1. "mama wa kiislamu na shughuli ya kiislamu" get over it man.....umeona story yako haitakuwa na ushabiki usipotaja uislamu?? kwa nn usiseme tu jirani yako alikuwa na shughuli then ukaendelea......wenye mabaa na virabu vya pombe vilivyojengwa karibu na makazi ya watu wakiwemo waislamu na miziki na vujo za pombe zinafanywa kila siku mbona hujasikia muislamu akisema hawa wakristu wanafanya sherehe zao za kilevi za kikristu??

    Lengo lako ni kuonesha kuwa jamii hiyo ambao wengi ni waislamu ndo wanatabia chafu.....acha uzushi hao ni wenyeji wa maeneo hayo na hapo ndipo kwao hivyo mila na desturi zao wanafanya hapohapo. kwa kifupi hapo ndo kijijini kwao kama wewe unavyokwenda bukoba kunywa lubisi na kupiga katerero au mchaga anapokwenda uchagani kunywa mbege....so kama unaona tamaduni zao hazikufai hama nenda huko kwenu kwenye mila za kistaarabu pengine kijijini unapotoka ndo ushenzini kuliko.
    acha ujinga next time jifunze jinsi ya kupresent topic usilete kujifanya umetoka jamii iliyostaarabika while in fact we ni bogus tu (kutokana na maelezo yako)

    ReplyDelete
  2. Ndugu yangu kama una kauwezo kidogo, basi nakushauri uhamie ULAYA (1st world countries)

    Africa HAKUNA SHERIA baba! In short in kwamba people are NOT CIVILIZED.
    Hivyo uvumilie tu hizo SHIDA au ukubali UGOMVI na watu kila siku.

    ReplyDelete
  3. Inasikitisha kwa kweli, pole sana! Ila kwa vile ni kitu ambacho kitajirudia tena mimi naona ni vema kumfahamu huyo "mjumbe" na kumueleza maoni yako na hata mbunge wako pia pengine wewe ndio ukawa chanzo cha kuleta mabadiliko ktk jamii hiyo inayokuzunguka na nchini kwa ujumla.

    ReplyDelete
  4. We mdau umewatibulia watu starehe zao, watakutupia jini bahari, subiri tu.

    ReplyDelete
  5. acha wivu hiyo ndo africa

    ReplyDelete
  6. Maoni ni mazuri na yanafaa kuwasilishwa kwa mjadala. Ila suala la 'Kiislamu' hapa linaingiaje? Naomba maoni zaidi.ephpPri precussi

    ReplyDelete
  7. Maelezo ya mlalamikaji ni sahihi lakini kuna kitu kimejificha ndani ya moyo wake.Sijui kwa nini amehusisha muziki na sherehe ya Kiislam wakati akijua kuwa Muziki kwa waislam ni haramu ila kwa wakristo ni halali.Anayepiga muziki mchukulie yeye kama binadamu mwingine hata kama wenye sherehe ni waislamu.Mtazamo wa maelezo yake anaonekana ni Mkristo na ana chuki zaidi ya muziki.Kwa nini asiwe na taarifa ya shughuli ya jirani yake wakati wenzake taarifa wanayo? Huyu hana ushirikiano na majirani zake. Mwisho napenda kumfahamisha kuwa muziki pia ni kero kwa waislamu tena ni haramu.Acha chuki tetea haki utapata haki.

    ReplyDelete
  8. pole sana mdau,ila hizi tabia za kishenzi wanazileta hao wanaoitwa wajumbe,paada ya kupewa rushwa,na kuogopa kupoteza kura,hii nchi inahitaji jeshi angalau mwaka mmoja watu tunyooke.

    ReplyDelete
  9. ahh una yako kwanaza mida uliyoandika na matendo yalivyokuwa na unavyohadithia ni kama chumvi nyingii. Maadili ya watoto tumewaachia mahausegal watulelee

    ReplyDelete
  10. Bongo Bull Crap ndo maana nilijiondokeaga long time niko zangu hapa nikishuhudia marais wanne wa marekani wakitawala. Inabidi uhamie Masaki kaka maana kule kinje alikuwaga anapiga muziki kwenye Bar yake lakini sasa hivi the rest is history
    Mdau mchana Boxxi lakini anaishi vizuri

    ReplyDelete
  11. Mkuu kwanza nakupa pole kwa masumbuko uliyopata,mimi binafsi napenda mziki na napenda mziki wa sauti kubwa ila nazingatia hali ya mazingira niliyopo kama simsumbui mtu mwengine kwa starehe yangu.Mkuu kila ulilosema mimi nakubaliana nalo 100% kuna umuhimu wa wazazi kubadilika kitabia. Ila sijakubaliana pale uliposema kuwa sherehe ilikuwa ya Kiislamu, kwani uislamu hauruhusu kucheza muziki ni kazi za shetani hizo, japo mimi pia ni mpenzi wa muziki ila kwa matamanio yangu sio kidini. Mkuu hapa najaribu kuutetea Uislamu ambao unapakwa matope. Pili,uliposema mama wa kiislamu ambao huwa wanajipamba wakati wa harusi tu, hio ni kashfa kwa wanawake wa Kiislamu, kwani wapo wanaojipenda kila na wapo ambao wana dini tofauti na hawajipendezeshi. Mkuu naomba msamaha kama nimekosea ni katika kueleweshana tu, nipo pamoja nawe katika ujenzi wa familia bora na jamii njema.

    ReplyDelete
  12. Siyo "msheHEREshaji" bali ni "msheREHEshaji". neno hilo likiwa limetokana na mzizi mkuu wa neno "SHEREHE".

    ReplyDelete
  13. Siyo "msheHEREshaji" bali ni "msheREHEshaji". neno hilo likiwa limetokana na mzizi mkuu wa neno "SHEREHE".

    ReplyDelete
  14. Yako ya harusi madogo maana ni siku moja tu.

    Hapa kwetu kuna disko karibu kila weekend na muziki unakwenda mpaka nane au tisa za usiku.

    ReplyDelete
  15. mdau nakupa heko, hili suala ni kero sn. na km unaishi uswahilini kwa matola kila wkend kuna shughuligy

    ReplyDelete
  16. hana jipya huyo kafata demu kwenye mdundiko kamkuta yupo na jamaa mwingine kaona kuingiza uislamu,ama kweli ujinga hauna kwao

    ReplyDelete
  17. Unajua ujumbe uko poa but ume offend Islamic Religous, mfano hapa marekani ukiongelea magaidi husemi islamic terrorist but unasema arabic terrorist maana ume generalize sana na umekua bias na hawa ndugu zetu waislam, mfano mwingine ule unasema kuna wamasai wanne na abiria kumi???That is nothing but discrimination na next time utajuta watakusomea albadili. Kaka umeandika kwa jaziba na kwa kiasi fulani umechafua hali ya hewa. Next time ikitokea kitu kama hiyo jaribu kutulia kwanza au kula chakula cha usiku na mkeo upunguze hasira.
    Ni hayo tu

    ReplyDelete
  18. huyu ana lake jambo (chuki dhidi ya uislam kwa kifupi) ingawa hoja yake ni ya msingi ila imejieleza zaidi kuwa ni mtu flani mdini sana..hatufai hata iweje,,sijampenda.take your time kama vipi njoo masaki..ostabei au nenda sehemuyoyote unayojua imetulia sio unang'ang'ania manzese halafu unajifanya kuujua ustaarabu

    ReplyDelete
  19. Hoja yako inapoteza malengo kwa kuingiza chuki zako binafsi za udini. Ulilolisema linaingia akilini lakini kwa sababu ya udini ujumbe wako unakosa dira.
    Ujue baa zote zinapiga makelele mpaka asubuhi maeneo ya makazi zinamilikiwa na woe waislam na wakristo. mimi napokaa jirani yangu ni kanisa siku wakiamua kukesha balaa kwa asiekuwa muumini wao. acha udini jenga hoja kwa msingi wa hoja yenyewe.

    ReplyDelete
  20. Hili ndio tatizo la kuhamia maeneo ya watu halafu mkataka kubadilisha mambo mtapewa majini si saizi yenu.kwa hayo maeneo watu hio ndio kawaida kama wewe unaona huiwezi bora ata ukimbilie kwengine maana ukitaka kubadilisha utajtafutia balaa na kupewa jini lisilozema bure. Bila shaka katika hayo maeneo wewe ni mkuja.

    ReplyDelete
  21. Konyagi 7 times.March 25, 2012

    Mtoto wa kiume unarudi nyumbani saa moja...hahaha! neno hiyo...wacha pata fresh ya shamba...unahitaji mzinga wa konyagi...au kuna kiuno umekipenda hapo jirani...YAANI NDEMBE NDEMBE...mambo ya pwani hayo tuachie MABAHARIA.

    ReplyDelete
  22. Mdini Huyo umeshindwa kuelezea tukio mpaka utaje dini?

    ReplyDelete
  23. MIMI NIMEAMUA KUANDIKA KWA HERUFI KUBWA ILI ISIRUDIE TENA KUWABUGHUDHI WATU NAMILA ZAKO, HILO ENEO LA TUNGI KIGAMBONI NALIFAHAMU SANA, WENYEJI WANA MILA NADESTURI ZAO NA WANAPENDA KUDUMISHA UTAMADUNIWAO TOKA MIAKA MINGI, WEWE NI MUHAMIAJI TU NA KIBAYA ZAIDI UMEJENGA AU UMEPANGA NYUMBA AMBAYO KIWANJA CHAKE NI CHA KIENYEJI.

    KWA KUANZA NA WEWE BINAFSI, WEWE NI MDINI TENA UNACHUKI MBAYA SANA NA UISLAMU NA MBAGUZI HUFAI HATA KUONGOZA KUNDI LA KUKU, UISLAMU HAPO UNAINGIAJE NA MZIKI, HIYO SHEREHE KATIKA MILA ZA KIISLAMU NI HARAMU, HAPO HUNA CHEMBE YA POINT ILA RELIGION DISCRMINATION NDIO IMEKUJAA.

    MWAFRIKA AKIPATA VIJIHELA NA POSITION KIDOGO TU SEHEMU FULANI ANAJIFANYA ETI YEYE NDIO MUHIMU, INAONYESHA WEWE NI MTU MWENYE ROHO MBAYA NA HUELEWANI NA JIRANI ZAKO. RUDI KWENU ULIPOTOKA KUNA MAENEO MAKUBWA AMBAYO NI KIMYA ILA SAUTI ZA FISI NDIO ZITAKUFANYA USILALE, KILA KABILA LINA USTAARABU WAKE, NDOA NI KITU KITOKEACHO MARA CHACHE KWA MWANADAMU WEWE UNALETA KUJUA, MIMI NAFIKIRI WEWE UNATOKA USHENZINI KULIKO HAO UNAOWAITA WASHENZI. HUWEZI KUISHI NAO RUDI KWENU UKATEMBEE KWENYE UDONGO MWEKUNDU ACHA MCHANGA WA PWANI MWEUPE NA WATU WAKE.

    DO NOT IMPLEMENT YOUR BELIEVES INTO OTHERS, IF YOU HAVE MONEY JUST LEAVE THE PLACE. TUNGI NI DUNIA MSONGAMANO, KWA TABIA ZAKO CHAFU HATA MAJIRANI WALISHINDWA KUKUPA TAARIFA, SASA NA WEWE SUBIRI UFIWE UONE MAJIRANI WATAKWAMBIA NINI, MSIBA MWISHO SAA 4 USIKU. JE UTAKUWA RADHI? ACHA UJINGA. USIKU MMOJA UTAKUATHIRI NINI WEWE NA CHUKI ZAKO ZA UDINI. PWANI WENYE HASA WAISLAMU WEWE UMEKUJA KUFANYA NINI? TENA SEHEMU YENYEWE TUNGI.

    NI MARA NGAPI KUMEKUWA KUNAPIGWA DISCO MIKADI, NG'ODA, CHADIBWA BEACHES MBONA HUJALALAMIKA? ETI UNAJIFANYA KUFUATILIA, NILICHOKUPENDEA KATIKA MAKALA YAKO HUKUFICHA ROHO MBAYA ULIYO NAYO PALE ULIPOSEMA ''UMEME ULIKATIKA'' NAWE UKAFURAHI, WAZI KABISA UNAONEKANA UNA CHUKI NA MAJIRANI ZAKO.

    NAPENDA KUKUFAHAMISHA HAO UNAOWAITA WAISLAMU, NI WAVUMILIVU SANA, KAMA UTAFUATILI SANA VILABU VYA POMBE VINGI VIPO MAENEO YA WATU, MBONA HUJASIKIA WAISLAMU WAKISEMA ''WAKRITO'' WANAFANYA FUJO? HEBU GEUZA KICHWA CHAKO NA UNAMBIE NI MAKANISA MANGAPI YA WALOKOLE KIGAMBONI YAPO MAENEO YA KUISHI WATU, NA WAO HUKESHA NA KUOMBA USIKU KUCHA KWA SAUTI NA KULIA NA WAKATI MWENGINE WAKIWA NA WATOTO (WANAFUNZI) MBONA HILO HUJALISEMA NA KUFUATILIA KWA MJUMBE?

    MIMI NAKUONYA WACHA UJINGA NA CHUKI ISHI NA MAJIRANI ZAKO KWA AMANI, UKITAKA KUONA NANI ANAVUNJA SHERIA UTAMALIZA NCHI NZIMA, UNA BAHATI SANA WEWE KAMA INGEKUWA SHEREHE YA WAISLAMU NA UNGEANZA HUO USHENZI WAKO MIMI NAFIKIRI HIVI SASA UNGESHAKUWA UMEHAMA HAPO TUNGI, ACHA TABIA HIYO MBAYA YA KUFUATILIA NA KUWAKOSOA WATU KWA BELIEVE ZAKO.
    MDAU.

    ReplyDelete
  24. Acha chuki za udini, tudumishe mila zetu.

    ReplyDelete
  25. Annoy wa kwanza na wengine amnbao mmemshambulia mtoa ujumbe kwamba ni "mdini" nadhani hamkumtendea haki. Annony wa kwanza umesisitiza umuhimu wa mtu kuwa mstaarabu lakini yeye mwenyewe umeonesha kiwango cha juu kabisa cha kukosa ustaarabu na ameonesha kwa kiwango cha juu kabisa kuwa ni mdini tena mkabila.... Kulikuwa n haja gani ya kutumia maneno "ushenzi", mara sijui nenda kwenu huko Bukoba ukanywe lubisi na kupiga katerero? Wewe ndio mdini na mkabila na inaonekana una chuki ya dhati dhidi ya Wahaya na Wachaga (ambao kimsingi wengi wao ni Wakristo) na hivyo una chuki ya moja kwa moja na Wakristo... Ni kweli kabisa mtoa ujumbe angeweza kusema tu kulikuwa na "harusi" bila ya kusema "harusi ya kiislamu" na ujumbe ungefika... Lakini pia embu tujiulize, kwa kusema kulikuwa na "harusi ya kiislamu" je mtoa ujumbe alikosea? Mimi sioni kosa lolote hapo...nadhani alikuwa anaelezea hali halisi... Ni kweli kabisa siku hizi hapa Tanzania tumekuwa ni watu tunaopenda sana kuambiwa uongo na tunakuwa wepesi wa kuukubali uongo badala ya ukweli... Mimi naamini kabisa mtoa ujumbe amesema ukweli wa kitu kilichotokea, sasa "wapenda udini na ukabila ndani yake"wanaibuka na kumshambulia kuwa eti yeye ni "mdini"....INASIKITISHA

    ReplyDelete
  26. mimi binafsi sio muislam.ila alichofanya jamaa sio fair (kachafua hali ya hewa).
    amewafanya wadau badala ya kuchangia mada waanze kumlaani!
    huwa tunawasema tu waislam wakali kumbe muda mwingine wanachokozwa...!

    ReplyDelete
  27. Mzee umechemka. Na chuki zako kwa uislamu,I don't think you have right kuuhusisha uislamu dini ya mwenyezi mungu na upuuzi huo,Tatizo Lakota unachuki binafsi na uislamu ndio maana hata Hao jirani zako hupatani nao kwasababu unawaangalia kwa jicho la chuki come over man Kama hutaki kukutana au kumuona muislam tafuta maeneo ambayo hawapo so that you will have peace of mind,otherwise Kama unakaa na jirani wa mchiriku itabidi utafute njia nzuri ya kumuelewesha and not for her religion.

    ReplyDelete
  28. Harusi ni kitu cha siku moja, kuvumilia usingizi wa usiku mmoja nadhani sio issue. Mwenye hoja naona una sababu nyingine, aidha wivu ama roho ya korosho aka roho ya kwa nini!!!

    Usiwe na choyo ya ubinadamu, mbona kuna mabaa ilala, manzese, mwenge yanachapa muziki kwenda mbele na yapo katika makazi ya watu, tena ni kila siku na weekend ndio inakuwa full kigongo lakini hakuna mtu analalamika kihivyo!?

    Wewe harusi ya siku moja unaivalia njuga na unaona kuna tatizo kubwa!?!? Nahisi dhumuni la ujumbe wako ni kuponda dini zaidi kuliko issue nyingine.

    Afrika bado tuna ubinadamu na tunajali majirani wanapokuwa aidha na sherehe ama kilio. Wewe unaona ni usumbufu sasa??

    Kila kabila lina sherehe zake, kuanzia mtoto kuzaliwa hadi unyago, na asilimia kubwa zinasindikizwa na ngoma hadi mtondogoo, je hizo hazikupi kichefuchefu!?!?

    Tuache kuiga tamaduni za wengine na kujisahau tulipotoka. Sherehe sio kwamba kila siku zinakuwepo, hivyo watu wanapojimwaga kwa usiku huo mmoja sio big deal.

    Grow up and value your roots and culture!!!

    ReplyDelete
  29. Kaka sijapenda ulivyowasilisha mada yako, jambo ulilolalamikia ni kero lakini mwenzetu naona una chuki binafsi kwa wenzetu wa kiislamu. Mpaka kufikia kumtusi jirani yako hajipendi mpaka awe na sherehe it's unfair. Jenga ujirani mwema wewe pamoja na mkeo mtaishi kwa maelewano mtaani. Kama vipi hamia kwetu Sinza huku ni kelele za mabar. Utazoea tu bro

    Julius.M

    ReplyDelete
  30. Kwa kweli WENYEJI asili wa Dar na vitongoji vyake wameshaporwa ardhi zao, itikadi zao, na sasa hata mila zao na waliovamia toka Magu, Sengerema, Chato, Katavi, Uyui, Machame nk...... yaani upcountry Tanzanians wameigubika Dar kabisa..... Mimi kama mzawa wa pwani huwa ninakerwa mno na kujikuta tabia za bara hasa za kufungua mabar ovyo kila kona na kupiga madisko kwenye bar usiku kucha zilivyoshamiri kila siku!!! Hiyo ya ngoma au mziki usiku kucha siku ya harusi, ni mila halisi ya watu wa pwani!
    Waislam kwa Wakristo.... Inaitwa CHESHA...
    Kigamboni pailkuwa na bado wapo "wenyeji" and so is Kariakor, Kinondoni Tandika Magomeni etc... It is therefore their God given right kufurahia na kujisherehesha kama mila zao zinavyotaka...
    Chesha ni part of that na wanayohaki kucheza ngoma zao "mpaka LIYAMBA" kaka...
    So my friend, you just have to live with it au kama mdau wa mwanzo alivyosema, rudi ukacheze katerero kwenu....

    ReplyDelete
  31. Acha chuki na uislamu. Hili ni tatizo la watu wanaojifanya wazungu waswahili lakini wametokea mbali kwao bara hivyo kuwaona wenyeji wa Pwani ni waislamu na watu duni. Hoja zako zingekuwa na mashiko kama usingeweka chuki dhidi ya uislamu lakini imepoteza maana kabisa.

    ReplyDelete
  32. What islamic religion has to do with this? c'mmon man...get life, leave your neighbors alone. Hoja yako ni ya msingi isipokuwa the fact that unamdhalilisha mwanamke wa dini moja, sijui imani yako ya dini, lakini dini ya muhusika haina lolote na hoja uliyoijenga....huu ukweli ni ustaarabu? Ustaarabu anafanyiwa mstaarabu, ni mtazamo tu.

    ReplyDelete
  33. Huna mpya wewe mlalamikaji umejaa udini mabaa na madisko yanayopigwa miziki usiku kucha kila week end huwa wote ni waisalamu pia unalo hilo waislamu utawaona hiviviwacha uchochezi

    ReplyDelete
  34. Yaani kaka nakupa pole, na nashkuru umeweza kuwasilisha mada kwa ufanisi mkubwa kwani umeweza kutuwakilisha wa bongo wengi tunaopata tatz kama hilo ktk maeneo tunayoishi.

    Ila nashangaa pale wachangiaji waliotangulia wanapoamua kutoona tatizo kwa upeo mkubwa. Ni kweli ulio dhahiri kuwa ni ndugu zetu waislam ndo wanapiga ngoma na taarabu usiku kucha ktk makazi ya watu wakati wa sherehe. Na kwa maeneo ninayoishi huku Pugu si harusi tu zinazokesha, bali binti akifundwa baada ya kuwa " mkubwa" basi ngoma zinakesha. Na ni hao ndugu zetu waislam ndo wanafanya mambo haya.

    Ushauri, kama ilivyo kwny sherehe za ukumbini ambazo zote zatakiwa kuisha saa sita, basi, hawa ndugu zetu waislam wapige hizo ngoma zao za maharusi, au kuchezeshwa mwali huko ukumbini na sio kwny makazi ya watu na mwisho iwe saa sita. Hii ni kuhimiza ustaarabu na kutobughudhi wananchi wengine.

    Yaani kaka wa kigamboni nakushkuru sana kwa maada hii maana ni kero namba moja huku Pugu na nafkiri maeneo mengi ya Dar

    ReplyDelete
  35. Mtoa mada umekosea usitegmee kutatua tatizo peke yako bila ushirikiano wa wananchi wenzako(participation approach) lakini ukiwakashifu ndio baadae utake ushirikiano wao hutofanikiwa hata kama ulikua na nia njema, badilika kwanza wewe mwenyewe ondoa miwani ya mbao ya udini mbeleyako ndio unaweza kuwa na mtizamo sahihi otherwise sote ni watanzania na tunatofautiana kwa mambo mengi.

    ReplyDelete
  36. Zaidi ya fujo:

    Ukeshaji wa Ngoma huleta uharibifu mkubwa kama Zinaa na Ubakwaji na Unajisi vinajiri sambamba na Pombe za Gongo, Bangi na Madawa ya Kulevya kutumiwa hadharani bila woga !

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...