Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Bi. Angela Kairuki akiweka mzigo katika mzani ili kuweka uwiano sawa kama ishara ya uzinduzi wa Wengine kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo Bi. Joaquine De Mello, Balozi wa Denmark nchini Johnny Flento, Jaji Mkuu wa Zanzibar Bw. Omar Makungu na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Bw. Semstocles Kaijage.
Balozi wa Denmark nchini Bw. Johnny Flento akiweka mzigo katika mzani ili kuweka uwiano sawa kama ishara ya uzinduzi wa Mfuko wa Msaada wa Huduma za Kisheria (Legal Services Facility) leo (Alhamisi, Mei 17, 2012) jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Bi. Angela Kairuki, Jaji Mkuu wa Zanzibar Bw. Omar Makungu na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Bw. Semstocles Kaijage.
Kikundi cha Kwaya cha Jaji Mwalusanya kikitumbuiza katika uzinduzi wa Mfuko wa Msaada wa Huduma za Kisheria (Legal Services Facility) leo (Alhamisi, Mei 17, 2012) jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Farida Khalfan wa Wizara ya Katiba na Sheria).
Na Farida Khalfan
Serikali inandaa muswada wa Sheria itakayosimamia shughuli za utoaji huduma za msaada wa kisheria zinazofanywa na Mawakili Jamii (paralegals).
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Bi. Angela Kairuki ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 17, 2012) wakati akizindua Mfuko wa Msaada wa Huduma za Kisheria jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa pamoja na kazi nzuri wanayofanya, wanahitaji msaada wa uratibu kisheria.
Mfuko huu unalenga kuboresha upatikanaji wa haki hususan kwa wanawake, watoto na watu wanaoishi katika mazingira magumu na ni sehemu ya msaada wa Serikali ya Denmark kwa Tanzania katika kuboresha sekta ya sheria.
Naibu Waziri huyo alisema Serikali kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria ilifanya utafiti wa kina kuhusu matumizi ya Mawakili Jamii katika utoaji wa huduma za kisheria ikiwemo kuwawakilisha wananchi katika Mahakama.
“Ninafurahi kuwataarifu kuwa Serikali imepokea taarifa ya utafiti huo hivi sasa inaifanyia kazi kwa lengo la kuwa na sheria itakayowatambua na kuwasimamia Mawakili Jamii (Paralegals) nchini”, alisema Naibu Waziri.
Kairuki alisema uwepo wa sheria hiyo utaongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi wengi zaidi kwa kuwa Mawakili Jamii ni watu wenye elimu ya kawaida na wanapatikana kwa wingi zaidi zaidi nchini kote ikilinganishwa na wanasheria.
Pamoja na uandaaji wa sheria hiyo, Naibu Waziri aliyashukuru mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwa kazi kubwa wanayofanya ya kutoa msaada wa huduma za kisheria kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Kairuki, wananchi wengi kutoka makundi maalum wamekuwa wakipata msaada kutoka katika mashirika haya.
“Wanafanya kazi nzuri sana. Watu wengi wakiwemo wajane, yatima, walemavu na hata wale wanaoishi na virusi vya ukimwi wanategemea msaada kutoka katika mashirika haya,” alifafanua.
Akimkaribisha Naibu Waziri katika hafla hiyo, Balozi wa Denmark nchini Bw. Johnny Flento alisema mfuko huo unaofadhiliwa na serikali ya Denmark una lengo la kujenga na kuboresha uwezo wa watoa huduma za msaada wa kisheria nchini ili kuongeza upatikanaji wa haki.
Kwa mujibu wa Balozi Flento, mafanikio waliyoyapata katika kusaidia mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma za msada wa kisheria, yameitia moyo Serikali yake na kuifanya kukubali kufadhili uanzishwaji wa mfuko huo.
“Uzoefu wetu umeonyesha kuwa msaada wa kisheria na Mawakili Jamii wana ushawishi mkubwa katika kuongeza uwezo wa wananchi kudai na kulinda haki zao na hivuyo kuboresha upatikanaji wa haki,’ alisema Balozi Flento.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo Bi. Joaquine De Mello alisema kwa kuanzia, mfuko huo utajikita katika mambo matatu.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuongeza wigo wa msaada wa kisheria katika wilaya zote nchini; kuboresha ubora wa msaada wa kisheria unaotolewa na kuboresha uratibu katika utoaji wa msaada wa kisheria katika ngazi zote.
Well done Hon. Kairuki and all involved, we all support and behind you - keep it up.
ReplyDeleteDiaspora (UK) - Northampton.