Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye akizindua shina la wakereketwa wa CCM la Melizine mjini Njombe wakati wa ziara ya kuimarisha uhai wa Chama mkoani Njombe.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye akihutubia mkutano wa hadahara katika kijiji cha Mlangali, Wilayani Ludewa mkoani Njombe, akiwa katika ziara ya kuimarisha uhai wa Chama na kukagua miradi ya maendeleo mkoani humo, jana.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye akicharaza ngoma wakati wa mapokezi yake katika kijiji cha Mlangali mkoani Njombe.
Mama aliyebeba mtoto wakishangilia kwa furaha wakati wa uzinduzi wa tawi la wakereketwa wa CCM la Liwigi, Ludewa mkoani Njombe uliofanyuwa na Nape katyika ziara hiyo.
Msafara wa Nape ukiongozwa na pikipiki wakati ukiingia mjini Njombe kwa ajili ya mkutano wa hadhara na kufungua matawi kadhaa aya CCM.

NA BASHIR NKOROMO, NJOMBE

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, CCM, Nape Nnauye amewananga CHADEMA kwamba aliyewapa wazo la kuanzisha kauli mbiu ya 'Vua gamba vaa gwanda' amewaingiza 'mkenge'.

Alisema, Chadema wameingizwa mkenge kwa kuwa inajulikana wazi kuwa kaulimbiu hiyo ililianzishwa na CCM, kukisafisha chama kiondokane na mafisadi wa aina zote, na kwamba kwa Chadema kuanzisha 'vua gamba vaa gwanda' maana yake wanafanya kampeni ya kubembeleza watu wa aina hiyo wasiotakiwa CCM na Tanzania kwa jumla wahamie kwao.

Nape alisema hayo, jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mlangali, wilaya ya Ludewa mko mpya wa Njombe, akiwa katika ziara ya kikazi katika mikoa mbalimbali kuimarisha uhai wa chama.

"Itakumbukwa, CCM kwa kuwa ni chama halisi cha siasa kwa kutimiza sifa, kinaendelea na mageuzi makubwa ya ndani, yanayoitwa 'Kujivua Gamba', ikiwataka wale wote wanaojihusisha na ufisadi wa ina zote kuondoka ndani ya Chama. Lakini Chadema kwa kujua au kwa bahati mbaya wameamua kupotosha maana halisi iliyo wazi ya zoezi hili kwa kuanzisha operesheni eti ya 'Vua Gamba, Vaa Gwanda'", alisema Nape na kuhoji;

"Je, kwa maana hiyo Chadema kama wamedhamiria hivyo na siyo bahati mbaya, wamemua kuutangazia umma wa Watanzania na dunia nzima kwamba wako tayari kuwapa hifadhi mafisadi wa aina zote ambao ni tishio kwa ustawi wa taifa letu la Tanzania, ili mradi tu wapate idadi kubwa ya wanachama?".

Nape alisema, kama Chadema wangetumia busara wangeanzisha operesheni 'Vua Gamba vaa Uzalendo', kwa sababu hakuna ambaye angeshangaa, kwa kuwa kinachosababisha watu kuwa mafisadi ni kutokana na kukosa uzalendo ndani ya mioyo yao.

"Kumwambia mtu avue nguo ya ina moja avae nguo ya rangi nyingine huo ni upuuzi, maana aina ya nguo inaweza kuwa utambulisho tu, lakini haisaidii kubadili wala kujenga tabia ya mtu kiasi cha kuachana na ufisadi akawa mwadilifu na mzalendo kwa nchi yale toka moyoni, mtu anaweza kuivaa na kuivua wakati wowote, lakini kama watu wakihimizwa kuvaa uzalendo wakauvaa sawa sawa, watakuwa nao mioyoni mwao daima, na hawatauvua muda wowote kama nguo", alisema.

Nape alisema kutokana na hali hiyo Wana-CCM wadilifu wasiwe na wasi wasi kuhusu 'magamba' yanayohamia Chadema, kwa sababu kwa kujiingiza katika kuyaona 'magamba' ambayo yamekubuhu kwa ufisadi kuwa ni mtaji kwao sasa chama hicho kinajichimbia kaburi.

"Wewe umesafiri kwa muda mrefu na gari lako, ukaliona mwendo wake umeanza kuwa wa ndivyo sivyo, ukaamua kuondoa oil chafu kusafisha injini, sasa wakati unasafisha akatokea mtu kuikinga akidhani itamfaa, wewe una hasara gani? si unamuacha tu akahangaike nayo?, alisema Nape.

Katika mkutano huo ambao ulijaa watu licha ya kufanyika kijijini, Nape aliponda operesheni iliyoambana na 'vua gamba vaa gwanda' ya 'Momement for Change-M4C', akisema hiyo ni operesheni ya kukusanya fedha tu, wala siyo ya kuleta mabadiliko kama Chadema wanavyodanganya watu.

Alisema, ni operesheni ya kutafuta fedha, na ndiyo maana kila wanapoitangaza operesheni hiyo, wanachangisha watu fedha ambazo baadaye huwa wachangishwaji hawaambiwi ni fedha kiasi gani kimepatikana.

"Ukinunua kitu ukahitaji fedha iliyobaki si unasema nipatie 'chenji' yangu? sasa wananchi muwe macho, msidhani hiyo ni operesheni ya mabadiliko, ni operesheni ya wanaharakati kutafuta fedha, maana hata wao walishakiri kwamba Chadema ni chama cha harakati na sasa kinajaribu kujitoa kwenye uana harakati kiwe chama cha siasa cha kutafuta kutawala nchi" alisema na kuongeza;

"Lakini nawahaapia, hawa watakuwa wanaharakati kwa muda mrefu sana, itawachulua muda mrefu kuwa chama cha siasa kwa kuwa historia inathibitisha kuwa makundi mengi ya harakati yalichukua miaka mingi sana ndipo yakawa vyama vya ssembuse hawa,watakula fedha zenu mpaka mtachoka", alisema Nape.

Nape jana alitarajiwa kufanyika mikutano mingine ya hadhara katika mkoa wa Njombe kabla ya kujerea Dar es Salaam kwenye maandalizi ya mkutano mkubwa wa CCM wa wajumbe wa mashina, matawi na viongozi mbalimbali wa CCM na wanachama, utakaofanyika kwenye viwanjan vya Jangwani, Juni 9, 2012.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 06, 2012

    Nape ndugu yangu naona inakuwia ngumu kuelewa maana ya Gamba licha kuwa ni kauli ya chama chako...gamba sio nguo....Hv mawaziri wa CCM waliokutwa na kashfa na report ya CAG wakavuliwa Uwaziri na wakaendelea kubaki na ubunge wa CCM hapo wamejivua nini? Huoni kwamba CCM bado ina watu wachafu? Kama CCM ingekuwa safi basi hawa mafisadi wangefukuzwa na uanachama. Mtu akivua Gamba na akavaa Gwanda ni sawa na mtu anayebatizwa/anayeungama ambaye anaapa kuachana na makosa na maovu yake na kukubali kuwa mtu/kimube kipya.

    Napata tabu sana Chama tawala kinapoanza kuwa chama cha Upinzani kabla ya wakati kufika. Au ndio mmeshaona dalili za 2015?

    Watanzania kwa sasa hawadanganyika. Hali mbaya ya maisha kwa sasa, mgao wa umeme, mfumuko wa bei, etc unafikiri nani alaumiwe kama sio Chama Tawala? Au unataka kuniambia nini maana ya CHAMA TAWALA?

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 06, 2012

    CCM WANAFUNGUA MATAWI LEO!! HII INAONYESHA JINSI GANI WALIVYO NA WANANCHI KWANI WALITAKIWA WAWE NA MATAWI NCHI NZIMA TANGU TUPATE UHURU HADI LEO! HIZI NI PROPAGANDA AMBAZO SIDHANI ZINASAIDIA CHAMA. WANAOTAKIWA KUFUNGUA MATAWI NI VYAMA VYA UPINZANI! CCM WAONGEZE WANACHAMA KUTOKA VIZAZI VIPYA I.E VIJANA WANAOTIMIZA MIAKA 18 KAMA WAPO TAYARI KUJIUNGA NAO. WENGINE WANAHAMA CCM KUTOKANA NA UBABAISHAJI ULIONZIA MWAKA 1995 HADI SASA. NINA MAANA BAADA YA KIPINDI CHA MTAKATIFU NYERERE!!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 06, 2012

    Uchaguzi wa jimbo wazi la Bahi lini maana huyo kimeshamnukia. Nataka kwenda kugombea kama mgombea binafsi. Je mtanipa????

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 06, 2012

    Mara ghafla li-CHADEMA linatokezea... CCM mtaisoma!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...