Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini VETA, licha ya mafanikio makubwa iliyoyapata katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo ujenzi wa vyuo vipya vinne vya kisasa na kukarabati vyuo vya zamani ambapo baadhi yake imevijenga upya, bado inakabiliwa cha changamoto kubwa ya fedha za vifaa kisasa, fedha za uendeshaji, fedha za ukarabati wa vyuo vilivyobakia na fedha za ujenzi wa vyuo vipya kwenye mikao mipya iliyoanzishwa hivi karibuni.
Changamoto hizo, zimetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Eng. Zebadiah Moshi wakati wa kufanya tathmini ya Sherehe za ufunguzi wa Chuo Kipya cha VETA cha Manyara, kilichojengwa chini ya mkopo nafuu kutoka nchini Korea ya Kusini, na kuzinduliwa na Makamo wa Rais, Dr. Mhomed Gharib Bilal mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Eng. Moshi amesema, kwa miaka ya hivi karibuni, VETA imepanuka sana, kwa mwaka wa fedha 2009/2010, vyuo 11 vilipanuliwa miongoni mwake vyuo vya VETA vya Singida, Tabora na Shinyanga vilijengwa upya. Kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011, vyuo 8 vipya vilijengwa na kukamilika, vikiwemo Chuo cha Hoteli na Utalii kilichopo Njiro Arusha, Chuo cha Veta cha ICT kilichopo Kipawa jijini Dar es Salaam na vyuo vya VETA vya Kigoma, Pwani, Lindi, Manyara na Chuo cha Veta wilaya ya Makete.
Eng. Moshi amesema, licha ya ongezeko hilo, kiwango cha fungu la fedha za uendeshaji wa VETA , Skill Development Levy au SDL, kimebakia kile kile cha Asilimia 2% , hivyo VETA imekuwa ikiomba kiwango hicho kiongezwe angalau kifikie asilimia 4% au hata asilimia 6% ili VETA iweze kukidhi mahitaji yake ya kujiendesha kwa ufanishi bila kuathiri ubora mafunzo yanayotolewa na VETA.
Akijibu maombi hayo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Philip Mulugo, amesema, ongezeko la vyuo vya ufundi stadi, kunaleta ongezeko la gharama za usimamizi na uendeshaji wa vyuo vya ufundi nchini, hivyo anaamini huu ni wakati muafaka kwa serikali kupitia wizara yake, kutathmini upya mahitaji ya fedha kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ili iweze kuviendesha vyuo hivi kwa ufanisi mkubwa.
Naibu Waziri amekiri serikali kuyapokea rasmi maombi VETA kuongezewa viwango vya SDL ambayo ni asilimia 2% tuu. na kuahidi kulishughulikia ombi hilo kikamilifu kwa kushirikiana na wizara ya fedha.
Kwa upande wake, Balozi wa Korea Kusini hapa nchini, Bwana Young Kim, amesema nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania mpaka pale ambapo Tanzania itafanikiwa kuzitumia rasilimali zake yenyewe.
Huku akiongea kwa lugha ya Kiswahili fasaha, Balozi Kim alisema Korea inaamini katiika misaada ya kimaendelea kuwawezesha Watanzania kujitegemea na kusema “ Usimpe mtu samaki, bali mfundishe kuvua samaki”.
Chuo hicho cha Veta Manyara, ni miongoni mwa vyuo vipya vinne na vya kisasa, vilivyojengwa kwa mkopo nafuu kutoka nchini Korea uliogharimu Dola za Kimarekani zaidi ya milioni 6 ambapo Korea imegharimia kwa asilimia 80% na Tanzania kuchangia asilimia 20%. Vyuo vingine ni Chuo cha Veta Lindi, Chuo cha Veta Pwani na Chuo cha ICT kilichpo Kipawa jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...