TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Makamu wa Rais wa Malawi, Mheshimiwa Joyce Banda kuomboleza kifo cha kiongozi wa nchi hiyo, Mheshimiwa Rais Bingu wa Mutharika.

Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Banda kuwa Tanzania imepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Rais Bingu wa Mutharika ambaye Rais Kikwete amemwelezea kama kiongozi wa karibu na rafiki mkubwa wa Tanzania.

Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo, “Sisi katika Tanzania tumepokea taarifa za kifo cha Rais Bingu wa Mutharika kwa mshtuko na majonzi. Alikuwa kiongozi na rafiki wa karibu wa Tanzania na rafiki yangu. Alikuwa kiongozi wa kutumainiwa miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la Afrika lote.”

Ameongeza Rais Kikwete: “ Kwa hakika, Afrika imempoteza kiongozi imara, aliyeamini katika maslahi ya Bara letu na watu wake. Siku zote tutamkumbuka kwa dhamira yake na moyo wake katika kupigania umoja, amani, utulivu na ustawi wa mataifa yetu mawili na Afrika nzima.”

“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba yangu mwenyewe, nakutumia wewe Mheshimiwa, familia ya marehemu na wananchi wote wa Malawi salamu za rambirambi za dhati ya mioyo yetu kufuatia kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Rais Bingu wa Mutharika,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
07 Aprili, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...