Waheshimiwa Wabunge, 
Napenda kuwafahamisha kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge katika Kikao cha dharura kilichofanyika siku ya Jumatatu tarehe 18/6/2012 iliazimia kufanya mabadiliko ya upitishwaji wa Muswada wa Sheria ya Fedha (The Finance Bill), kwamba badala ya Muswada huo kupitishwa mara baada ya hotuba ya bajeti na bajeti kupitishwa, sasa upitishwe mwishoni kabisa mwa Mkutano wa bajeti wakati bajeti za Wizara zote zitakapokuwa zimepitishwa.

Itakumbukwa kuwa kwa nia njema utaratibu wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha mapema ulianzishwa wakati wa Bunge la Tisa ili kuruhusu mchakato wa ukusanyaji wa mapato ya serikali uanze kuanzia Julai mosi badala ya kutegemea Sheria inayoruhusu mapato yakusanywe hata kama sheria ya fedha haijapita (Provisional Collection Tax).

Hata hivyo utafiti unaonyesha kuwa Mabunge mengi ya Jumuiya ya Madola (Common Wealth) yana utaratibu wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha (The Finance Bill) na Muswada wa Sheria ya Matumizi (Appropriation Bill) mwishoni kabisa wa mjadala wa Bajeti. Lakini tumefuatilia na kubaini kuwa mchakato wa kupitia Bajeti unaanza mapema na kumalizika kabla ya Mwaka wa Fedha mpya kuanza. Mathlani Bunge letu lingepaswa liwe linakutana na kuanza mchakato wa kupitia Bajeti ya Serikali mapema na inapofikia Juni 30 Mkutano wa Bajeti uwe umemalizika na Muswada wa Sheria ya Fedha kuanza kutumika ifikapo Julai Mosi, ambapo mwaka mpya wa Fedha unaanza.
Hivyo basi, kwa kuzingatia ombi la Serikali na Waheshimiwa Wabunge walio wengi pamoja na maoni ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi na kwamba hata pasipo kupitisha Sheria hii bado Serikali inaweza kukusanya mapato, na kwa kuwa, Kanuni ya 106 ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007 bado haikufanyiwa mabadiliko, na kwamba utaratibu wa kupitisha Muswada huu mwishoni utatoa fursa kwa Wabunge kushauri vyanzo vingine vya mapato kutokana na michango ya Wabunge wakati wa mjadala wa Bajeti; na kwa kuwa kwa kujadili Muswada wa Fedha mwishoni tutatoa muda mzuri kwa Kamati na Waziri wa Fedha kujadiliana kwa undani kuhusu Muswada huu kabla ya kuletwa rasmi Bungeni. Vile vile utaratibu huu ulikuwa unatumika zamani na unaendelea kutumiwa na Mabunge mengi ya nchi za Jumuiya ya Madola kama nilivyoeleza hapo juu tumeona ni vema tuendelee na utaratibu wa zamani unaotamkwa na Kanuni za Kudumu za Bunge ili mawazo ya Wabunge wakati wa mjadala wa Bajeti nzima yaweze kuboresha Muswada huo wa Sheria ya Fedha.
Kutokana na mabadiliko hayo, mjadala wa Hotuba ya Bajeti utakuwa wa siku tano (5) badala ya nne (4) ambapo utahitimishwa siku ya Ijumaa tarehe 22/6/2011 na Bajeti itapitishwa siku hiyo. Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2012 badala ya kupitishwa tarehe 22/6/2012 sasa utapitishwa mwishoni mwa Mkutano wa Nane wa Bunge.
Aidha, Kanuni za Bunge zitaendelea kufanyiwa mabadiliko ambayo hatimae yatawezesha Bunge letu lifuate utaratibu wa nchi nyingine kwa Mkutano wa Bunge wa Bajeti kufanyika mapema na kumalizika kabla ya Mwaka wa Fedha mpya kuanza. Hii itawezesha Mkutano wa Bajeti uwe umeisha kufikia Juni, 30.
  
Anne S. Makinda (MB)
SPIKA
 19 Juni, 2013

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 20, 2012

    SAMAHANI KWANINI TUIGE JUMUIA YA MADOLA KWANINI TUSIFANYE KITU KULINGANA NA MAISHA YETU, YA JUMUIA YA MADOLA YAMEPITWA NA WAKATI TUNA WATANZANIA WAMESOMA JAMANI TUFANYE MAMBO KULINGANA NA HALI HALISI YA NCHI YETU NA MAENDELEO YA NCHI YETU

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 20, 2012

    Lakini hii hotuba spika alipaswa kuitoa 19 June 2013 mbona kaitoa mwaka huu au hiyo ni typo at the end of the speech?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...