Ubao ukionyesha namna  kila nchi ilivyopiga kura wakati   Baraza  Kuu la  Umoja wa Mataifa, lilipokutana siku ya Ijumaa kulipigia kura Azimio liliwasilishwa na Saudi Arabia. Azimio   ambalo pamoja  na mambo mengine lilikuwa linajaribu kutoa shinikizo  kwa utawala wa Syria kuacha matumizi ya silaha dhidi ya wananchi wake, lakini wakati huo huo Azimio hilo  kutoonyesha  ukali wowote kwa  upande wa Upinzani, vikundi vya kigaidi au nchi ambazo zimekuwa zikiwapatia wapinzani silaha. Azimio hili limepitishwa kwa kupigiwa kura ambapo nchi 133 zimeunga mkono, 12 zimepiga kura ya hapana huku 31 zikipiga kura ya kutofungamana na upande wowote.  nchi ambazo zimepiga kura ya hapana na zile ambazo  hazikufungamana na upande wowote baadhi zimeeleza kwamba zimechukua hatua hiyo kutokana na ukweli kwamba azimio hilo  limeegemea zaidi upande mmoja, lakini pia lilikuwa linaingilia masuala  ya ndani ya nchi huru jambo  ambalo ni kinyume na  sheria za kimataifa.
 
=========  =========  ======== ========
 
UMOJA WA MATAIFA WAJARIBU TENA KUIBANA SYRIA
 
Na Mwandishi Maalum

 Ikiwa ni wiki mbili zimepita  tangu Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kupitisha azimio ambalo lingeongeza kibano kwa  utawala wa Syria,  jana ( Ijumaa) Baraza   Kuu  la Umoja wa Mataifa,  limepitisha azimio jingine ambalo  licha ya kuibana serikali ya Syria lakini pia  limeitupia lawama Baraza Kuu la Usalama kwa kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Azimio hilo  ambalo limeandaliwa na  Saudi Arabia na washirika wake wengine, limepitishwa  ikiwa  pia ni siku moja, tangu  Bw. Koffi Annan alipotangaza kujiuzulu wadhifa wake wa kuwa  Mjumbe  maalum  wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  na Muungano wa Nchi za Kiarabu katika mgogoro wa Syria.  Azimio hilo limepitishwa  kwa kupigiwa kura ambapo nchi 133 zilipiga kura ya ndiyo, 12 zikapiga kura ya hapana na  nchi 31 zikapiga kura ya kutofungamana na upande wowote.

Pamoja na kupitishwa kwa azimio hilo,  lakini linakosa nguvu ya kisheria kwasababu, kwa utaratibu wa Umoja wa Mataifa, mara nyingi maazimio yanayopitishwa na  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa  yanakuwa  ya kisiasa zaidi na hayana nguvu kama  yale yanayopitishwa na Baraza Kuu la Usalama.Azimio hilo ambalo  limeinyosheza kidole zaidi serikali ya iliyoko madarakani  kuliko upande wa  upinzani. Linaalani vikali pamoja  na mambo mengine,matumizi ya silaha nzito  ikiwamo mizinga na helikopta za kivita na mauaji holela ya  wananchi wasio kuwa na hatia.

Aidha  azimio hilo linaitaka serikali iliyopo  madarakani kurudisha nyuma vikosi vyake na vifaa vya kijeshi kutoka maeneo ya raia, lakini halitamki lolote kuhusu makundi ya upinzani ambayo nayo yamekuwa yakitumia silaha nzito ikiwa ni pamoja na  mauaji.

Awali akizungumza kabla ya kupigwa kwa kura, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, aliwasihi wajumbe wa Baraza kuliunga mkono kwa kauli moja azimio hilo. Akasema  kuwa sauti ya pamoja na Baraza hilo inaweza siyo tu kupeleka ujumbe  kwa watawala wa Syria lakini pia itaongeza shinikizo la kuwataka watawala  na pande nyingine zinazohusika  kurejea katika meza ya mzungumzo.

Akasema  Ban Ki Moon. “ Mgogoro wa Syria ni mtihani mwingine kwa Umoja wa Mataifa, kwamba, kushindwa kwa Taasisi hiyo ya kimataifa kuutafutia  ufumbuzi mgogoro huo ni  hatari na hakutatoa ujumbe mzuri”

Akasititiza kwamba Umoja   Mataifa usingependa kushuhudia yale yaliyotokea Rwanda au Sebrenica kwasababu tu Umoja huo ulishindwa kuchukua hatua kwa wakati muafaka.  Akasisitiza kwamba machafuko na mauaji ya kiholela ya wananchi wasio na hatia nchini Syria  yanaweza kuchukuliwa kama ukiukwaji wa haki za binadamu na makosa ya jinai dhidi ya binadamu  ambapo wote watakaopatwa na hatia watapashwa kuchukuliwa hatua za kisheria bila kujali ni wa upande gani.

Ban Ki Moon akasema   ni jambo la kushangaza na kusikitisha sana kwamba pande zinazopingana zimeamua kutumia njia ya vita kila mmoja  akiamini kwamba kwa njia hiyo anaweza kushinda, lakini ukweli ni kwamba hakuna mshindi  zaidi ya wananchi wasio na hatia kuendelea kuangamia.“ Sisi sote tuliopo hapa tunawajibika kwa wananchi wa Syria,  ni lazima tutumie njia za amani kama zinavyoelezwa katika   Katiba ya Umoja wa Mataifa, ili kuaanda mchakato wa upatikanaji wa amani ambao utawahusisha wananchi wenyewe wa Syria”.  Akasisitiza Ban Ki Moon.

Nchi ambazo zimepiga kura ya hapana au ya kutofungamana na upande wowote  baadhi zilieleza kwamba zimefanya hivyo  kwa sababu moja kuu ya msingi ambayo ni, Azimio  hilo lilikuwa limeegemea upande mmoja, lakini pia zilikuwa zinapinga   uingiliaji wa mambo  ya ndani ya nchi nyingine  jambo ambalo ni kinyume si kama inavyoelezwa katika  Katiba  ya Umoja wa Mataifa bali hata katika sheria mbalimbali za  Kimataifa.

Aidha nchi nyingine zimeeleza bayana kwamba hazikuunga mkono azimio hilo kwa kuwa,  wakati  mataifa mengine yamejikita katika kuilamu na kuilaani serikali ya Syria, lakini  zilikuwa hazisemi lolote kuhusu baadhi ya mataifa ambayo  yamekuwa yakisaidia  kwa hali na mali ikiwa ni pamoja na kuvipatia silaha  vikundi vya upinzani hali ambayo imechochea zaidi mgogoro huo badala ya kuutatua.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Kabla ya Umoja wa Mataifa (United Nations Organization) tuliokuwa nao leo dunia ilikuwa na League of Nations, umoja/ushirika huu ulindwa kutuliza amani ya mataifa ambayo kimsingi ndio jukumu kubwa la uanzish=shwaji wake. Ilivyokuwa UNO nayo jukumu hilo imeshindwa kulitekeleza sasa kuna haja kubwa (sio choo) ya kuanzishwa umoja mwingine wa mataifa ambao utatupilia mbali masuala ya kura ya veto! Hivi leo Syria inashambuliwa na waasi wenye silaha ambazo zinatolewa na Marekani lakini yenyewe inaambiwa eti iache kuwashambulia hao waasi,yaani iache kujilinda, sasa wafanyeje? Huu si ni upuuzi jamani?

    ReplyDelete
  2. Haswaa ni upuuzi, miye hata sielewi malengo ya hawa wakubwa. Somalia walikuwa na amani mwaka 2006, marekani kwa kuwa waliokuweko madarakani kipindi hawakuwa vibaraka wao wakawatumia Ethiopia kusambaratisha nchi. Sasa wanasema kuna al-shaabab, wakati hawa ni wale ambao walikuwa wameunda serikali mwaka 2006 na ambao marekani hawakuwataka.Nasikia pana mafuta na gesi hapo somalia na waheshimiwa wameshaanza kuyafanyia kazi.Sielewi siye hapa nchini kwetu tutakaposema wazee faida izidi sisi kwani ni masikini kuliko nyie na nyie matajiri sana..., sijui kama hawatasema Tanzania ni nchi ya kishenzi... na kutaka kuivamia...

    ReplyDelete
  3. aMERIKA INACHOCHEA WA-sYRIA WAUANE BURE BADALA YA KUWAKUTANIISHA KWA SABABU WANATAKA REGIME XHANGE! eTI REGIME CHANGE.! hAWAMTAKI HUYO rAIS WA sYRIA TU NA WANAMWUA KWA NJIA ZOZOTE. sASA ciaNDIO WANAOPIGANA VITA HIYO!

    ReplyDelete
  4. Na sisi tusipotaka ushoga watatuvamia. Dunia imeisha!!!!!"""

    ReplyDelete
  5. Change ime fika Tanzania. Mambo yana badlika kidogo dogo watu wame lala. Una ona vipi Rais na safari zake za kisiri siri Merikani. Ufisadi tu. Sasa hana laku sema.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...