Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano Kampuni ya bia ya Serengeti Teddy Maounda akizungumza na waandishi wa habari kwenye klabu ya City Sports Lounge asubuhi hii wakati alipotangaza udhamini wa kampuni hiyo kwa tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka inayoandaliwa na chama cha waandishi wa habari za michezo TASWA Kulia ni Katibu Mkuu wa TASWA Amir Mhando na katikati ni Mwenyekiti wa TASWA Juma Pinto
Mwenyekiti wa TASWA Juma Pinto Kulia akitoa shukurani zake kwa kampuni ya bia ya Serengeti kwa kudhamni tuzo hizo mwaka huu, kutoka kulia ni Makamu mwenyekiti wa TASWA Maulid Kitenge, Nandi Mwiyombela Meneja miradi Endelevu SBL na Teddy Mapunda Mkurugenzi wa Mawasiliano SBL.
KAMPUNI ya Bia ya Serengeti imetangaza kudhamini tuzo za Mwanamichezo Bora wa Tanzania Mwaka 2011 kwa sh. Milioni 150, tuzo ambazo zinaandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
Udhamini huo ulitangazwa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano Kampuni ya Bia ya Serengeti Teddy Mapunda, alipokuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye klabu ya City Sports Lounge, Dar es Salaam, ambapo aliambatana na viongozi wa TASWA.
Alisema kampuni yake inaona fahari kuendelea kudhamini tuzo za TASWA ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo, hivyo mwaka huu wameongeza udhamini zaidi ili kuzoboresha.
Alisema tuzo hizo zitafanyika Juni 14 mwaka huu ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP) Dar es Salaam na kwamba wana matumaini makubwa zitakuwa bora kuliko zilizopita.
Naye Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliwashukuru Serengeti na kusema udhamini huo ni ishara ya namna kampuni hiyo inavyothamini wanamichezo hapa nchini na kwamba umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka sh. Milioni 80 za mwaka jana.
Hata hivyo Pinto alisema milango ipo wazi kwa wadhamini wengine kujitokeza kama wadhamini washiriki kwa
vile bajeti ya tuzo hizo ambayo awali chama chake kimepanga ni sh. milioni 370, lakini hata udhamini huo unatosha kufanya kitu kizuri zaidi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema Kamati Maalum ya Tuzo hizo inaendelea na mchakato wake wa kupata wanamichezo hao na kwamba kadri watakavyokuwa wanapiga hatua watatoa taarifa kwa wanahabari.
Kwa miaka mitano iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA walikuwa ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao wote ni wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...