Na Jackline Swai, Arusha.
SHIRIKA lisilo la kiserikali la PSI Tanzania ambalo linajishughulisha na usambazaji wa bidhaa za huduma ya afya nchini , limezindua rasmi mafunzo kwa wasambazaji wa bidhaa za familia mjini hapa ambapo mafunzo hayo yatafanyika nchi nzima.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa ushirikiano kutoka shirika hilo, John Wanyancha wakati akizindua mafunzo hayo kwa wasambazaji zaidi ya 50 kutoka maduka mbalimbali ya dawa yaliyopo mkoani hapa.
Alisema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wasambazaji hao juu ya bidhaa za familia ili waweze kutoa huduma nzuri kwa wateja wao na kuweza kujua njia rahisi za upatikanaji wake.
Alisema kuwa, utafiti uliofanywa na taasisi ya takwimu mwaka 2004 unaonyesha kuwa asilimia 6 tu ya wanawake Tanzania ndio walikuwa wanatumia uzazi salama, huku kwa mwaka 2010 takwimu zikionyesha kuwa asilimia 27 ya wanawake Tanzania ndio wanaotumia njia za uzazi salama .
Wanyancha alisema kuwa , bado elimu juu ya matumizi ya uzazi salama kwa wanawake inahitajika kwa kiasi kikubwa sana kwani takwimu hizo zinaonyesha kuwa bado mwitikio wa wanawake wanaotumia njia za uzazi salama ni mdogo sana hali ambayo ni hatari sana.
‘Ukiangalia takwimu za kiulimwengu ni asilimia 54 tu wanawake ndio wanatumia uzazi salama ,hivyo ni jukumu letu kuendelea kuwaelimisha wasambazaji wa bidhaa zetu ili waweze kuboresha huduma zao pamoja na kuwashawishi wanawake kujitokeza kwa wingi kutumia uzazi salama kwa manufaa yao’alisema Wanyancha.
Alifafanua zaidi kuwa, kutolewa kwa mafunzo hayo kutasaidia kwa kiasi kikubwa sana wasambazaji hao kuweza kupata elimu hiyo na kuweza kutoa elimu hiyo kwa wale wote wanaowahudumia na hatimaye idadi ya wanaotumia uzazi salama kuweza kuongezeka .
Wanyancha aliongeza kuwa, mafunzo hayo ndio ya kwanza kuzinduliwa hapa nchini ambapo watatoa mafunzo hayo kwa wasambazaji na watoa huduma ya bidhaa za familia katika mikoa yote hapa nchini lengo likiwa ni kuwafikishia huduma hiyo kwa njia rahisi na haraka.
Aidha alitoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi kujifunza umuhimu wa kutumia njia za uzazi salama kwani zimedhibitishwa na watu wengi na zimekuwa zikisaidia kwa kiasi kikubwa sana kupanga uzazi wa mpango ulio salama na hazina madhara yoyote .
Aidha alisema kuwa, ni vizuri wanawake wote wanaotaka kutumia njia hizo za uzazi salama kuhakikisha kuwa wanapata kwanza ushauri kwa wasambazaji wa bidhaa hizo katika maduka mbalimbali ya dawa ili kuweza kupewa njia sahihi za kutumia bidhaa hizo.
Naye mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo, Bariki Mushi alisema kuwa mafunzo hayo yatamwezesha kuweza kutoa huduma iliyo bora kwa wateja wao na kutoa elimu mbalimbali ya uzazi wa mpango na hatimaye kuweza kuzitumia kwa manufaa yao.
Alisema kuwa, kitendo cha kupatiwa elimu hiyo kitawezesha sana kuboresha utendaji kazi wa wasambazaji wa bidhaa hiyo katika maduka mbalimbali ya madawa na kuweza kutoa huduma iliyo safi na salama zaidi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...