MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora inayosikiliza kesi ya kupinga matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi Dk. Dalaly Kafumu katika Jimbo la Igunga mkoani Tabora kupitia tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika mwaka jana, itaanza kusikilizwa leo na mashahidi 80 wanatarajiwa kufika mahakamani.
Kesi hiyo imefunguliwa na Joseph Kashindye aliyekuwa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya Dk. Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo.
Mahakama hiyo itaanza kusikiliza hoja za msingi zilizoridhiwa na pande zote ili kupata ufumbuzi wa uamuzi ya mahakama hiyo.
Kashindye kupitia kwa wakili wake, Profesa Abdallah Safari amewasilisha mahakamani hoja 15, ambazo miongoni mwake anamlalamikia Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwamba akiwa katika mkutano wa kampeni Kata ya Igulubi, kwa kutumia madaraka yake, aliahidi ujenzi wa Daraja la Mbutu kama wananchi hao watampigia kura mgombea wa CCM.
Aidha, anadaiwa kuwa waziri huyo aliwatisha wananchi wa kata hiyo wasipoichagua CCM daraja hilo halitojengwa na kwamba wasipomchagua Dk. Kafumu watashughulikiwa.
Akiendelea kusoma hoja hizo huku kila hoja ikisomwa ikijadiliwa na kupitishwa kwa pande zote, Profesa Safari alitaja hoja nyingine ni Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Igunga, liliwakataza wasiipigie Chadema pamoja na Rais mstaafu Benjamin Mkapa kutoa ahadi ya kugawa mahindi kwa wananchi wa Igunga siku mmoja kabla uchaguzi ili wakichague Chama Cha Mapinduzi.
Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Mary Shangali, alisema hoja hizo 15 zimekubaliwa kwa pande zote na kesi hiyo itaanza kusikilizwa leo huku ikiwa na mashahidi 80 kutoka pande zote tatu.
Shangali amebainisha kuwa upande wa walalamikaji watakuwa na mashahidi wasiopungua 50 huku upande wa mlalamikiwa unaowakilishwa na Wakili Kamaliza Kayaga wakiwa na mashahidi 20 wakiwamo mawaziri, baadhi ya wabunge ambapo upande wa Serikali watakuwa na mashahidi 10.
CHANZO:HABARI LEO
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...